The House of Favourite Newspapers

Zahera: Tutalipa Fedha Kuwafunga Rollers

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amefunguka kuwa atatumia fedha ili tu awafunge Township Rollers katika mechi ya marudiano kati yao kwa kutumia kuwapa timu mbili ambazo watacheza nazo mechi za kirafiki za kuwaongezea ujuzi zaidi mastaa wake kabla ya mechi ya marudiano.

 

Yanga, juzi Jumamosi ilijikuta ikibanwa na Rollers katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Yanga kwa sasa itacheza mechi ya marudiano itakayopigwa nchini Botswana.

 

Zahera ameliambia Championi Jumatatu, kabla ya mechi yao ya marudiano ya kombe hilo watacheza mechi mbili za kirafiki ambapo watazipa fedha timu hizo na kuzielekeza namna ya kucheza ili kuwaongezea ujuzi wachezaji wake kabla ya kwenda Botswana.

 

“Tutacheza mechi mbili za kirafiki kabla ya kwenda Botswana kwenye mechi ya marudiano. Katika mechi hizo tutazilipa fedha timu hizo na kuzielekeza jinsi ya kucheza kwa namna ya kutujenga ili tukienda kwenye mechi hiyo basi tuwe vizuri zaidi.

 

“Lengo la kutumia mechi hizo mbili ni kujinoa na kuongeza ujuzi zaidi baada ya kuona kuna shida kidogo katika mechi yetu ya hapa nyumbani. Naamini kwamba baada ya hapo tutakuwa vizuri na tutakuwa na nafasi ya kufanya vizuri.

 

“Tulijitahidi kucheza vizuri kwa kutengeneza nafasi ambazo tulishindwa kuzitumia sawasawa kwa sababu katika mashindano haya ushindi unaanzia nyumba, wao wameweza kupata bao kwetu na sisi tunaweza kwenda kufanya hivyo kwao ili tusonge mbele.

 

“Lakini kabla ya mchezo wa marudiano Botswana nimepanga kucheza mechi mbili za kirafiki ili kufanyia kazi makosa yetu kabla ya mchezo wa marudiano kwa sababu tunahitaji kufika mbali jambo ambalo linawezekana,” alisema Zahera.

SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam

Comments are closed.