Zengwe Bata la Dimpoz Marekani
DAR ES SALAAM: Zengwe limeibuka! Wakati ikiwa hana muda mrefu sana tangu arejee kwenye gemu la muziki baada ya kuumwa kwa muda mrefu, bata la mkali wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’, limewashtua wengi na kuibua maswali kibao, Gazeti la Ijumaa limekukusanyia habari kamili.
TUJIUNGE MAREKANI
Mapema wiki hii, Dimpoz akiwa na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho walitupia picha tofautitofauti wakila raha katika mji maarufu kwa mastaa Beverly Hills, California nchini Marekani huku nyingine wakijiachia na staa mkubwa wa muziki wa Pop duniani, Paris Hilton.
AJIACHIA PIA HOLLYWOOD
Kama hiyo haitoshi, Dimpoz alitupia picha nyingine akiwa katika mji mwingine wa kishua wa Hollywood nchini humo ambao upo jirani na Beverly Hills ambako nako alionekana akijiachia kwenye milima maarufu ya Hollywood ambako mastaa wengi hutembelea.
FULU MANDINGA YA MAANA
Dimpoz alizidi kuwakata maini wasiopenda maendeleo ya watu mitandaoni kwa kutupia picha tofauti akiwa kwenye magari ya kifahari tofauti pande hizo za Marekani.
Kwenye vipande vya video ambavyo aliviachia, mkali huyo alionekana akitoka kwenye hoteli zenye hadhi ya kistaa, akiwasha moja ya magari hayo ya kifahari (yale ya milango ya kufunguka kwa juu) na kutokomea kusikojulikana.
AMFUNIKA BOSI WAKE
Tathimini ya wachangiaji mbalimbali mitandaoni walionesha kuwa bata analokula Dimpoz linamfunika bosi wake katika Lebo ya Rockstar 4000, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ ambaye mara nyingi si mtu wa kupenda makuu au mbwembwe za kifahari.
“Kiba si mtu wa haya mambo ndiyo maana unaona ni rahisi sana Dimpoz kumfunika maana yeye anapenda haya mambo,” aliandika shabiki mmoja wa msanii huyo kwenye Mtandao wa Instagram.
ZENGWE SASA…
Kufuatia bata hilo ambalo halihitaji elimu ya chuo kikuu kugundua kwamba msanii huyo anateketeteza mamilioni ya fedha, zengwe sasa likaibuka kwenye mitandao mbalimbali inayoandika habari za mastaa nchini Kenya pamoja na mitandao ya kijamii.
Mitandao hiyo ilijaribu kuhoji kuhusiana na bata hilo la Dimpoz hasa kwa kuzingatia hawakuona picha zozote za shoo zaidi ya kula bata katika maeneo ambayo ni ya gharama kubwa.
“Sasa inakuwaje kweli hata kama Joho ana pesa waende tu kuziteketeza bure Marekani kweli? Dimpoz ni mwanamuziki, Joho ni mwanasiasa, wapi na wapi? Tungeona picha za shoo labda tungesema amekwenda kikazi,” alichangia Okech kwenye moja ya mitandao hiyo ya nchini Kenya.
Kama hiyo haitoshi waliozidi kuamsha zengwe mitandaoni walishikilia pia hoja ya kuwa Dimpoz anafanya kufuru hiyo kwa pesa zake au ni za Joho na kama ni zake atakuwa amezipata wapi kwani hana muda mrefu kwenye gemu tangu atoke kuumwa.
WENGINE WAMSIFIA JOHO
Pamoja na watu wengi kuhoji kuhusu maana ya bata hilo, wapo wengine ambao walijaribu kufafanua kuwa inawezekana Joho akawa ameenda na Dimpoz kutumia tu kwani uwezo wa kufanya kufuru hizo upo chini ya uwezo wake kutokana na mkwanja mrefu alionao.
Wachangiaji hao walikwenda mbele zaidi kwa kusema si tu kwamba amekwenda na Dimpoz kula bata hilo bali amekuwa akifanya hivyo kwa wasanii mbalimbali wanapokwenda nchini Kenya na amekuwa hata akiwasaidia pindi wanapopata matatizo binafsi.
WAKUMBUSHIA LA DIMPOZ
Wachangiaji hao walibainisha kuwa hata kipindi kile Dimpoz alipokuwa anaumwa, alitumia gharama kubwa sana katika matibabu yake hivyo suala la kuponda raha katika miji ya Marekani kwa siku mbili-tatu haliwezi kumsumbua.
Gazeti la Ijumaa lilimvutia waya Dimpoz kwa njia ya mtandao wa WhatsApp ambapo simu yake iliita bila kupokelewa. Kuna wakati ilionekana anataka kupokea, lakini hadi tunakwenda mitamboni ilishindikana kumpata kufuatia kuonekana kuna shida ya mawasiliano.
MENEJA WAKE ANENA
Hata hivyo, Gazeti la Ijumaa lilimtafuta mmoja wa mameneja wa Dimpoz, Aidan Seif ambaye alijibu kwa kifupi kuwa msanii huyo yupo nchini Marekani kwa ziara ya kikazi.
“Yupo kikazi, kama unavyojua dili za kazi haziwezi kumzuia mtu kupiga picha katika maeneo mbalimbali wakati hayo maeneo ndipo kulipofanyika pia baadhi ya vikao hivyo vya kazi,” alisema Aidan.
SI MARA YA KWANZA
Kwa muda mrefu Dimpoz amekuwa ni mtu wa bata na kujiachia maeneo mbalimbali ya kifahari duniani ikiwemo mji wa ufukweni wa Ibiza nchini Hispania.
Stori: ERICK EVARIST, IJUMAA
Comments are closed.