Zijue Njia 10 Za Kuwa Tajiri Kama Dangote -2
Wiki iliyopita tulijifunza namna ambavyo tajiri namba moja barani Afrika, Aliko Dangote alivyofanikiwa kuuaga umaskini kupitia njia kumi (10) ambapo tuliishia njia ya tano ambayo ni kujenga ushirikiano na watu na kutafuta mpenyo mkubwa. SASA ENDELEA…
Tuliona jinsi ambavyo Dangote alipata mpenyo wake mkubwa pale alipofanikiwa kupata leseni ya kuagiza sementi kutoka nje ya Nigeria.
Halikadhalika, tajiri Bill Gates, mpenyo wake mkubwa ni pale aliposaini mkataba na kampuni kubwa ya Kompyuta ya IBM. Je, wewe mpenyo wako mkubwa ni upi? Ni lazima ujue ni wapi unapotakiwa kuanzia au kutokea na huo ndiyo uwe mpenyo wako.
6: AMINI KUWA UNAWEZA KUTAJIRIKA HATA HAPO ULIPO SASA
Kwa mujibu wa Dangote, yeye anaamini kabisa kuwa, ili mtu uweze kujenga biashara imara na yenye mafanikio ni lazima uwe na imani thabiti juu ya nchi yako, uamini kwamba fursa zimejaa tele kila mahali, ila tu kinachotakiwa ni mtu awe na jicho la kijasiriamali, lenye uwezo wa kuona fursa hizo pale ambapo mtu wa kawaida asingeona kirahisi.
Dangote anakutia moyo kuzitafuta fursa ndani ya nchi yako na siyo kwenda kuhangaika katika nchi za watu ambako hutakuwa na uhakika wa mafanikio.
7: FANYA KAZI KWA BIDII
Hili halina ubishi. Dangote anasisitiza mara zote anapopata nafasi ya kuwaelezea watu siri zake za mafanikio. Hebu soma maneno yake mwenyewe hapa chini:
“Mwenyewe huwa nafurahia sana maisha lakini nakuwa na furaha zaidi ninapokuwa nafanya kazi. Ninaamini katika kufanya kazi kwa bidii na moja ya siri zangu za mafanikio kufanya kazi kwa nguvu zangu zote.”
Ingawa Dangote hufanya kazi kwa bidii sana lakini hafanyi kazi tu ilimradi amefanya, la hasha, hutumia akili na zaidi ya yote hupanga nini cha kufanya kabla hajafanya kazi zenyewe. Ni lazima ufanye kwanza utafiti wa kutosha ili upate dira na mwelekeo wa kile unachotaka kukifanya.
8: RUDISHA KWA WALE WALIOKUPATIA
Hata kama ukiwa na juhudi ya kazi vipi lakini kamwe huwezi ukasimama na kudai eti mafanikio yako hakukuchangia mtu, wateja wenyewe wa biashara yako ni miongoni mwa watu wanaochangia ufanikiwe. Huwezi kutajirika kwa mikono yako mwenyewe. Kuna wafanyakazi, wadau mbalimbali, wabia, taasisi, makampuni na jamii kwa jumla, wote wana mchango kwako ili ufanikiwe. Cha msingi ni kujichanganya na kujenga imani kwao ili wakuamini.
Kwa namna moja au nyingine, kuna wakati ulihitaji msaada fulani na ukasaidiwa na watu/mtu fulani ndipo ukaweza kufanikiwa. Kwa hiyo basi ili waendelee kukusapoti au kukuunga mkono, huna budi kuwakumbuka kwa kuwarudishia sehemu ya kile walichokupa. Kuna njia nyingi za kuwarudishia, ikiwemo misaada ya kijamii, kufadhili shughuli mbalimbali na mengine mengi ya kujitolea. Hicho ndicho anachokiamini Dangote na wewe ukifanya hivyo lazima utafanikiwa.
9: HESHIMU NA KUTII
SHERIA ZA NCHI
Katika hili, masuala kama ya kukwepa kodi na kutumbuliwa majipu, hakuna, unatakiwa kuhakikisha sheria zote na taratibu zilizowekwa na mamlaka halali unazifuata. Dangote anawashauri wajasiriamali kuwa watu wenye kufuata sheria za nchi pasipo kupindishapindisha ikiwa ni pamoja na kulipa kodi halali.
10: NI LAZIMA UJASIRIAMALI UWE NDANI YA DAMU
Ni lazima uwe na tabia za kijasiriamali, huwezi kufanikiwa ikiwa hautazitilia maanani na kuziishi. Haitoshi tu kuzijua kinadharia, kila kitu utakachofanya, ukifikiri, ukiota, ukifanya jambo lolote lile basi liwe ni biashara na siyo kitu kingine. Roho ya kutafuta fedha utakayokuwa umeipanda kwa jinsi hiyo haitakufa kamwe hata ikiwa wewe kimwili utakuwa umekufa, yenyewe itaendelea kuishi miaka mingi baadaye.
Ni kama unavyoona wajasiriamali mfano wa akina Thomas Edison, hata baada ya kufa siku nyingi kampuni yake ya General Electrics bado ipo. Andrew Carnegie, kitabu chake Think & Grow Rich ni miaka zaidi ya 70 sasa na bado kinawavutia watu wengi duniani. Hata Mzee Warren Buffet aliyewahi kuwa mtu tajiri zaidi duniani, ingawa ameshazeeka sasa lakini bado ndani ya damu yake ujasiriamali unaendelea kuchemka. Ni lazima uwe muumini wa ujasiriamali.