The House of Favourite Newspapers

Zahera azuia safari ya Yanga Kigoma

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mkongoman, Mwinyi Zahera, ameukataa mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United.

Yanga ilitarajiwa kwenda mkoani Kigoma kwa ajili ya mchezo huo uliopangwa kuchezwa keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.

Akizungumza na Championi Jumatatu, mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema mchezo huo hautakuwepo tena baada ya kocha kuzuia mechi hiyo huku akimtaka msaidizi wake Mzambia, Noel Mwandila kuendelea na programu ya mazoezi.

 

Saleh alisema, kocha ametaja sababu ya kwanza umbali wa safari kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma kwa njia ya basi, usafiri ambao ulipangwa ambao kiafya siyo vizuri kwa wachezaji.

Alitaja sababu ya pili kuwa Singida ni wapinzani wanaotarajiwa kukutana nao hivi karibuni kwenye Ligi Kuu Bara, hivyo ni ngumu kucheza mechi hiyo kwa hofu ya kutibuliwa mbinu zao mara watakapokutana.

 

“Kiufundi siyo sahihi kucheza na wapinzani wetu tunaotarajia kukutana nao katika ligi hivi karibuni, kwani watatujua mapema kabla ya kukutana nao, hivyo kocha akashauri tuachane na mechi hiyo.

“Hao Singida kama wanataka kucheza na Yanga, basi wasubirie tutakutana kwenye ligi, kocha hataki kuona mbinu zikijulikana na wapinzani wake mapema kabla ya kukutana nao.

 

“Pia, kiafya siyo sawa kama unavyofahamu tayari tuna wachezaji watatu wamepata nafuu ya majeraha yao wanaotarajiwa kuanza mazoezi kesho (leo) ambao ni Makambo (Heritier), Abdul (Juma) na Mahadhi (Juma), hivyo tunahofia kujitonesha na kupata majeruhi wengine wapya,” alisema Saleh.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.