The House of Favourite Newspapers

Za Chembe kwa Young D, Kuhusu Matumizi ya ‘Unga’

young-dee1BONGO Fleva hivi sasa ni muziki unaolipa, unawatoa vijana wengi wadogo ambao baada ya ku-hit na nyimbo moja au mbili tu, tayari wanatengeneza mkwanja mrefu kuliko kaka na dada zao waliotumia miaka mingi huku wakitoa albamu kadha wa kadha.

Kuna huyu mdogo wangu mmoja, anaitwa David Genzi, lakini ni maarufu sana kama Young D. Ninafuatilia kazi na mambo yake, anafanya vizuri na kama anaweza kushikilia hapo alipo, wazungu wanasema ku-maintain, anaweza kufika mbali hasa kwa kutilia maanani umri wake ulivyo mdogo.

Kuna wasanii wengi waliingia katika hii fani wakiwa wadogo kiumri, mfano akina Dully Sykes, Mr Blue, Abby Skills, Dogo Hamidu (Nyandu Tozi) kwa mifano ya wachache, lakini bahati mbaya kwao ni kuwa waliukuta muziki ukiwa bado ni wa kupata sifa na hela kidogo ya kula. Ndiyo, kwa umri wao wakati ule, uliwasaidia maana leo, wale walio-maintain, Dully na Mr Blue kwa mfano, wanakutana nazo, ingawa siyo kwa kiwango wanachostahili.

Young D anakuwa katika kundi moja na vijana wenzake wengi, akina Young Killer, Mo Music, Harmonize, Raymond na wenzao wa kizazi chao. Wanafanya muziki na unawalipa kama ambavyo huyu dogo alivyofanya, aliwahi kukomboa nyumba yao iliyokuwa ikisubiri kupigwa mnada na benki baada ya familia kukopa ili kumuuguza baba yake, ambaye bahati mbaya alifariki dunia.

Lakini pia kwa maneno yake mwenyewe, aliwahi kununua gari kwa pesa ya muziki, kitu ambacho hakuwahi kufikiria kama angeweza. Kwa kijana wa Kibongo wa umri wake, unaona kabisa kuwa ni mtu mwenye maono, mipango na malengo. Big up sana kwake.

Lakini kuna upande mmoja bwa mdogo anakuja ndivyo sivyo. Bahati nzuri aliwahi kukiri mwenyewe kuwa ni kweli alikuwa anabwia unga, akawaomba radhi mashabiki wake na kuahidi kuachana na tabia hiyo ya kijinga.

Lakini majuzi, mmoja wa watu waliomsaidia, ambaye amekuwa kama mfadhili wake, alitangaza kuachana naye baada ya msanii huyo kurudia ‘kula unga’.

Ni habari isiyopendeza, hasa kwa kijana mdogo kama Young D. Mimi najua anaiga, hasa baada ya kuwakuta ‘kaka zake’ wakitumia hiyo kitu, kwa umri wake, anadhani ni starehe kama starehe zingine anazojifunza, kama kunywa pombe labda na wanawake.

Nasisitiza zaidi kuwa huyu dogo anaathiriwa na umri na pengine ulimbukeni. Ninaamini amekulia katika familia ya kimasikini, anaujua msoto. Sasa ghafla leo kuwa mtu mwenye uwezo wa kupata fedha nyingi kwa mara moja, anadhani maisha yako hivyo siku zote.

Kwa vile ninamtakia heri, nimsihi aachane na madawa kwa sababu inawezekana. Aache kula unga kwa vile hautamsaidia, utamporomosha na atakuwa na maisha mabaya kuliko hata aliyowahi kuishi kabla.

Aache ulimbukeni, watoto wajanja huiga yaliyo mema, kama anadhani yeye ni staa mkubwa, anajidanganya. Na asije kufikiri kununua gari ndiyo kuyapatia maisha. Gari anaweza kuliuza dakika moja tu na kitakachobaki ikawa historia.

Ana muda mzuri wa kuwa mmoja kati ya matajiri wakubwa Afrika kupitia muziki. Kuna starehe nyingi nzuri, unatumia fedha na akili inazunguka kuona namna gani ya kuongeza kipato.

Asimkufuru Mungu kwa nafasi aliyompa. Kuna vijana wenzake kwa mamilioni mtaani wanaitafuta bahati kama yake, yeye kaipata anaanza kula unga, acha mara moja dogo.

Anaandika Ojuku Abraham | Gazeti la Ijumaa, Toleo la Januari 13, 2016

Comments are closed.