The House of Favourite Newspapers

Zijue Hasara za Ushauri wa Kimapenzi kwa rafiki yako?

Couple-in-BedKARIBU tena msomaji wangu katika kona yetu hii ya Sindano za Mahaba. Natumai ni mzima wa afya bila shaka unaendelea na ujenzi wa taifa, kwa wale wagonjwa niwapeni pole Mwenyezi Mungu atawapa wepesi na mtapona.

Leo katika kona yetu hii nitaongelea hasara za ushauri wa kimapenzi. Wengi wamekuwa wepesi sana kukimbilia kwa rafiki zao ili kuomba msaada wa mawazo ya nini wafanye kwenye mapenzi. Imani iliyojengeka kwa watu wengi katika jamii yetu ni kuwa ushauri ni kitu muhimu sana kwa kila hatua.

Kwa mtazamo wa haraka unaweza kuishia kwenye ukomo huo wa fikra na kuamini juu ya ushauri wa mtu kukufikisha mahali sahihi kwenye mapenzi. Unapokerwa na mpenzi unakimbilia kushauriwa na wakati mwingine hata unapotaka kuoa au kuachana na umpendaye, unamuomba rafiki yako ushauri.

Je, umeshawahi kufikiria hasara za kuomba ushauri wa kimapenzi kwa rafiki yako? Hebu ungana nami nikumegee kidogo hasara za ushauri.

UTAKUPOTOSHA

Ni wazi kwamba kipimo cha uelewa kinatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Ifahamike kuwa, uhodari wa mambo nao hutofautiana, mtu anaweza kuwa mahiri katika siasa na akaaminika kwenye jamii, lakini ukimpelekea suala la mapenzi anakuwa hajui kitu, hivyo ni rahisi kukupotosha.

Uchunguzi unaonesha kuwa, wapenzi wengi sana hupotoshwa na rafiki zao wasiokuwa na uelewa wa kutosha juu ya tatizo au suala husika la kimapenzi. Ni vema kuwa makini unaposhauriwa.

UTARAHISISHA MAMBO

Mara nyingi washauri huwa si wao wanaokabiliana na mambo, hivyo ni rahisi kwao kupima vitu kwa juujuu tu na kushauri kirahisi. “Duuh kakupiga namna hii, aaa huyu si mwanaume kwa kweli ni bora ukaachana naye.” Anasema ni bora kuachana naye kwa sababu haumizwi na kuachana, unayeachana ni wewe anayekushauri.

“Mkubali tu bwana unalaza damu, hiyo tabia yake ya uhuni atabadilika, shosti unataka kuacha bahati ipite?” Kwa mshauri ni rahisi kusema hivyo lakini kumbuka ukubwa wa tatizo hatimaye utakabiliana nao wewe. Hii ina maana kwamba, unapofikiria kuhusu ushauri ufikirie pia kuhusu kushauriwa jambo kirahisi, ukiuvaa mkenge mwenye kuumia utakuwa ni wewe.

UTAKUGEUZA

Ulimwenguni kuna aina zaidi ya 1,000 za mapenzi na kila mmoja anatajwa kupenda kwa staili zake. Mapenzi ni kama chembe hai nyekundu zilizopo kwenye damu ya mwanadamu ambazo zinaelezwa na wataalam kuwa hazifanani hata kidogo. Uzoefu unaonesha kuwa, washauri wengi hushauri kwa uzoefu wao, lakini je, ni sahihi uzoefu huo uwe msaada kwa mtu mwingine?

Jibu ni hapana, kinachotokea mara nyingi kwenye ushauri ni mtu kumfanya mwenzake awe kama yeye alivyo, yaani apuuze aamue na apende kama staili yake, jambo ambalo haliwezekani kabisa kwenye mapenzi.

Vipi Mathayo ageuke ghafla awe kama John kwenye suala la mapenzi? Ushauri ni muhimu lakini upime kama unalingana na matakwa yako.

UTAKUONDOLEA UJASIRI

“Kwa maelezo hayo mumeo ni malaya sana, naona itakuwa vigumu kumbadilisha ni bora ukaanza maisha yako kwa sababu kuna siku hali itakuwa mbaya.”

Huu ni ushauri unaoweza kumuondolea mtu ujasiri wa kukabiliana na tabia ya mumewe hadi kufikia hatua ya kumrekebisha.

Ushauri huondoa ujasiri wa kukabili tatizo hasa pale anayeku-shauri atakapo-lipeleka suala lako kwenye njia ngumu isiyokuwa na ufumbuzi. Ikumbukwe kuwa anayeamini kushindwa ni mshauri lakini wewe kama mwanamke unaweza kusimama kutetea penzi lako na kuliweka sawa mpaka jamii ikasema: “Jamani huyu dada kamrekebisha sana mumewe kaacha ulevi.”

UTAKUNYIMA FURSA

Kwenye mapenzi kuna fursa nyingi za mafanikio ambazo unaweza usizipate ukiwa mtu wa kusikiliza sana ushauri wa watu.

Baada ya kuangalia madhara ya ushauri wa kimapenzi sasa tugeukie katika njia za kuzuia watu wasiingilie mapenzi yenu.

Udhibiti wa taarifa kwa wengine 

Kadiri unavyoelezea uhusiano wako kwa watu wengine ndivyo unavyowapa nafasi kutoa maoni na hata kudhani kuwa wana dhamana ya kukuelekeza unavyotakiwa kuishi na mwenza wako.           Hivyo basi, chukua muda wa kutosha kutafakari na kufanya uchunguzi kuhusu masuala yako ya uhusiano kabla haujaanza kutafuta maoni, ushauri kwa watu wengine.

Upekee wa mambo

Tambua kuwa tabia ya mpenzi wako inaweza kuwa ni ya kipekee, mazingira pia ya tukio linalokufanya utake ushauri au maoni kwa wengine yanaweza kuwa ni ya kipekee, hivyo ushauri au maoni utakayopokea yanaweza yasikusaidie moja kwa moja katika suluhisho lako.

Ukitambua hili, utafanya bidii ya kujenga uwezo binafsi wa kuchambua tatizo unalokumbana nalo.

Kwa leo niishie hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.