The House of Favourite Newspapers

Za Chembe: Man Fongo kwa Staili Hii Utapotea Aisee!

JINA lake halisi anaitwa Amani Fongo lakini wengi wanamjua zaidi kwa jina la Man Fongo, msanii wa Singeli ambaye anabamba sana kutokana na umahiri wake katika muziki huo unaopendwa zaidi Uswazi.

Amefanya kazi kubwa, mitaa yote inamjua na hajafika hapo kwa bahati mbaya! Juhudi na kujituma ndivyo vilivyomfikisha hapo alipo leo.

 

Namfahamu Man Fongo kabla hajawa msanii mkubwa, enzi hizo ‘akihaso’ kutafuta njia ya kutokea, kitaa cha Kwa Ali Maua na Tandale. Hata alipokuja kutoboa na ngoma yake ya Hainaga Ushemeji iliyogeuka kuwa ‘wimbo wa taifa wa masela’, sikushangaa kwa sababu tayari nilishakiona kitu kikubwa ndani yake.

Kwa waliowahi kukaa karibu na Man Fongo, watakubaliana na mimi kwamba kwa kipindi kirefu alikuwa akisifika kwa heshima, adabu, kutokuwa na majivuno na upole! Japokuwa amekuwa akiishi maisha ya ‘kisela’, ilikuwa vigumu kumhusisha na matukio ya kihuni tofauti na vijana wengine wa rika lake!

 

Hata hivyo, baada ya jina lake kuwa kubwa na kupata ustaa, kuna mambo yameanza kubadilika kwa Man Fongo. Yamekuwepo madai ya Man Fongo kuanza kuishi ‘kisanii’, ameanza kuwa mjanjamjanja, ameanza kupoteza uaminifu, skendo za ajabuajabu zimeanza kumtafuna na pengine ameshalewa na mafanikio kiduchu aliyoyapata!

 

Desemba 9, 2016, Man Fongo na msanii Zuwena Mohamed ‘Shilole’ walipata shavu la nguvu kwenda kufanya shoo nchini India! Kipindi hicho Hainaga Ushemeji ndiyo imepamba moto. Wengi walishangaa iweje Man Fongo apate shavu hilo la kwenda India kirahisi namna hiyo wakati ndiyo kwanza alikuwa ameingia kwenye gemu?

 

Kwa Man Fongo kukwea pipa mpaka India halikuwa jambo dogo! Hata hivyo, baadaye imekuja kuibuka skendo kubwa kuhusu safari hiyo! Benard Luta ‘Ben Gang’ ni promota aliyeandaa safari hiyo na ni yeye ndiye aliyewatafuta Man Fongo na Shilole.

Wakiwa India, kuna jambo lilitokea kati yake na promota huyo. Ifahamike kwamba mbali na kuwa promota, Ben Gang pia ni msanii wa muziki wa Hip Hop, mwandishi wa mashairi na prodyuza.

 

Wakiwa kwenye ziara hiyo ya kimuziki nchini India, Ben Gang anaeleza kwamba alimsikilizisha Man Fongo moja kati ya kazi zake nyingi alizoziandaa kwa mkono wake! Alifanya

 hivyo kwa kuamini kwamba yupo na ‘home boy’, mwana, akawa ni kama anataka kusikia maoni kutoka kwa Man Fongo kuhusu ngoma hiyo.

 

Cha ajabu ni kwamba, Man Fongo na Shilole waliporejea Bongo, kwa kuwa Ben Gang alikuwa akiishi India, jamaa aliamua kuleta ujanjaujanja! Kumbe wakati wanaondoka India, Man Fongo ‘alichukua’ flash iliyokuwa na kazi kadhaa za Ben Gang, ikiwemo ile aliyomsikilizisha Man Fongo, ambayo mwenyewe aliipa jina la Naogopa!

Man Fongo akaingia studio na kuirekodi fasta ngoma hiyo ya Naogopa na kuipa jina la Lau Nafasi, yaani ukisikiliza ngoma zote mbili, ni copy and paste isipokuwa yeye ameongeza ladha ya singeli tu!

 

Kwa kupitia meneja wake aitwaye G-Maker, Man Fongo amekuwa akikanusha tuhuma hizo na kudai kwamba ‘eti’ waliandika pamoja mashairi ya wimbo huo na alichokifanya yeye ni ‘kuwahi’ tu kuingia studio na kurekodi.

Ukilitazama sakata hili kwa jicho la tatu, unagundua kwamba Man Fongo ameanza kubadilika kitabia! Kwa wenzetu, kesi kama hii unapelekwa mahakamani na unalipa fidia ya mamilioni ya fedha na jina lako linachafuka kabisa, kwa hapa Bongo inaonekana kama ni ishu ya kawaida tu.

 

Juzikati kulizuka tetesi nyingine kwamba Man Fongo amekamatwa na kutupwa selo kwenye Kituo cha Polisi Ali Maua, kwa madai ya ‘kuchikichia’ mkwanja wa mtu, yaani kapewa fedha akafanye shoo akaleta ujanjaujanja! Hata kama madai haya si ya kweli, jina lako linapoanza kutajwatajwa kwenye ishu kama hizi, hiyo ni dalili mbaya!

 

Achana na hayo, yapo madai kwamba Man Fongo anashinda kwenye ‘maskani’ moja ya wahuni mitaa ya Shule ya Sekondari ya Mama Salma Kikwete, watu anaoshinda nao wana sifa moja kubwa, wanakula ‘ndumu’ kama hawana akili nzuri! Sitaki kusema kama na yeye anakula nao kwa sababu sina ushahidi wa hilo, lakini unapokaa na watu wa aina fulani, jamii itakutafsiri kwamba na wewe ni walewale!

Kama kweli una njaa ya mafanikio, haya unayofanya Man Fongo sio siri unazingua na nakuhakikishia usipobadilika, itakuwa ngumu sana kwako kuendelea kuwa juu! Ni wakati sasa wa wewe pamoja na menejimenti yako, kukaa na kuangalia mmekosea wapi, bado unayo nafasi ya kufanya makubwa kwenye gemu lakini hilo litawezekana kama utaachana na hizo mishe zako ambazo sizo!

 

 HASHI-POWER | IJUMAA

Comments are closed.