Zari ‘Jogoo wa Shamba’ Aliyewika Mjini
ZARINA Hassan ‘Zari’ amezima nyota ya Wema Sepetu na amefubaza mno muonekano wa kisupastaa wa wasanii wengi wa kike Bongo; bisha watu wakushangae.
Zari alipokuja Bongo aligeuza msemo wa ‘mgeni njoo mwenyeji apone.’ Ukawa ‘mgeni njoo mwenyeji afe’ na kweli wenyeji wamekufa; anapokuwepo Zari, dada zetu wa Kibongo wote mikono juu, mwendo wa mateka.
JE, ZARI NI MZURI SANA?
Suala la uzuri ni falsafa ya mate; kila mtu ana yake. Ukikubali uzuri wake au ukiukataa yote ni sawa, lakini Zari anabaki kuwa ni mama wa watoto watano. Ukijazia kuwa jua la umri wake limeegama, hilo litakuwa lako.
Zingatio ni kwamba, maana zote mbili; yaani awe mzuri au la! Bado ukweli kuwa amewafunika akinadada wa Bongo unabaki palepale. Unapoona Zari ‘kamuua steringi’ wa mastaa, Wema Sepetu, ujue kafikia mwisho wa filamu, yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii ni maandishi tu.
AMEPATAJE KUWIKA UGENINI?
Hazina aliyonayo kichwani ni kubwa, anatambua kila thamani anayopewa na Mungu ni fedha na maisha bora. Zari hachezei fursa, haishi kwa kumfurahisha mtu bali nafsi yake.
Paap; alipotua Bongo alimkuta Wema na mastaa wenzake wanachezea fursa, akatambua mbinu ya kumuwezesha kuwika Bongo ambayo ni: “Ukitaka kuwatawanya kondoo, mpige mchungaji.”
Alipofanikiwa kumdhibiti Diamond kimapenzi kiasi cha kumwagana na Wema; watu wote wakashtuka; nani huyu tena? Wakaambiwa Zari the big boss kutoka Uganda kaingia Bongo.
Hapo ndipo kazi ya kutengeneza fursa ya kupiga fedha ilipofunguka; mikataba ya matangazo ya makampuni mbalimbali mfano Coca Cola, Vodacom, Red Gold na mingine akaiteka kirahisi, kwenye shoo za muziki ikiwemo pati gumzo ya Zari All White, nako alivuna mihela si ya kitoto.
WABONGO WAMEPOTEA JUMLA?
Wakiendelea kuzubaa ni kweli watapotea jumla maana hatajiriki mtu kwa kumchukia tajiri. Walikosea wakampa chati Zari na sasa wanaendelea kufanya makosa.
Wema alipokuwa na Diamond ukomo wa fikra zake ulikuwa ni kupata fedha na kuzimwaga kwenye majukwaa ya bendi za muziki, kulewa, kufanya anasa na vituko vya kila aina; kwa Zari kila fedha inayopatikana, hufanya kazi ya maendeleo.
Kinachowapoteza njia mastaa wengi wa kike Bongo si kutokutumia vipaji vyao bali ni kuvitumia na kubaki watumwa.
Kama atatafuta mpenzi basi huyo ampe fedha akalewe, ampagie nyumba nzuri kidogo na kigari cha kuzugia mitaani watu wamkome, basi inatosha!
Wanasahau kuwa njiwa wanajua mapenzi kuliko wao lakini maisha yao yako chini ya mwenye banda siku akiamua kuwachinja hakuna wa kumzuia.
Ndivyo walivyo mastaa wengi, wanahangaika weee na wanaume, wanatumika kweli lakini mwisho wa siku wanaishi chini ya watu, Zari hafanyi ujinga huo.
Leo kamtimua Diamond lakini maisha ya Zari yanaenda, hashuki thamani. Wajinga wanaishia kumshambulia kwenye mitandao ya kijamii wakidhani wanamshusha kumbe ndiyo kwanza wanamuo-ngezea umaarufu. Nimesema huwezi kutajirika kwa kumkasirikia tajiri. Kwa Bongo hii hakuna staa wa kike anayeweza kumfikia Zari!
MOJA LA MWISHO
Zari alikuwa mwanamuziki, alipowika kidogo tu akakamata fursa, hivi sasa ni mfanyabiashara mkubwa, anamiliki shule na maduka ya urembo, makazi yake ni Sauz. Nanyi Wabongo amkeni mkamate fursa mtusue kimaisha.
Mfano, wewe Wema, Uwoya, Wolper, Lulu, Aunt Ezekiel, Kajala, wote mmekuwa mastaa, mnajulikana. Mkiamua kufungua mgahawa halafu wote mkawa mnahudumia; ni wateja wangapi watakuja kula na kuwaona? Mtapiga fedha ninyi, hakuna mfano. Mkiambiwa fursa za kushika ndiyo hizo; ZIKAMATENI MJIKOMBOE
Comments are closed.