The House of Favourite Newspapers
gunners X

Zitto Ahofia Kurudi Tanzania Kutokana Na Vitisho Alivyovipata

0

Zitto Kabwe ahofia kukamatwa, kufunguliwa mashtaka na kufungwa pindi atakaporejea nchini. hiyo inatokana na kile alichokiita mfululizo wa vitisho vilivyotolewa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

Hofu hiyo ya Zitto imeibuka baada ya Kiongozi Mkuu huyo ACT Wazalendo kuandika barua kwa Benki ya Dunia (WB) kuitaka kusitisha mkopo wa Dola za Marekani milioni 500 kwa Tanzania kutokana na kile alichodai kuna ubaguzi katika elimu kwa watoto wa kike waliopata ujauzito wakiwa shuleni.

 

Zitto alieleza hofu yake hiyo jana, akidai kuwa analichukulia kwa uzito suala hilo kwa kuwa upo mfano wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kupigwa risasi mjini Dodoma na hadi sasa ameshindwa kurejea nchini kutokana na hofu ya usalama wake.

 

“Ninachukulia vitisho hivi kwa uzito kwa sababu tuna mfano wa mwenzetu Lissu, lakini usije kushangaa ukisikia nimekamatwa na kufungwa nitakaporejea Tanzania kwa sababu sasa hivi kesi za utakatishaji fedha zinatumika kuwanyamazisha wakosoaji kwa sababu mashtaka yake hayana dhamana,” alisema.

 

Wiki iliyopita, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi, kuchunguza kitendo cha Zitto kuiandikia barua WB kuzuia mkopo huo ili kuona kama kuna jinai au la na kumchukulia hatua mbunge huyo kufuatia hoja binafsi iliyowasilishwa bungeni na Mbunge wa Siha, DK. Godwin Mollel (CCM), kutaka kuchunguzwa kwa jambo hilo.

 

Zitto kwa sasa yuko Amerika ya Kaskazini kwa shughuli ambazo chama chake hakijaziweka wazi kwa umma.

Leave A Reply