ZAIDI YA WAKULIMA 250 WA KIWANGWA WAPATIWA SEMINA YA KILIMO

Baadhi ya wakulima  wa kilimo cha Nanasi  katika  kata  ya Kiwangwa, Wilaya ya   Bagamoyo mkoa wa Pwani  wakimsikiliza Kaimu Afisa kilimo  wa kata hiyo, Minihaji Msangi (kulia) akitoa elimu kuhusiana na matumizi ya mbolea mbalimbali zinazozalishwa na GSM Tanzania.

Mtaalamu wa masuala ya kilimo wa”Kilimo Joint”,  Linda Byaba akitoa elimu  ya matumizi ya mbolea mbalimbali zinazozalishwa na GSM Tanzania kwa  wakulima  wa kilimo cha Nanasi, Wakati wa Uzinduzi wa semina ya”Kilimo Darasa”.

Linda Byaba akitoa elimu  ya matumizi ya mbolea mbalimbali zinazozalishwa na GSM Tanzania kwa  wakulima  wa kilimo cha Nanasi, Wakati wa Uzinduzi wa semina ya”Kilimo Darasa”.

Wakulima wakimsikiliza  kwa makini  mtaalamu wa masuala ya kilimo wa”Kilimo Joint” Linda Byaba  wakati akitoa elimu  juu ya  matumizi ya mbolea. 

Diwani wa kata ya Kiwangwa, Wilaya ya   Bagamoyo mkoa wa Pwani, Malota Kwaga, (wapili kulia) akiwaonyesha wakulima  wa kilimo cha Nanasi  wa  kata hiyo  jinsi ya kuweka mbolea zinazotengenezwa na GSM Tanzania kwenye miche ya nanasi. 

 

WAKULIMA  wa zao la mananasi wa kijiji cha  Kiwangwa, wilayani Bagamoyo  wamepatiwa elimu ya kulimo darasa ikiwa ni sambamba na matumizi bora ya mbolea ili waweze kulima kulimo chenye tija na kuinuka kiuchumi.

Elimu hiyo itakayofanyika nchi nzima imetolewa  na kampuni inayojishughulisha na masuala ya kilimo ya Kilimo Joint kwa kushirikiana na  GSM Tanzania  kupitia kampuni yake tanzu ya GS Agro ambayo  imejikita kuhakikisha inabadilisha kilimo nchini Tanzania kwa kuleta bidhaa za kisasa za kilimo  ili kuongeza tija kwa wakulima nchini.

 

Akiongea wakati wa mafunzo hayo Afisa biashara mkuu wa GSM Tanzania, Remmy Nindi alisema shirika hilo linalosambaza madawa ya kilimo , mbolea na mbegu kwa bei nafuu, lina lengo la  kubadilisha  kilimo nchini  Tanzania kwa kutoa mafunzo ya matumizi bora ya mbolea  kwa wakulima ili waweze kulima kilimo chenye tija na cha kisasa na kupata faida.

 

 

“Lengo lililotuleta hapa leo ni kukaa na wakulima kutoa elimu ya shamba darasa jinsi ya matumizi halisi  ya mbolea inatumikaje ikiwemo kiwango gani cha mbolea kwa shamba heka ngapi, ili  wakulima waepuke kulima kwa mazoea ili mwisho wa siku  waweze kupata mavuno Bora na yenye viwango vinavyotakiwa kwa soko la ndani na nje ya nchi,” alisemA Nindi.

 

Afisa biashara huyo alisema awali walifanya utafiti na kubaini kuwa baadhi ya wakulima wamekuwa wakilima kwa mazoea  wakiamini kuwa ardhi ina rutuba bila kujua kama ardhi nayo huchoka, ndipo wakaamua kutoa  mafunzo ili waweze kuwatoa  katika mfumo wa zamani wakulima kwa mazoea na kuwapeleka kwenye ukulima wa kisasa na kunufaika na kilimo .

 

Alisema programu hiyo ya  kutoa mafunzo kwa wakulima imeanza kwa mkoa wa Pwani na baadae wataendelea mikoa mingine hapa nchini ikiwa ni pamoja mkoa wa Singida, Arusha  na  mbeya kwa ajili ya kwenda kutoa mifuko ya mbolea sambamba na kutoa elimu ya matumizi bora ya mbolea  hadi wakulima wote wafikiwe na kuleta mabadiliko kilimo.

 

“GSM kupitia kampuni yake tanzu ya GS Agro ina mpango wa kuleta mabaliko katika kilimo, tunatarajia kuwafikia wakulima wote bila kujali aina ya mazao wanayolima, ili waweze kulima kwa kufuata taratibu za matumizi ya mbolea ili hata viwanda vya chakula na anafaka vinavyoendelea kuanzishwa hapa nchini viweze kutegemea mazao bora  kutoka kwa wakulina wetu, lakini pia wakulima nao wafurahie kilimo chenye faida,”Alisema Nindi.

 

Akizungumzia suala la kuwawezesha wakulima kupata mikopo , alisema wanatarajia kufanya hivyo kwa kushirikiana na benki ya Kilimo na benki ya NMB ili wakulima waweze kupata mikopo ya mbolea na kuwa kwa sasa wako katika mazungumzo na benki hizo.

 

Baadhi ya wakulima waliopata mafunzo hayo  ya matumizi bora ya mbolea na shamba darasa walishukuru kampuni hiyo na kusema wakitumia mbolea kwa usahihi  itawasaidia kupata mavuno  yanayokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi na kuinuka kiuchumi.

 

“Mwanzo tulikuwa tunalima mananasi yasiyo na ubora  hata ukiyapeleka kwenye kiwanda hayakubaliki , hayana sukari na hata uzito wake nao unakuwa mdogo , lakini baada ya elimu hii ya matumizi bora ya mbolea za aina mbalimbali kutoka kampuni hii ya GSM tunaamini sasa mazao yetu yatakuwa bora, “alisema Salumu Mfikirwa mkulima wa mananasi Kijiji cha Kiwangwa.

Toa comment