Zelensky: Sikufanya lolote baya kwa Trump
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekataa kuomba msamaha baada ya mabishano makali na majibizano ya maneno na mwenzake wa Marekani, Donald Trump katika Ikulu ya White House.
Mkutano wa viongozi hao wawili katika Ofisi ya Oval, ambao hapo awali ulipangwa kukamilisha makubaliano ya kuipatia Marekani haki ya madini adimu ya Ukraine, uligeuka na kuwa piga nikupige ya maneno baina ya marais wa Marekani na Ukraine.
Fukuto lilipozidi katika Ikulu ya White House, Volodymyr Zelensky alitoka kwa hasira bila kujibu maswali ya waandishi wa habari. Mkutano huo uliisha ghafla, huku Trump akifuta pia mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari uliokuwa umepangwa.
Akijibu swali la mtangazaji wa Fox News kuhusu iwapo anadhani kuwa ana deni la kuomba msamaha kwa Trump, Zelensky amesema: “Ninamheshimu Rais na watu wa Marekani. Nadhani tunahitaji kuwa wawazi na wakweli. Pamoja na hayo sina uhakika kwamba nimefanya jambo lolote baya.”
Zelensky aliondoka White House na msafara wake, na kuacha mpango wa madini bila kutatuliwa. Afisa wa Ikulu ya White House alithibitisha baadaye kuwa, hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa baina ya pande mbili hizo.