The House of Favourite Newspapers

Zamu yao

0

ZAMU Yao! Leo Jumamosi Simba na Yanga zinapambana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya Ligi Kuu Bara, makocha wa timu hizo wana sababu tofauti za kutaka ushindi.

Hii ni mechi ya 11 kuzikutanisha timu hizi tangu Oktoba 2011 na katika hizo, Yanga imeshinda mara mbili tu, Oktoba 29, 2011 ilipoifunga Simba bao 1-0 na Mei 18, 2013 iliposhinda mabao 2-0.

Ukitoa mechi hizo, Simba imeshinda mechi nne na nyingine nne timu hizo zimetoka sare. Rekodi hiyo imemfanya Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, kukuna kichwa na kutengeneza mbinu nyingi za kuhakikisha leo timu yake inashinda.

Pluijm ameliambia Championi Jumamosi kuwa, licha ya kutaka kuendeleza rekodi yao ya ushindi katika ligi kuu, jambo la msingi ni kuifunga Simba ili kuwapa faraja mashabiki wa Yanga.

“Ukitazama rekodi ni tatizo kidogo, sitaki kutumia matokeo yaliyopita baina ya timu hizi lakini nimejipanga kuhakikisha vijana wangu wanashinda ili faraja irejee Yanga,” alisema kwa msisitizo Pluijm.

Yanga kabla ya mchezo huo imezifunga Coastal Union mabao 2-0, Prisons mabao 3-0 na JKT Ruvu mabao 4-1. “Hayo ni matokeo mazuri, sasa tunataka kuendelea kwa mechi zinazofuata,” alisema Pluijm akimaanisha mechi ya leo na Simba.

UJANJA KIDOGO

Siku mbili kabla ya kuondoka Pemba, Pluijm alionekana akiwapiga mkwara wachezaji wake kuzungumzia mchezo huu wa leo kwa kile kilichoelezwa wauone ni mchezo wa kawaida tu.

“Mara zote Yanga inapokuwa katika nafasi ya kuifunga Simba, wachezaji huwa wana hamu ya kuingia uwanjani na kupata ushindi na matokeo yake hali hubadilika, hivyo sasa hivi Yanga wana tahadhari kubwa,” alisema mmoja wa viongozi wa Yanga aliyekuwa kambini Pemba.

Pluijm alionekana akiwasisitizia zaidi wachezaji wake kuwa makini katika kukaba kuanzia washambuliaji hadi mabeki huku akiwataka kucheza pasi za chinichini kuanzia katikati ya uwanja kila wanaposhambulia.

SIMBA USHINDI TU

Kocha wa Simba, Dylan Kerr yeye anataka kuendeleza rekodi ya ushindi inayoupata timu yake katika mechi za ligi kuu. Simba ilianza kwa kuifunga African Sports bao 1-0, ikaifunga Mgambo JKT mabao 2-0, halafu ikaifunga Kagera Sugar mabao 3-0.

Kerr alisema: “Najua mashabiki wanataka ushindi katika mechi hii, mimi na wachezaji wangu tunataka kuendeleza rekodi ya ushindi na hii ni zamu ya timu nyingine kufungwa.”

Kocha huyo raia wa Uingereza, alisema anataka kuthibitisha Simba ipo vizuri na haikubahatisha katika mechi zake tatu za kwanza ilizoshinda.

VITA YA KIIZA, TAMBWE, NGOMA

Katika ufungaji wa ligi kuu, Hamisi Kiiza wa Simba anaongoza kwa ufungaji akiwa amefunga mabao matano katika mechi tatu huku Amissi Tambwe na Donald Ngoma wa Yanga wakiwa wamefunga mabao matatu kila mmoja.

“Kama nimefunga katika mechi ngumu kama za Tanga, nadhani nitafunga pia dhidi ya Yanga kwenye uwanja mzuri (Taifa) lakini kazi itakuwa ngumu,” alisema Kiiza.

Nguvu ya Yanga katika ufungaji itawategemea zaidi Ngoma, raia wa Zimbabwe na Tambwe wa Burundi. Yanga ina pointi tisa katika nafasi ya kwanza, sawa na Simba iliyo katika nafasi ya pili.

Tofauti pekee kati ya timu hizo ni mabao ya kufunga ambapo Yanga inayo tisa na Simba ina sita, zote zimefungwa bao mojamoja. Hii inaonyesha safu zao za ushambuliaji zipo vizuri hata beki zao.

USIFANYE FUJO TAIFA

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, aliliambia Championi Jumamosi kuwa, ulinzi umepangwa kuwa mkali na wa uhakika, hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi.

“Huu ni mchezo maalum na mgumu sana, kwenye ulinzi tumejiandaa vizuri kuhakikisha amani inakuwepo,” alisema Kizuguto.

Katika mchezo huo, mwamuzi atakuwa Israel Nkongo akisaidiwa na Josephat Bilali (Tanga), Ferdinand Chacha (Mwanza) na Soud Lila (Dar), wakati kamisaa wa mechi atakuwa ni Charles Mchau (Kilimanjaro).

 

Mechi  tatu za mwisho za Simba na Yanga

  1. Desemba 13, 2014

Yanga       0-2   Simba (Mtani Jembe)

  1. Oktoba 18, 2014

Yanga       0-0   Simba

  1. Machi 8, 2015

Simba       1-0   Yanga

Leave A Reply