Zanzibar: Uchaguzi Urais, Wawakilishi Kufanyika Siku 2

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imetangaza Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa urais na uwakilishi utafanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.

 

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Mkuu Mstaafu, Hamid Mahmoud, wakati akizungumza na waandishi wa habari  Alhamisi tarehe 30 Julai 2020 visiwani humo.

 

Amesema, kura ya mapema kwa watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi huo, itafanyika siku moja kabla yaani Jumanne tarehe 27 Oktoba 2020.

 

“Natangaza rasmi tarehe ya uchaguzi itakuwa Jumatano tarehe 28 Oktoba mwaka huu, ndugu wananchi, sheria ya uchaguzi imetoa nafasi kufanyika kura ya mapema, napenda kuwajulisha, upigaji kura ya mapema itafanyika tarehe 27 oktoba 2020 siku moja kabla ya upigaji kura pamoja,” amesema Jaji Mahmoud.

 

“Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, upigaji kura mapema utahusisha watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi siku ya uchaguzi, watendaji hao ni wasimamizi wa uchaguzi, wasaidizi wasimamizi uchaguzi, wasimamizi wa vituo, askari polisi watakaokuwa kazini siku ya uchaguzi ,” amesema Jaji Mahmoud.

 

Siku hiyo ya uchaguzi mkuu, inafanana na ile iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania kuwa, uchaguzi mkuu utafanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.

 

NEC ilisema shughuli ya uchukuaji fomu kwa wagombea ambapo wagombea wa ubunge na udiwani watachukua fomu tarehe 12 hadi 25 Agosti 2020, katika ofisi za NEC za halmashauri na kata nchi nzima.

 

Uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 25 Agosti 2020, huku kampeni zitaanza tarehe 26 Agosti hadi 27 Oktoba 2020.

 

Kazi ya kuhesabu kura na kutangaza matokeo itakuwa Oktoba 28 -31 mwaka huu. Tume imetangaza tarehe hiyo kutokana na kutamkwa kwa tarehe rasmi ya kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambayo ni Agosti 20.

Toa comment