The House of Favourite Newspapers

Zijue dalili za Homa ya Bonde la Ufa na matibabu yake

0

RVF (1)

Homa ya Bonde la Ufa (RVF) ni moja ya magonjwa yenye asili ya wanyama ambayo pia huweza kuenezwa kwa binadamu, magonjwa haya kitaalamu hujulikana kama ‘Zuonosia’. Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo huanza kushambulia mifugo na baadae huweza kuenezwa kwa wanadamu pia. Maambukizi ya virusi vya ugonjwa huu yanaweza kusababisha dalili ndogo na ugonjwa hatari kwa wanyama na wanadamu.

Unatokana na nini?

Ugonjwa huu husababishwa na kirusi cha RVF ambacho ni miongoni mwa Jenasi (kundi la viumbe vyenye maumbile yanayofanana) ‘Phlebovirus’, moja ya Jenera 5 za Familia ya ‘Bunyaviridae’. Kirusi hiki kinaweza kusambaa kwa kubebwa na mbu au nzi wanaokula damu kutoka sehemu yenye maambukizi hadi sehemu isiyo na maambukizi.

Ulitokea wapi?

Ugonjwa huu uliripotiwa mara ya kwanza katika mifugo maeneo ya Bonde la Ufa la Kenya miaka ya mwanzoni mwa 1900, navyo virusi vyake vilitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1931 wakati wa uchunguzi kitaalamu wa kondoo katika shamba moja huko Bonde la Ufa la Kenya. Tangia hapo, milipuko/mizuko ya ugonjwa huu imekuwa ikiripotiwa kusini mwa Jangwa la Sahara na Kaskazini mwa Afrika.

Mizuko kwa kawaida hutokea katika misimu ya mvua nyingi inayosababisha ongezeko la idadi ya mbu. Mwaka 1997-1998 mlipuko mkubwa ulitokea Kenya, Somalia na Tanzania. Mnamo Septemba, 2000 kesi kadhaa za ugonjwa huu zilithibitika Saudia Arabia na Yemen, zikifanya kesi za kwanza kuwahi kuripitiwa nje ya bara la Afrika, hali hii iliongeza wasiwasi zaidi kwa mataifa mengine maana ugonjwa unaweza kusambaa zaidi sehemu zingine za Asia na Ulaya.

Unaenea jinsi gani?

Wanyama wafugwao kama vile ng’ombe, kondoo, mbuzi na ngamia wanaweza kuathiriwa. Ugonjwa huu mara nyingi husambazwa katika mifugo hawa kupitia mbu aliyebeba kirusi cha ugonjwa huu. Kirusi cha RVF kinaweza kumpata mtu wakati akishika damu au nyama yenye maambukizi wakati wa kuchinja, kupumua hewa ya eneo la machinjio ya wanyama lenye maambukizi, kukata nyama iliyo na maambukizi buchani, kunywa maziwa mabichi (yasiyochemshwa) ya mnyama aliyeambukizwa.

Pia, wakati wa kumsaidia kuzaa mnyama aliyeambukizwa, wakati wa kutoa huduma kwa mifugo iliyo na maambukizi au taka za vitoto vilivyozaliwa kwenye maambukizi au kuumwa na mbu walioambukizwa hasa aina ya ‘Aedes’.

Kirusi cha RVF kinaweza kusambazwa na nzi wanaokula damu. Hadi leo, hakuna ripoti inayodai kuna maambukizi kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine pia hakuna maambukizi yaliyoripotiwa kwa mtumishi wa afya waliochukua tahadhari za kujikinga na magonjwa wakati wakitoa huduma kwa wagonjwa wa RVF.

Una dalili gani?

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF) huchukua siku 2 hadi 6 tangu kuambukizwa hadi kutokea kwa dalili. Waliambukizwa wanaweza wasiwe na dalili zozote mwanzoni, baadhi wanaweza kupata dalili ndogo ndogo kama mafua na homa, kuumwa misuli na viungo na kuumwa kichwa.

Baadhi ya wagonjwa hupatwa na ugumu katika shingo, kukerwa na mwanga, kukosa hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika. Katika hatua za mwanzo, wagonjwa wa RVF wanaweza kufananishwa na wagonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo (Meninjitisi).

Dalili za RVF hudumu kuanzia siku 4 hadi 7, baada ya hapo mfumo wa kinga huitikia na kufanya virusi vionekane kwenye antibodi na huanza kupotea muda hadi muda. Hivyo utambuzi hufanywa kwa kutafuta antibodi za kukabiliana na virusi au uwepo wa virusi vyenyewe katika damu.

Bainisho la ugonjwa huu linaweza kufanyika kwa vipimo vya damu kama ELISA/EIA kuangalia antibodi IgM. Kirusi chenyewe kinaweza kugundulika kwenye damu kipindi cha mwanzo cha ugonjwa kwa vipimo vya antijeni na RT-PCR.

Ingawa wengi walioambukizwa huwa na dalili ndogo, asilimia chache hupata dalili kali zaidi. Dalili tatu kali, moja au zaidi kati ya hizo hufanya hali ya mgonjwa kuwa mbaya zaidi. Dalili hizo ni Ugonjwa wa Macho (kupoteza uwezo wa kuona) huwapata 0.5 – 2% wiki ya tatu baada ya kuambukizwa, Meningo-ensefalatisi (inflamesheni ya ubongo na membreni zake) ambao husababisha maumivu makali ya kichwa na kuchanganyikiwa huwapata < 1% au Ugonjwa wa kutokwa damu (Hemorrhagic Fever) huwapata < 1%. Watu wanaovuja damu wana uwezekano wa kufa wa hata 50%.

Nini matibabu na chanjo yake?

Kwa kuwa wengi walioambukizwa huwa na dalili ndogo na za muda mfupi, hakuna tiba/dawa maalumu ya ugonjwa huu ingawa wagonjwa wenye dalili kali hupewa matibabu ya kuwasaidia kupunguza ukali wa ugonjwa. Wataalamu wa afya wameithibitishia FikraPevu kugundua kwa chanjo ya binadamu. Hata hivyo kufikia mwaka wa 2010, chanjo hii haipatikani katika sehemu nyingi kwa kuwa bado haijapewa leseni ya kuingia sokoni ingawa imejaribiwa kwa madaktari wa mifugo na walio katika maabara za mifugo kwa kuwa wao wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa.

Jinsi gani ujikinge?

Kuanzisha mfumo mzuri wa kutambua kesi mpya za RVF kwa kuwa ni muhimu katika kutoa ishara ya mapema kwa madaktari wa mifugo, ili waweze kuzuia mlipuko/mzuko wa ugonjwa huu. Kinga ya ugonjwa huu katika binadamu ni kwa kuchanja wanyama dhidi ya ugonjwa wenyewe, chanjo lazima ifanywe kabla ya mzuko kwa sababu ikifanywa wakati wa mzuko inaweza kuzorotesha hali hii.

Kuzuia mifugo kuhama kutoka sehemu ya maambukizi kwenda sehemu nyingine wakati wa mzuko. Ikiwa kuna mzuko, wananchi wanashauriwa kuendelea kujikinga na hali hatarishi kama damu ya wanyama, kujikinga na mbu & nzi wanaokula damu, kupika nyama na maziwa vizuri kabla ya kula/kunywa.

Wahudumu wa afya kuendelea kujikinga na damu kwa vifaa kama mipira ya mikono wakati wakihudumia wanaohisiwa au wenye RVF. Kuharibu vizalia vya mbu na kuua mbu wenyewe ili kuzuia kuendelea kusambaza ugonjwa huu na kujikinga dhidi ya kuumwa na mbu & nzi wanaofyonza damu kwa kutumia mafuta ya kupaka ngozi yanayoua wadudu au kuvaa nguo za kufunika ngozi ya mwili.

Vilevile, mamlaka za hali ya hewa zinapaswa kutoa utabiri wa hali ya hewa mapema hasa kuhusu mvua nyingi ambazo huchochea mbu wengi kuzaliwa ambao husambaza virusi vya RVF kutoka sehemu moja hadi nyingine na kusababisha mzuko wa ugonjwa huu.

Ugonjwa huu unaweza kusababisha athari za kiuchumi kwa vifo na kuharibu mimba kwa wanyama walioambukizwa. Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi inahitaji zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kuwapatia chanjo mifugo wote nchini, kitu kisipofanyika kinaweza kugharimu watu uhai na kugharimu serikali mabilioni ya pesa zaidi ya ile ingetumika kutolea chanjo.

CREDIT: FIKRA PEVU

Leave A Reply