ZARI AMTIA MATATANI MONDI

KILICHOMPONZA Nasib Abdul ‘Diamond Platnumz’ ni kauli yake kuwa mjengo anaoishi mzazi mwenzake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kule Sauz (Afrika Kusini) ni wake. 

 

Diamond au mwite Mondi kwa kifupi alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akifanya mahojiano maalum na kituo kimoja cha redio hapa nchini. “Ile nyumba ni yangu na document (nyaraka) zote ninazo, nikitaka kuiuza naweza kuiuza wakati wowote, lakini kwa kuwa wanaishi wanangu…” alisema Mondi.

 

AINGIA MATATANI

Kwa juujuu, kauli hiyo ya staa wa muziki wa Bongo Fleva aliyepata kuwa mpenzi wa Zari kabla ya kuachana mapema mwaka jana (Februari 14) ilionekana kuwa haina kwaro, lakini wenye chekeche la maneno waliyachukuliwa kama ni ya udhalilishaji na kuanza harakati za kupambana naye.

 

Kundi la watu wanaojiita Team Zari walianzisha mashambulizi dhidi ya Mondi kwa kuposti mambo ya ovyo kwenye mitandao ya kijamii na maneno ya kuumuudhi msanii huyo huku wakimkumbusha kuwa nyumba anayosema ni yake alishampa Zari kama zawadi.

“Kwenye birthday ya Zari iliyofanyika Sauz Diamond alisema nyumba hiyo amempa Zari kama zawadi yake.  “Leo mtu yuleyule anakuja na kusema kwamba nyumba ni yake kwa hiyo alimpa kwa kumringishia au ndiyo ilikuwa kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa…” mchangiaji mmoja mtandaoni aliandika katika posti yake.

 

HARAKATI ZA KUMSHUSHA MONDI ZAFAYWA

Kutokana na kuwa mahojiano hayo maalum aliyafanya Mondi wiki ambayo alitoa wimbo wake na kuuweka kwenye Mtandao wa YouTube na kuonekana kufanya vizuri uchunguzi unaonesha kwamba Team Zari walihamasishana kutounga mkono sanaa yoyote ya mwanamuziki huyo.

 

Ingawa madhara ya moja kwa moja hayakuonekana kitalaam kwamba hamasa hiyo ilimuathiri chochote Mondi na wimbo wake wa The One uliokuwa unaongoza kwa kushika namba moja, lakini ulishuka ambapo baadhi ya mashabiki walionesha kufurahishwa na kuporomoka huko.

 

“Huu ndiyo ushindi wetu, arudi akaedelee kupiga domo,” mchangiaji mmoja aliandika mtandaoni. Wimbo wa The One ulitolewa kwenye nafasi ya kuwa namba moja na wimbo wa mwanamuziki Ali Kiba ‘King Kiba’ aliyeachia ngoma yake mpya iitwayo Mbio.

 

WATETEZI WA MONDI WAIBUKA

Kutokana na mashambulizi ya kumsakama Mondi kwa kauli yake hiyo, mashabiki wake nao hawakulaza damu walianzisha harakati za kutetea heshima ya mwanamuziki huyo kwa kuzima tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake na timu Zari.

 

Mondi ‘sapota’ kutoka ndani na nje ya nchi waliwashambulia waliokuwa akimponda huku nguvu kubwa ikielekezwa kumdhalilisha Zari kwa kuweka picha na video zake mbaya.

VITA YAZIDI

Kwenye mitandao ya kijamii zilipostiwa kila aina ya kejeli baina ya makundi hayo mawili hadi kufikia hatua ya kutukanana matusi mazito ambayo hayastahili kuandikwa gazetini. Hata hivyo, wakati Team Mondi ikijigamba kwa kuweka video zinazoonesha makaratasi yanayodaiwa kuwa ni nyaraka halisi za nyumba ya Mondi Sauz, Zari yeye alikuwa akijitetea kwa kusema hatishwi kwa chochote kwa sababu anazo nyumba za thamani zipatazo nne.

 

Aidha, alikoleza hali ya kutokujali kwake sakata la kuhamishwa kwenye nyumba ya Mondi kama Team Mondi walivyotaka, aliandika hivi kwenye ukurasa wake wa Instagram; “Simuoni mtu wa kuja kunitoa hapa na kwa taarifa yenu sihami hapa.”

 

MSANII AFUNGUKA

Mmoja kati ya wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya nchini ambaye hakupenda kuandikwa gazetini alisema katika sanaa, sarakasi kama hizi za Mondi wakati mwingine ni nzuri katika kukuza jina.

 

“Nenda Marekani na kwingineko mambo kama haya ya wasanii wenyewe au wapenzi wao kushambuliana yanatokea na mengine yanatengenezwa ili kuyaweka masikio ya jamii tayari kwa jambo fulani. “Nimefuatilia mjadala wa Diamond na Zari na masuala yao ya nyumba na mapenzi ni mzito, lakini sifikirii kama unaweza kumshusha Diamond kimuziki, sanasana unampaisha,” alisema msanii huyo.

 

USHAURI WATOLEWA

Hata hivyo, baadhi ya watu mitandaoni waliwashauri Zari na Mondi kuacha kuukuza majadala huo kwa sababu ya heshima yao na watoto wao. “Kumbukeni mmezaa watoto, haya mambo ya ovyo mkiedelea kuyapa nafasi yataharibu heshima yenu, potezeeni mambo yaishe,” aliandika mchangia mmoja aliyejitaja kwa jina la @ mdadampole.

Toa comment