Zimbwe Jr wa Simba: Haukuwa msimu bora kwetu kufikia malengo

MOHAMED Hussein Zimbwe Jr nahodha msaidizi wa Simba ameweka wazi kuwa 2023/24 haukuwa msimu bora kwao kutokana na kushindwa kufikia malengo yao.
Ipo wazi kwamba Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda ilipishana na mataji yote muhimu iliyokuwa inapambania mwanzo wa msimu.
Ni Ligi Kuu Bara, CRDB Federation Cup haya yote yalikwenda Yanga na katika Ligi ya Mabingwa Afrika iligotea hatua ya robo fainali.
Zimbwe amesema kuwa walikuwa na malengo ya kufanya vizuri kwenye mechi zao zote lakini haikuwa hivyo kutokana na matokeo kuwa tofauti.
“Ilikuwa ni msimu wenye ushindani na haukuwa bora kwetu kwa kuwa malengo yetu hatukutimiza, kwa yaliyotokea nina amini kwamba tutafanyia kazi msimu ujao tuwe bora.
“Mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kwani tunaamini kwamba wanapenda matokeo mazuri hata sisi pia tunapenda kuona inakuwa hivyo.”
Simba itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024/25 baada ya kugotea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 69.
Stori na Lunyamadzo Mlyuka, GPL