The House of Favourite Newspapers

Zijue Aina za Ugumba kwa Wanawake / Wanaume

UGUMBA ni hali inayotokea iwapo watu wawili, mwanaume na mwanamke wanakutana kimwili bila kutumia njia yoyote ile ya upangaji uzazi kwa muda wa miezi 12 kisha kutoweza kupata ujauzito.

 

AINA ZA UGUMBA

Ugumba wa asili – Hii ni pale inapotokea mwanaume na mwanamke hawajawahi kutungisha mimba kabisa maishani mwao hata baada ya kukutana kimwili kwa muda wa mwaka mmoja na zaidi bila kutumia njia yoyote ile ya kuzuia kupata mimba.

 

Ugumba unaotokea baadaye maishani – Hii ni pale ambapo wote wawili, mwanamke na mwanaume wameshawahi kupata ujauzito au kutungisha mimba angalau mara moja maishani mwao na baada ya hapo hawajafanikiwa kupata au kutungisha mimba tena.

 

Asilimia 30-40 ya tatizo la ugumba huwakumba wanaume na asilimia 40-50 ya tatizo hili huwakumba wanawake, wakati asilimia 10-30 zilizobakia za tatizo hili husababishwa kwa pamoja na matatizo kati ya wanaume na wanawake, hapa sababu halisi hazijulikani.

Kwa wale wenye afya njema, uwezekano wa kupata au kutungisha mimba iwapo watajamiiana mara kwa mara kwa mwezi ni asilimia 25-30. Wanawake hufikia kilele cha kupata ujauzito wakiwa na miaka kuanzia 20. Mwanamke aliye na umri wa zaidi ya miaka 35 (au baada ya miaka 40) ana uwezekano wa kupata ujauzito kwa asilimia 10 tu na haishauriwi kubeba mimba mwanamke akiwa na miaka hiyo.

 

Mimba hutungwa baada ya mwanamke kutoa yai kutoka katika moja ya ‘viwanda’ vyake vya mayai ya kike yaani ovaries, kitendo hiki hujulikana kama ovulation. Yai husafiri hadi kwenye mfuko wa uzazi ujulikanao kama uterus kupitia kwenye mirija ya uzazi inayojulikana kama mirija ya fallopian.

 

Mbegu moja ya kiume ni lazima itungishe au iungane na yai au mayai ya kike wakati yai likielekea kwenye uterus. Baada ya mbegu ya kiume na yai la kike kuungana, muunganiko uliotengenezwa yaani kiinitete hushuka mpaka kwenye mfuko wa uzazi na kujiwekeza hapo ili kiendelee kuwa kiumbe.

TATIZO LA UGUMBA KWA MWANAMKE

Tatizo la ugumba linaweza kutokea wakati wa yai au kiumbe kilicho ndani ya mfuko wa uzazi (uterus) kushindwa kukua hadi kufikia kuwa mtoto, mayai yaliyo ndani ya mfuko wa uzazi kushindwa kujishikiza kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi (uterus lining), matatizo kwenye njia ya kupita yai au mayai wakati yanakwenda kwenye mfuko wa uzazi na matatizo ya mayai ya uzazi (ovaries) kushindwa kutoa mayai.

 

Tatizo la ugumba kwa wanawake pia husababishwa na matatizo katika mfuko wa uzazi na shingo ya kizazi kama uvimbe na matatizo katika mfumo wa kuganda damu. Sababu nyingine ni afya iliyodhoofika, matatizo ya kula, baadhi ya madawa au sumu, msongo wa mawazo, tatizo la kukosekana kwa usawa wa mfumo wa vichocheo mwilini na uzito uliopitiliza.

 

Sababu nyingine ni unywaji pombe kupindukia, kuwa na magonjwa ya muda mrefu kama kisukari, magonjwa ya kinamama, magojwa ya zinaa au saratani. Pia uvutaji sigara, madawa ya kulevya kama cocaine, bangi, hashishi nk, wanawake wanaopata hedhi bila kutoa mayai, kuwepo kwa cervical antigens ambazo huua mbegu za mwanaume hivyo kusababisha kwa mwanamke kutopata ujauzito.

UGUMBA KWA WANAUME

Tatizo la ugumba linaweza kutokea kwa mwanaume wakati wa kupungua idadi ya mbegu za kiume, mbegu kuzuiwa kutolewa na mbegu za kiume ambazo hazifanyi kazi yake vizuri.

 

Kwa mwanaume, tatizo la ugumba husababishwa na mazingira yaliyo na kemikali zinazoathiri uwezo wa mwanaume kumbebesha mimba mwanamke, kukaa sehemu zenye joto kali sana kwa muda mrefu, unywaji pombe kupindukia, matumizi ya madawa ya kulevya na kukosekana kwa baadhi ya vichocheo mwilini. Ugumba kwa mwanaume unaweza kutokea kwa sababu ya kuwa na magonjwa ya korodani au kwenye mishipa ya korodani.

 

TIBA YA UGUMBA

Tiba ya tatizo ni pamoja na ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa afya na kuwaelimisha wapenzi wawili. Kuna wanaume wengi ambao hufika kilele haraka wakati wa kujamiana na hivyo kutoa mbegu ya kiume mapema kabla ya muda muafaka, hii husababisha lawama zote hupelekwa kwa mwanamke pasipo mwanaume kugundua kuwa tatizo ni lake.

 

Tatizo lingine ni kutofahamu lini hasa ni muda muafaka wa kujamiana ili kushika mimba kwa urahisi. Kuna wanawake ambao hawajui hata mzunguko wao wa hedhi, yaani hawajui wanaanza na kumaliza hedhi lini na wakati wa hedhi wanatumika kwa muda wa siku ngapi. Ongeza nafasi yako ya kushika ujauzito kwa kujamiana angalau mara tatu kwa wiki kuelekea wakati wa ovulation au kujamiana wakati wa kipindi chote cha ovulation.

Comments are closed.