The House of Favourite Newspapers

Zahera Wachimba Mkwara Stand United

Kikosi cha timu ya Yanga.

KOCHA Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera ametamba kuwa amekipeleka kikosi chake Shinyanga kwenda kuchukua pointi tatu tu na si vinginevyo.

 

Yanga, leo itakuwa mgeni wa Stand United katika mchezo wa ligi kuu uliopangwa kupigwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga saa 10 jioni.

 

Katika mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi, Yanga ilifanikiwa kuwafunga Stand mabao 3-2 mchezo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Zahera alisema katika kuelekea mchezo huo kikosi chake hakitakuwa na mabadiliko na kile kilichowafunga Mwadui FC mabao 3-1 kutokana na matokeo mazuri waliyoyapata.

 

Zahera alisema, katika mchezo huo mchezaji atakayeingia ni Heritier Makambo pekee aliyerejea nchini juzi Jumatano alfajiri akitokea DR Congo alipokwenda kuweka sawa ishu za kifamilia.

Aliongeza kuwa, Makambo ataingia katika kikosi chakecha kwanza baada ya kumuona kwenye mazoezi yake ya siku mbili aliyoyafanya pamoja na timu tangu aliporejea kujiunga na kikosi hicho.

 

“Binafsi kwa upande wangu maandalizi niliyoyafanya yanatosha kabisa kupata ushindi katika mchezo huu ambao ni mgumu kwetu tukiwa ugenini huku tukihitaji pointi tatu.

 

“Kikubwa ninataka kuona tunaendeleza rekodi yetu ya kuendelea kucheza mechi za ligi bila ya kupoteza, hayo ndiyo malengo yangu ambayo ninaamini yatatimia kutokana na kikosi changu kuimarika kila siku.

 

“Ninaamini Stand wana timu nzuri na wamejiandaa kama sisi tulivyojiandaa, lakini sisi pia tumejiandaa kwa ajili ya mchezo huo na kikubwa tunahitaji ushindi pekee, hivyo tutashambulia na kulinda goli ndani ya wakati mmmoja,” alisema Zahera.

STORI NA WILBERT MOLANDI

Comments are closed.