The House of Favourite Newspapers

Zuchu Amuonea Aibu Mondi

0

PAMOJA na kukanusha kwamba wao si wapenzi, lakini ishara nyingi zinaonesha vingine baina ya mastaa wawili wa muziki wanaowika zaidi nchini Tanzania, Nasibu Abdul almaarufu Diamond Platnumz na msanii wake, Zuhura Othman au Zuchu, IJUMAA linakupa uchambuzi kamili.

 

Wengi wa waliowashuhudia kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar, usiku ule wa Valentine’s Day, likiwemo gazeti hili la IJUMAA wanakiri kwamba kuna asilimia zaidi ya tisini kwamba kuna uhusiano wa kimapenzi kati ya Diamond au Mondi na Zuchu.

 

Pamoja na kwamba waliingia Mlimani City wakiwa kwenye gari moja kama wapenzi kisha kuoneshana mahaba ya kutosha kwenye zulia jekundu (red carpet) kwa kushikana kimahaba, lakini walipofika ndani kila mmoja alikaa kwenye meza yake na wageni wake.

 

ZUCHU KUMUONEA AIBU DIAMOND

Hata hivyo, pamoja na kukaa mbalimbali ukumbini humo, lakini bado kulikuwa na ishara kedekede wakipeana viashirio vya kutazamana na kutamaniana kama wafanyavyo wapenzi walioshibana, lakini kubwa lililokuwa waziwazi ni kitendo cha Zuchu kumuonea aibu Diamond na kusababisha ukumbi kurindima kwa minong’ono kwamba kwa vyovyote kuna kitu kinaendelea kati yao na siyo bure.

 

Tofauti na wakati mwingine wowote ambao Diamond na Zuchu wameonekana kwenye matukio tofauti, lakini siku hii ilikuwa tofauti mno kwani mahaba yao yalikuwa siyo ya nchi hii. Tofauti na siku hii, nyakati zote ambazo wawili hao wamekuwa pamoja walionesha tabia za mtu na msanii wake au mtu na bosi wake, lakini safari hii ishara za mapenzi zilikuwa waziwazi;

 

baadhi ya watu walisikika wakisema hata kama mtu hawezi kusoma, lakini anaweza kuona hata kwa picha.

 

ASIMIA 90 NI WAPENZI

Wengi wanakiri kwamba, kuna asilimia zaidi ya tisini (90%) ya uwezekano wa Diamond na Zuchu kuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa sababu mbali na Zuchu kumuonea aibu Diamond pia Diamond naye kuna wakati alikuwa akimuonea aibu Zuchu hivyo wakawa wanaoneana aibu.

“Ukimtazama Zuchu namna alivyokuwa akimshika au kumsogelea Diamond, sura na lugha ya mwili vilikuwa vinaongea mno kiasi cha kutetemeka na kushindwa kumtazama usoni kutokana na kuona aibu.

 

“Wakati Zuchu akipafomu, kuna wakati alimfuata Diamond kisha akamvua koti kumpunguzia joto kama wafanyavyo wapenzi au wanandoa walioshibana na kumuomba waendende kupafomu, lakini matukio hayo yote waliyafanya kimahaba mno huku mashabiki wakitamani wafanye kitu kikubwa pale ukumbini kutokana na shangwe walilopigiwa kiasi cha Zuchu kutamani kufunguka tu, lakini inawezekana hakuruhusiwa kufanya hivyo.

 

“Kwa wataalam wa saikolojia hawakuwa na sababu ya kuendelea kudadisi au kutaka uthibitisho, bali lugha za miili yao na matukio waliyoyaonesha yalitosha kuthibitisha kuwa kuna uhusiano wa kimapenzi,” anasema mmoja wa mashuhuda ukumbini humo.

 

Watu wa karibu wakiwemo baba wa kambo wa Diamond, Uncle Shamte, Baba Levo, Diva, Juma Lokole na wengine; wote walionesha shangwe kuonesha kuna jambo linaloendelea kati ya wawili hao. Vyanzo vya ndani vinasema kuwa, siku hii haikuwa rasmi kuthibitisha hilo, badala yake kuna siku inakuja kwa ajili ya kuweka mambo yote hadharani.

 

DIAMOND HUANZA HIVIHIVI

Wapo wanaosema kuwa, Diamond amekuwa na tabia hiyo ya kuanzisha uhusiano kwa staili hiyo kama alivyofanya kwa ‘maeksi’ wake, Wema Sepetu na Tanasha Donna kwani mazingira yalifanana kwa asilimia zote kama ilivyo kwa Zuchu.

 

Mbali na ishara hizo za ukumbini, lakini kabla ya hapo, Diamond na Zuchu wamekuwa na ishara nyingi za kimapenzi ikiwemo kuvaa saresara za nguo na viatu huku wakipostiana na makopakopa kama yote.

 

DIAMOND AFUNGUKA

Kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na Zuchu, akiwa kwenye zulia jekundu (red carpet) Diamond anafunguka kuwa, uhusiano wake na Zuchu ni kama wa mzazi na mtoto wake huku akitulipilia mbali madai ya mitandaoni kwamba ni wapenzi. “Zuchu ni msanii wangu na siyo mara ya kwanza kuja naye redcarpet.

 

Nilikuja naye mara ya kwanza nikamtambulisha alikuwa mtoto. Amekua sasa ni msanii mkubwa. Kwa hiyo namleta tena, mtoto kwa baba hakui,” anasema Diamond akisitasita.

 

Vilevile, Diamond aligusia mambo na uhusiano wake wa kimapenzi akisema kuwa yupo kwenye uhusiano unaofanya vizuri na hivi karibuni ataweka wazi uhusiano wake na kuwaomba mashabiki kuendelea kusikiliza kazi zake.

 

Ikumbukwe kwamba, kabla ya tukio hilo, Zuchu alidokeza kwamba siku hiyo ya Wapendanao atafika ukumbini na mpenzi wake na akafika na Diamond hivyo kuwafanya watu kuamini kinachosemwa mitandaoni.

STORI; WAANDISHI WETU, DAR

Leave A Reply