DAR ES SALAAM: Tufani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwazoa wapinzani bado inapiga. Duru za kisiasa zinaonesha kuwa sasa anayesubiriwa kwa hamu kurejea ndani ya chama hicho tawala ni waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Lowassa aliyekihama chama hicho mwaka 2015 na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na baadaye kuwania urais katika uchaguzi mkuu uliopita, amehusishwa mara kadhaa kurejea alikotoka. Chanzo cha kuaminika cha habari kutoka ndani ya CCM kililiambia Uwazi kwa sharti la kutokutajwa jina kuwa kazi ya kumrejesha waziri mkuu huyo wa zamani imefika pazuri na kwamba inachosubiriwa hivi sasa ni wakati timilifu.
Wakati kukiwa na taarifa hizo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally aliliambia Uwazi kwa njia ya simu juzi (Jumapili) kuwa hawezi kumsemea Lowassa kuhusu nia yake ya kurejea CCM.
“Kakuambia kuwa anarudi CCM? Mimi siwezi kumsemea, lakini nikuambie tu kwamba hayo unayoyaona yanatokea chama chetu kinatesti tu mitambo,” alisema Dk. Bashiru bila kufafanua kutesti huko kumelenga kufanya nini kikubwa.
UPINZANI KUZIDI KUBOMOKA
Achana na wanachama wadogowadogo wa vyama pinzani kutimkia CCM, siku za hivi karibuni miamba ya siasa za upinzani nchini kama Julius Mtatiro kutoka Chama cha Wananchi ‘Cuf’ alikiacha chama chake na kujiunga na chama tawala jambo lililowaacha wapinzani midomo wazi huku wakijiuliza “Hata Mtatiro?”
Wengine walioibua mshtuko katika siku za hivi karibuni ni pamoja na Mbunge wa Ukonga Mwita Waitara, Mbunge wa Monduli nyumbani kwa Lowassa, Julius Kalanga na Diwani wa kata hiyo nao walimuasi waziri mkuu huyo mstaafu na kujiunga na CCM.
Kubomoka huko kwa ngome ya Lowassa iliyokuwa ngumu kuvunjika enzi za uimara wake kisiasa kumetajwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni ishara ya moto wa upinzani uliowashwa na waziri mkuu huyo mwaka 2015 kuanza kuzimika.
“Monduli inafahamika miaka nenda rudi, halikuwa jambo la rahisi kwa mtu kwenda kinyume na kiongozi huyo, Lowassa anaheshimika, anaaminika lakini leo ukiona kuna watu wanakwenda kinyume naye basi yako mambo mawili, moja ni kwamba nguvu zake zimepungua au naye anakubaliana na hali hiyo itokee,” alisema Hussein Said mchambuzi wa masuala ya siasa aliyeko Magomeni jijini Dar es Salaam.
Tangu uvume upepo wa CCM kuubomoa upinzania alioujenga Lowassa Monduli kumekuwa na taarifa nyingi, moja ikiwa ni kuwepo kwa kundi la wanachama wa chama tawala kumuomba arudi CCM ili alinde heshima yake kutokana na madai kwamba siasa za upinzani zimepoteza dira.
Hata hivyo waziri mkuu huyo mstaafu amekaa kimya mara zote, akiacha uvumi wa kurejea katika chama chake cha zamani uendelee bila kupatiwa majibu sahihi.
LOWASSA ASUBIRIWA KWA HAMU
Uchunguzi uliofanywa na Uwazi umebaini kuwa pamoja na baadhi ya wabunge na wanachama kutoka vyama vya upinzani kuhamia CCM kwa wingi wao katika siku za hivi karibuni, anayesubiriwa kwa hamu kuchukua uamuzi huo ni waziri mkuu mstaafu Lowassa.
“Wapinzani wameshapoteza mwelekeo, mimi nakuambia siku ambayo Lowassa atarejea CCM nitachinja mbuzi, nakuapia kwa Mungu kuwa hili litakuwa pigo la mwaka kwa wapinzani wetu,” alisema Mohamed Omary mwanachama wa CCM Temeke Kata ya 14, jijini Dar.
Mbali na wanachama wengi wa CCM kutamani Lowassa arejee kwenye chama chake cha zamani upande wa upinzani nako hofu kwa baadhi ya wanachama wanaoamini nguvu zake kisiasa inazidi kutanda hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
“Kila mtu anajua, wingi wa kura tuliopata wapinzani ulipatikana kutokana na nguvu za Lowassa, hata kuna baadhi ya wabunge wetu walishinda siyo kwa sababu walikuwa wanakubalika kwenye majimbo yao bali walisaidiwa na nguvu za Lowassa.
“Kama Lowassa atarudi CCM mimi nakuambia uchaguzi ujao mimi hata kupiga kura sitakwenda kwa sababu ushindi wa CCM utakuwa wazi kabisa,” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Jabir, mkazi wa Ubungo ambaye pia ni mfuasi wa Chadema.
LOWASSA NA MAGUFULI WANAELEWANA?
Miaka mitatu tangu ufanyike uchaguzi mkuu uliowakutanisha Lowassa aliyekuwa anagombea kupitia muungano wa vyama vya upinzani maarufu kwa jina la Ukawa na Rais aliyeko madarakani Dk. John Pombe Magufuli kutoka CCM, inaelezwa kwamba harakati za kuwania kiti cha urais hazikuwaachia kovu wanasiasa hao na kwamba wanaelewana na kuheshimiana.
Mara kadhaa Rais Magufuli amemsifu Lowassa hadharani na kumtaja kuwa ni mwanasiasa mkomavu aliyeleta mchango mkubwa wa kimaendeleo katika taifa. Lowassa na Rais Magufuli walipokutana Ikulu Januari, mwaka huu, katika kikao chao cha siri rais alisema:
““Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane nae, na leo nimekutana nae, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu, kwa ujumla Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.”
Naye Lowassa alitoa yake ya moyo kwa kusema: “Na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira, Stiegler’s Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru Mhe. Rais, you made my day.”
Ukaribu huu wa viongozi hawa, umekuwa ukitazamwa na wengi kuwa ni kichocheo cha Lowassa kuweza kuamua kurejea katika chama alichotoka ambacho kinatajwa kuwa kimejaa marafiki zake wengi kuliko upinzani ambao anafanya nao kazi hivi sasa.
CCM INATOA RUSHWA KUNUNUA WAPINZANI?
Baada ya kuwepo kwa wimbi kubwa la wapinzani kujiunga na CCM, baadhi ya viongozi wa upinzani wamekuwa wakilalamika kwamba chama tawala kinacheza mchezo mchafu wa kuwanunua wapinzani ili kuwadhoofisha nguvu. Akijibu tuhuma hizo mara baada ya kuulizwa na Uwazi juu ya uwepo wa madai hayo, Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru alisema:
“Naomba nikuambie kuwa chama chetu hakina hela za kununua wapinzani na mimi ndiye mtendaji wa chama, sijawahi kuona fungu la hela linatengwa kwa ajili ya kuhonga wapinzani. “Kinachotokea ni kwamba, chama chetu kimefanya mageuzi makubwa, sasa kinaaminika, kinawavutia watu.
“Sisi tunapoona watu wanavutika na chama chetu ndiyo tunazidi kupata nguvu ya kuendelea kufanya kazi zaidi zenye lengo la kuwaletea wananchi maendeleo. “Tunaendelea kuwakaribisha wote wanaovutiwa nasi, na kama Lowassa anavutiwa na utendaji wetu tunamkaribisha na wenzake wote.”
WIMBI KUBWA LA WAPINZANI KUHAMIA CCM
Uchunguzi uliofanywa na Uwazi umebaini kuwa kasi ya wafuasi na viongozi wa upinzani kuhamia CCM itazidi kuongezeka kuelekea uchaguzi mkuu na kwamba hiyo ndiyo mikakati ya chama tawala kujihakikishia ushindi usiokuwa na jasho katika uchaguzi mkuu ujao. “Kama chama hatutaki kufanya makosa, kilichotokea mwaka 2015 kimetupa funzo, kazi tuliyonayo hivi sasa ni kuimarisha safu yetu ya ushindi na kusema kweli adui yako muombee njaa.
“Sisi tunapoona upinzani unabomoka tena kwa sababu ya chama chetu na Serikali yake kufanya vizuri kiutendaji hili ni jambo zuri sana, kwa sababu litaleta utulivu na maendeleo kwa ujumla,” kilisema chanzo chetu kutoka safu ya juu ya uongozi wa CCM kulichoomba kisitajwe jina.
Hata hivyo, wapinzani nao mara kadhaa wamekuwa wakilalamika kwamba mbali na kufanyiwa rafu za kisiasa watahakikisha kuwa wanajiimarisha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa lengo la kushika dola.
KUBENEA ATOA YA MOYONI
Kufuatia kuwepo kwa madai kwamba kuna baadhi ya wabunge kutoka Chadema ambao wako mguu sawa kukihama chama chao na kujiunga na CCM akiwepo Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, mbunge huyo ametoa ya moyoni kwa kusema hivi:
“Kwanza wanaosema narudi CCM wananikosea sana, mimi katika maisha sijawahi kuwa CCM, sifanani na watu wa CCM, sasa narudije huko. “Mimi nakuambia kamwe sitajiunga na CCM, nitabaki kwenye siasa za upinzani na kama kuna changamoto za ndani nitakabiliana nazo nikiwa humuhumu.”
Baadhi ya viongozi waliotoka upinzani na kujiunga na CCM ni pamoja na Anna Mgwira, Kitila Mkumbo, Juliana Shonza, Moses Mashali, David Kafulila, Maulid Mtulya, Mwita Waitara na Patrobas Katambi.
Comments are closed.