The House of Favourite Newspapers

Zahera: Simba Wana Kikosi Hatari Msimu Huu

0

KOCHA wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa anahudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi wa Gwambina, Mkongomani Mwinyi Zahera, amefunguka kuwa Simba wana kikosi cha hatari msimu huu kutokana na kuwa na timu yenye wachezaji wenye vipaji vikubwa.

 

Zahera ambaye alihudumu kama kocha wa Yanga kwa kipindi cha msimu mmoja na nusu, aliyasema hayo muda mfupi baada ya kushuhudia kikosi chake kikipoteza baada ya kucheza na Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.Kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar, Gwambina ilikubali kipigo cha mabao 3-0.

Mabao ya Simba yalifungwa na Meddie Kagere, Pascal Wawa na Chris Mugalu.Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema Simba ina kikosi cha wachezaji wengi ambao wana vipaji vikubwa jambo ambalo linaweza kumuweka kwenye hatari mpinzani yeyote wanayekutana naye.

 

“Ni jambo lisilopingika kuwa Simba msimu huu imejipanga kufanya mambo makubwa kutokana na ubora wa kikosi chao ulivyo.

 

“Kabla ya mchezo dhidi yao tulikaa na wachezaji wetu na kuwaambia kuwa tunakwenda kucheza dhidi ya timu bora zaidi ya zile tulizocheza nazo hapo awali hasa kwa kulinganisha uwezo wa mchezaji mmojammoja.

 

 

“Kwa upande wangu nadhani miongoni mwa michezo yetu minne iliyopita huu ndiyo mchezo pekee ambao unaweza kusema tulistahili kupoteza kwa sababu tulizidiwa lakini kwenye michezo mitatu iliyopita tulicheza vizuri lakini hatukuwa na bahati ya kupata mabao,” alisema Zahera

STORI: SAID ALLY NA JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave A Reply