The House of Favourite Newspapers

ZITTO KABWE AMALIZANA NA TAKUKURU

MBUNGE wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe, amaliza kuwasilisha ushahidi wa tuhuma za rushwa inayodaiwa kuhusisha viongozi wa juu Serikalini katika mradi wa uzalishaji chuma wa Mchuchuma na Liganga kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

 

Zitto ambaye jana aliandika maelezo ya ushahidi huo na kumalizia kutoa ushahidi huo leo, amema; “Nimemaliza mahojiano na TAKUKURU Kuhusu Taarifa Nilizotoa kuwa Mradi wa Mchuchuma Liganga unacheleweshwa kwa makusudi na kufaidisha kampuni zinazoagiza bidhaa za chuma kutoka nje kwa mradi wa Reli. Leo nimeandika maelezo kwa takribani muda wa saa tatu na jana saa mbili.

 

“Nimewaomba TAKUKURU wafanye Uchunguzi wao kwa weledi kwani naamini kuwa tendo la hongo limefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya TAKUKURU namba 11 ya mwaka 2007. Kuchelewa kutoa maamuzi ya mradi huu imeipa Tanzania hasara ya mpaka $12bn kwa mwaka.

 

“Nimewasihi pia TAKUKURU kuwa njia hii hii waliyotumia kuniita kufuatia Taarifa nilizoandika hapa Twitter waitumie pindi Viongozi wa Serikali au wapambe wa Serikali na vyombo vyao wanapotoa matamko dhidi ya Wananchi, Wafanyabiashara, Wakulima, Wavuvi Au Viongozi wa upinzani.

 

Zitto alisema aliwasilisha vielelezo hivyo kwa kuwaeleza zilizomfanya aamini kuwa ucheleweshaji wa mradi huo ni wa makusidi, unaofanywa na watendaji wa Serikali kwa ajili ya kufaidisha kampuni zinazoagiza bidhaa zinazotumika katika miradi ya chuma ikiwamo kampuni inayojenga reli ya kati na inayojenga bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Tanga.

 

Wiki iliyopita Zitto alitoa tuhuma kwamba viongozi wa juu wa Serikali wanahusika katika rushwa ya kuzisaidia kampuni za nje kuuza chuma nchini na kuyumbisha kwa makusudi uendelezaji wa uzalishaji wa chuma cha Mchuchuma na Liganga kwa kumkwamisha mwekezaji aliyekuwa tayari kuzalisha chuma kwa ajili ya miradi ya ndani na ya nje.

 

Comments are closed.