The House of Favourite Newspapers

ZARI AIBLOKI FAMILIA YA DIAMOND

DAR ES SALAAM: “Nikanyage bahati mbaya, nikulipue makusudi!” Mstari huo wa Wimbo wa Ni Hayo wa Rapa Fareed Kubanda ‘Fid Q’ unaakisi kitendo anachodaiwa kukifanya mwanamama wa Kiganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kwa kuwakatia mawasiliano (kuwa-block) familia nzima ya mzazi mwenzake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Gazeti la Ijumaa lina mchapo kamili.

 

Mrembo huyo aliyemzalia Diamond au Mondi watoto wawili, Tiffah na Nillan kabla ya kumwagana mapema mwaka jana, anadaiwa ‘kuwabloki’ familia nzima ya Mondi kwenye Mtandao wa Instagram mara baada ya kuona familia hiyo inamletea ‘mapichapicha’ kwa kujinasibu na wanawake tofautitofauti wa Mondi.

 

VYANZO MBALIMBALI

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vilivyovujisha ubuyu kwa Gazeti la Ijumaa, Zari alianza kukata mawasiliano na Diamond, lakini alikuwa akiendelea kuwasiliana na ‘mkwewe’, Sanura Kassim ‘Bi Sandra’ na wifi yake, Esma Khan kabla ya kuwa-block wote.

 

“Unajua Zari ni mtu mwenye misimamo sana. Baada tu ya kutangaza kummwaga Mondi Februari 14, mwaka jana, alisema penzi lake na Mondi limekufa, lakini hawezi kukata mawasiliano na familia yake maana wao hawana makosa yoyote.

“Ndiyo maana ulikuwa unaona akaunti ya mama Diamond anayotumia jina la mama Dangote kwenye Insta ilikuwa inaendelea kupendeza na picha za wajukuu zake, Tiffah na Nillan kwa sababu Zari alikuwa vizuri na mama Dangote (mama Diamond), lakini baadaye walivyoanza kumletea mapichapicha ya wanawake wengine, Zari akaona isiwe shida, acha awafyekelee mbali,” kilieleza chanzo kimoja.

 

CHANZO KINGINE

Chanzo kingine kilicho karibu na familia ya Mondi kilieleza kuwa, Zari aliamua kuwa-block wote baada ya kuona mama Diamond na Esma wako bize kutupia mitandaoni picha za mrembo mwingine aliyedaiwa kutoka na Mondi, Lilian Kessy ‘Kim Nana’ na kabla hajakaa sawa akaona wako bize na mrembo wa sasa wa Mondi, Tanasha Donna ‘Zahara Zaire’.

 

“Unajua Zari ana roho ya kizungu, hakutaka kuwakatia mawasiliano, lakini amejikuta akifanya hivyo baada ya kuona matendo ya kina mama Diamond na Esma yanaweza kumtukanisha hususan pale mashabiki watakapoona vitendo vyao vya kuwaunga mkono wanawake wengine wa Mondi.

 

“Sasa ili asione mambo wanayoyaweka na namna mashabiki wanavyowashadadia katika mitandao ya kijamii, Zari akaona dawa yao ni kuwa-block ili asiwe na uwezo wa kuona yanayoendelea katika akaunti zao za Instagram,” kilisema chanzo hicho.

Kama hiyo haitoshi, vyanzo hivyo vilidai kuwa kutokana na kutofurahishwa na mambo hayo yanayofanywa na familia ya Mondi, ameamua kumkatia mawasiliano mazima Mondi hata katika suala zima la kwenda kuwaona wanaye Sauz (Afrika Kusini) anakoishi.

IJUMAA LAJIRIDHISHA

Baada ya kupewa ubuyu huo, kabla ya kuwatafuta wahusika, Gazeti la Ijumaa lilijaribu kujiridhisha kwa kuperuzi kwenye akaunti za familia ya Diamond na kubaini kuwa ni mama Diamond pekee ndiye aliyekuwa akionekana kuwa karibu na Zari kwa kuendelea kuposti picha mpya kabla ya kukata mawasiliano mwishoni mwa mwaka jana.

 

Hiyo ilionesha ni dhahiri kuwa, kama ilivyoelezwa na vyanzo kuwa Zari aliendelea kuwasiliana na mama Mondi, lakini aliacha pale tu alipoanza kuona ‘wakwe wapya’ wanakaribishwa katika familia ya mzazi mwenzake huyo.

ESMA AFUNGUKA

Juzi, Gazeti la Ijumaa lilijaribu kumtafuta Diamond ili kumsikia anazungumziaje ishu hiyo ya kupigwa block na mzazi mwenzake, lakini simu yake iliita bila kupokelewa kama ilivyokuwa kwa mama Mondi.

 

Hata hivyo, gazeti hili lilimvutia waya dada yake Mondi, Esma ambapo alipopatikana alikiri kupigwa block muda mrefu, lakini akasema haoni tatizo kwani hayo ni mambo yao binafsi, lakini zaidi ni kwamba wao wanamuunga mkono ndugu yao pale anapokuwa kwenye uhusiano wake.

“Sisi hatuwezi kuingia sana kwenye uhusiano wa Nasibu (Mondi), lakini huwa tunamsapoti pale anapokuwa. Kwa sasa yupo na Tanasha, basi tunamuunga mkono,” alisema Esma.

ROMMY KAMA ESMA

Alipotafutwa binamu yake Diamond, Rommy Jones ambaye ni official DJ wa mwanamuziki huyo na kuulizwa kuhusu ishu hiyo alikiri na yeye kulishwa block na Zari, lakini akasema kitu kikubwa wanachoangalia wao kama familia ni ndugu yao kuwa na amani katika uhusiano wake.

“Sioni tatizo kublokiwa, lakini sisi tunachoangalia ni furaha ya Diamond inakuwepo basi, hayo mambo mengine si muhimu sana,” alisema DJ Rommy.

 

KUHUSU MONDI KUZUIWA SAUZ…

Alipoulizwa kuhusu suala la Mondi kupigwa ‘stop’ Sauz kwenda kuwaona wanaye, Rommy alisema hilo ni jambo lisilowezekana maana nyumba anayoishi Zari kule Sauz ni ya Mondi hivyo hawezi kumzuia asiende.

 

IJUMAA LINAFAHAMU

Hata hivyo, Gazeti la Ijumaa linafahamu ni muda mrefu umepita Mondi hajaonekana Sauz kama ilivyokuwa zamani ambapo alikuwa hakai zaidi ya mwezi au miezi mitatu hajaenda kuwaona wanaye.

Stori: IMELDA MTEMA, IJUMAA

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.