Zimebaki Siku Nne Dar Boxing Derby
KUELEKELEA katika pambano la Dar Boxing Derby ‘mwana ukome’ kwa sasa zimebakia siku nne kwa mabondia 30 kupasuana katika pambano linalotarajia kupigwa Oktoba 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kinesi Dar.
Oktoba 30, mwaka huu ndani ya Uwanja wa Kinesi inatarajiwa kupigwa pambano la Dar Boxing Derby ‘Mwana Ukome’ ambalo litawakutanisha Idd Pilali dhidi ya Ramadhan Shauri wakati Selaman Kidunda atacheza Jacob Maganga huku Francis Miyeyusho akitarajia kumvaa Adam Kipenga.
Pambano hilo ambalo limeandaliwa na Kampuni ya Peak Time Media, chini ya Mkurugenzi wake, Kepteni Seleman Semunyu na kudhaminiwa na Gazeti la Championi, Globla TV, Bongo Boxing Safari, Smart Gin, Furaha TV na ITV huku kiingilio kikiwa ni Sh 7,000 kawaida na Sh 20,000 kwa VIP.
Akizungumza na Championi Jumatatu, promota wa pambano hilo, Kepteni Seleman Semunyu alisema kuwa maandalizi ya pambano hilo yamekamilika na kwa sasa inasubiriwa siku kufika kwa mabondia hao kupanda ulingoni.
“Maandalizi yamekaa sawa hadi kufikia sasa, tumeweza kutembelea kambi za mabondia na kuona namna wanavyoweza kujiandaa kuelekea kwenye Dar Boxing Derby kuweza kushuhidia zile ngumi za mwana ukome.
“Nadhani kutoka leo Jumatano tutakuwa tumebakiwa na siku nne kabla ya kufikia Oktoba 30, ambayo itakuwa siku ya Jumamosi, kikubwa wadau na mashabiki wa ngumi waendelee kukata tiketi ili wasipate usumbufu wa kuweza kuingia ndani,” alisema Kepteni Semunyu.
IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam