The House of Favourite Newspapers

Zahera: Mapema tu Sibomana, Balinya wanamaliza shoo

Kocha Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera.

ACHANA na presha waliyokuwa nayo wapinzani wao, Township Rollers ya Botswana, unaambiwa Kocha Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera amepanga kumaliza shoo ndani ya dakika 10 za mwanzo za mchezo.

 

Mabosi wa Rollers hivi sasa wanahaha kuhakikisha wanawaondoa Yanga kwa kutumia njia ya hujuma ikiwemo iliyokataliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ambalo liliandikiwa barua ya kubadili uwanja kabla ya kukataliwa ombi lao.

Hivyo, washambuliaji wa Yanga wakiongozwa na Juma Balinya, Patrick Sibomana, Sadney Urikhob wana kibarua kigumu cha kuhakikisha wanafanyia kazi maelekezo ya kocha wao.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Zahera alisema kuwa kikubwa anataka kuona timu yake inapata bao la mapema na ndani ya dakika 10 za mwanzo wawe wanaongoza. Zahera alisema kuwa katika mchezo uliopita uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar, wachezaji walishindwa kucheza kwa kufuata maelekezo yake na kusababisha watoke sare hiyo ambayo ni mbaya kwao.

“Katika mchezo huu ninataka tucheze kwa malengo, kwani ni lazima tushinde kama kweli tunataka kusonga mbele kwenye mashindano haya makubwa Afrika na hilo linawezekana kwetu kutokana na maandalizi niliyoyafanya.

 

“Kama tuliweza kufunga bao tukiwa nyumbani kwa nini tushindwe kufunga hapa ugenini, kikubwa kinachotakiwa ni kucheza kwa tahadhari ya kuwahofia wapinzani wetu ambao nao wapo vizuri,” alisema Zahera.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.