Zahera: Yanga Nipeni Pesa Niwaletee Makambo

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amewaambia mabosi wa timu hiyo kuwa kama wana fedha mkononi, fasta anakamilisha dili la usajili la mshambuliaji wa Horoya AC ya nchini Guinea.

 

Hiyo ikiwa siku chache tangu uongozi wa Horoya ukubali kumuachia mshambuliaji huyo kwa dau la Sh 100Mil ili wavunje naye mkataba wa mwaka mmoja alioubakisha.Makambo ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Yanga, ni kati ya washambuliaji wanaotajwa kutua kujiunga na timu hiyo katika msimu ujao.

 

Kwa mujibu wa Zahera, yupo tayari kuwapambania Yanga ili wafanikishe usajili wa Makambo kama watakuwa na fedha mkononi za kusitisha mkataba wake wa mwaka mmoja ambao ameubakisha.

 

Zahera alisema kikubwa wanachotakiwa kukifanya Yanga ni kuhakikisha wanauvunja mkataba wa mshambuliaji huyo kwa dau ambalo wametajiwa kabla ya klabu nyingine kuingilia kati usajili huo.

Aliongeza kuwa hakuna asiyefahamu uwezo wa Makambo katika kufunga mabao, hivyo Yanga ni lazima waingie gharama katika kutoa fedha ili wauvunje mkataba wake.

 

“Kama nilivyomtoa kumuuza Horoya ndiyo nitakavyofanikisha kumrejesha Yanga, hivyo ni lazima waingie gharama za kununua mkataba wake wa mwaka mmoja.

 

Kikubwa Yanga waache ubahili wa kusubiria mchezaji hadi mkataba wake utakapomalizika, uzuri mchezaji mwenyewe ameonyesha nia kubwa ya kutaka kurejea kuichezea Yanga.

 

“Wao wanachotakiwa wawe na pesa mkononi, baada ya hapo waniachie mimi kila kitu nisimamie usajili wake na nakuhakikishia ninamleta Makambo,” alisema Zahera.

STORI: WILBERT MOLANDI,Dar es SalaamTecno


Toa comment