The House of Favourite Newspapers

Ndugai: Zitto Ananisumbua Sana, CAG Asipokuja Tutamuonyesha – Video

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai,  amesisitiza kuwa bunge lake siyo dhaifu hata kidogo kama ambavyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, alisema wakati akihojiwa nje ya nchi.

 

Ndugai amesema hayo leo kwatika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari na kusisitiza kuwa CAG huyo lazima aripoti kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Januari 21, mwaka huu vinginevyo asipofika ‘watamuonyesha’ huku akieleza kwamba mzozo na CAG ni wa muda lakini utamalizika muda wowote.

 

“Mzozo kati ya Bunge na CAG ni wa muda mrefu. Utamalizika muda wowote lakini siwezi kusema ni keshokutwa au lini. Hakuna kinachofichwa katika kamati, ndiyo maana wenyeviti wake (PAC na LAAC) wanatokea upinzani. Kama tungekuwa na nia ya kuficha kamati si zingeongozwa na CCM? Haya mambo ya ni ya kutunga na muda utaeleza kama tulikuwa na lengo la kuficha au kutokuficha.

 

“Zitto Kabwe ni miongoni mwa wabunge wanaonisumbua sana, amekuwa akipotosha mara kwa mara, hebu nisaidieni nimfanyaje? Mbunge mwenyewe yuko peke yake kwa chama chake, nikimfukuza nani atamwakilisha? Anatafuta umaarufu, sijafikiria hata kumuita.

 

“Suala la Tsh. Trilioni 1.5 lilitolewa maelezo na serikali mwaka jana (2018), si waichukue hiyo waichambue maana ina matumizi yote? Upinzani wa Tanzania shida yake ni upotoshaji mwanzo-mwisho. Ishu ilivyoanza hadi sasa inajulikana, tunachokilalamikia mnakijua. Tazama katika vitabu vya CAG kama kuna hoja ya Tsh trilioni 1.5. Hiyo haijawahi kuwa hoja.

 

“Hivi vyama vingine tulitakiwa kuviita vyama vya ‘ushindani’ na sio ‘upinzani’ maana hilo jina limepelekea kila kitu wanapinga tu hawana jema. Bunge hili sio dhaifu na kuhusu CAG suala liko palepale, atakuja tu kwenye Kamati ya Haki Kinga na Madaraka ya Bunge, asipofika tutamuonyesha.

 

“Sisi Tanzania tumeweka balozi nchi mbalimbali na maofisa ambao kazi yao ni kui-brand nchi yetu, hizo ni gharama. Marekani wanatupa misaada halafu wewe ofisa unatoka Tanzania unaenda kule unasema Bunge la Tanzania ni ‘bogus’. Sasa nyie mnaoshangilia watu wetu kwenda kuichanachana nchi yetu nje eti kwa sababu wana nafasi fulanifulani, hivyo ni vitu vya ajabu hata kama wewe ni mpinzani siyo upinzani huo.

 

“Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa unaendelea kama kawaida, sasa hivi upo kwenye ngazi ya kamati, tukianza bunge muswada unaingia, wao kama wanakimbiakimbia kwenye korido za Dar, muswada utatungwa.

 

“Nasema bunge siyo dhaifu… Sasa hivi wanasema tena, wengine wapo Segerea, wanarudia kusema serikali ni dhaifu? Wanakimbia kwa Ndugai wanafikiri kule ndo rahisi zaidi,” amesema Ndugai.

 

Mzozo kati ya Ndugai na CAG ulianza baada ya Profesa Assad wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kusema kushindwa kutekelezwa kwa ripoti anazowasilisha bungeni huenda kunatokana na udhaifu wa chombo hicho, kauli ambayo Ndugai alisema ni ya kudhalilisha Bunge na kumtaka kufika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa.

 

Spika amesimamisha Bunge kufanya kazi na ofisi ya CAG kwa muda hadi mzozo huo utakapotafutiwa ufumbuzi.

 

SPIKA – “CAG Asipokuja Nitamuonesha / Zitto Ningemfukuza Ila..”

Comments are closed.