The House of Favourite Newspapers

YUDA THADEY: Mlemavu Anayeushangaza Ulimwengu

0

NA WAANDISHI WETU, UWAZI, HABARI

UKIFIKA Wilaya ya Mwanga maeneo ya Ugweno mkoani Kilimanjaro, jina la Yuda Thadey George ni maarufu na kila kijana lazima anatambua uwezo na kipaji alichonacho mlemavu huyo aliyepooza kuanzia sehemu ya kiuno hadi miguuni, hivyo kushinda akiwa amelala tu.

Yuda aliliambia Uwazi kuwa wakati mwingine anafanya kazi akiwa kitandani kwa muda mrefu kwani anapoanza jambo lake hataki lilale, lazima ahakikishe analimaliza ndipo anaendelea na kitu kingine kitu ambacho kinawashangaza watu mbalimbali wanaofika kijijini hapo wakiwemo wa kutoka nje ya nchi.

 

Thadey George akiwa na familia yake.

NI FUNDI MAHIRI

Mlemavu huyo anawashangaza walimwengu kwani ni mahiri katika utengenezaji wa vifaa vyote vya umeme kama simu, kompyuta, redio, runinga, pia ana uwezo wa kuhariri video na kurekodi.

Yuda pia anaweza kutayarisha muziki wa aina yoyote japokuwa kabobea zaidi katika Muziki wa Injili ambao anaupenda kwa sababu ameokoka.

 

HISTORIA YAKE

Akielezea historia yake, Yuda alisema alizaliwa mwaka 1973 akiwa mzima kabisa na kulelewa vizuri na wazazi wake, akiwa darasa la tatu ndipo alipopata matatizo.

MTI WA MZAMBARAU

Akifafanua zaidi, alikuwa na haya ya kusema: “Mwaka 1985 nikiwa darasa la tatu nilipata ajali ya kuanguka kutoka juu ya mti niliokuwa nachuma zambarau. Baada ya kuanguka nilikimbizwa katika Hospitali ya Kifura lakini kutokana na hali yangu kuwa mbaya nilihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi ambako madaktari walibaini nilivunjika uti wa mgongo.

 

“Nililazwa hospitalini hapo kwa miezi mitano hali ikawa bado mbaya nikahamishiwa katika Hospitali ya KCMC lakini kutokana na uhaba wa fedha wazazi hawakumudu gharama, hivyo nilirudishwa tena Mawenzi.

“Baadaye nilirudishwa nyumbani kwetu Ugweno huku madaktari wakishauri niwe nahudhuria mazoezi katika Hospitali ya Mawenzi lakini kutokana na hali duni ya maisha waliyokuwa nayo wazazi wangu, ilishindikana baada ya kutokea tatizo lingine la kiafya.

 

KUVUNJIKA MGUU

“Siku moja asubuhi nikiwa bado na hali hiyo mbaya, nilipokuwa nafanya mazoezi mepesi kama nilivyokuwa nimeshauriwa na madaktari, nilianguka na kuvunjika mguu, nikawa kitandani tena.

“Baada ya kuvunjika mguu nilipelekwa katika Hospitali ya Kifura ambako nililazwa tena kwa miezi minne, kisha nikaruhusiwa kurudi nyumbani lakini hata hivyo, baada ya mwaka mmoja nilivunjika tena mguu wa pili nilipokuwa naamka kitandani.

ASHINDWA KWENDA SHULE

“Nikiwa nyumbani baada ya kushindwa kuendelea na shule, baba yangu aliwatafuta walimu walionifundisha kusoma vitabu na magazeti, jambo ambalo lilinisaidia kwani nilikuwa mtundu sana hivyo nikaanza kutengeneza saa, redio na televisheni nikiwa nimelala.

ALIPENDA NINI MAISHANI?

“Maishani mwangu nilikuwa napenda kuwa mtangazaji, naona ndiyo maana nikawa fundi redio na ujuzi huu nilifundishwa na jirani yangu, mzee Juma ambaye kwa wakati huo alikuwa akitumia majina ya vifaa ambavyo si halisi, hivyo kwa sababu napenda kusoma niliweza kufahamu vifaa hivyo vinaitwaje kitaalamu.

“Mimi pia ni mwalimu wa muziki wa aina zote, naweza kutunga mashairi, naimba, napiga kinanda, gitaa na kurekodi japo kwa sasa sitaki kuimba kwani nikiimba napata shida ya kuumwa kifua, nahisi ni kutokana na kutumia nguvu wakati wa kufungua televisheni au redio ninapotaka kuvitengeneza.

“Hivi sasa nasumbuliwa sana na kifua kutokana na kutengeneza vitu nikiwa nimelala.

UGONJWA WA U.T. I

“Pia huwa naugua ugonjwa wa U.T.I mara kwa mara kutokana na mpira ambao nimefungwa kwa ajili ya kujisaidia unapoingia katika dumu ambalo linapokea mkojo linapojaa na kukosekana mtu wa kuumwaga hurudi katika mpira.

OMBI KWA JPM, WATANZANIA

“Namuomba Rais Dk. John Magufuli au Mtanzania yeyote kunisaidia kuninunulia solar na kujengewa studio ili niwe na kazi moja tu ya kuwafundisha vijana wengi ujuzi nilionao kwani ufundi ni sekta ambayo mtu anaweza kujiajiri na kuwa sehemu ya kupunguza tatizo la ajira.

ANA FAMILIA?

“ Nina mtoto wa kike aitwaye Yustina niliyerithishwa akiwa mdogo kwa sababu mama yake ana tatizo la ugonjwa wa kuanguka. Lakini kazi hii inanisaidia mimi na familia yangu kwani wazazi ni wazee.”

Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii ya Yuda na ana chochote cha kumsaidia awasiliane naye kwa namba 0753 495 178- Mhariri.

Leave A Reply