The House of Favourite Newspapers

Zuchu Anuka Pesa

0

STAA mpya wa Bongo Fleva, Zuhura Othman Soud almaarufu Zuchu ambaye kwa sasa anakimbiza na wimbo wake wa Kitu, ameonesha namna anavyonuka pesa baada ya hivi karibuni kuhamia kwenye mjengo wa kifalme, Global Publishers ina exclusive.

Global Publishers imebaini kwamba, mrembo huyo mwenye nyota ya kipekee ambaye pia ni mtoto wa Malkia wa Afrika, Khadija Omary Kopa anaishi kwenye mjengo huo wa ghorofa uliopo ushuani Mbezi- Beach jijini Dar.

“Hivi mna taarifa kuwa Zuchu amehamia kwenye mjengo wa kifahari? Yaani kifupi ni kwamba hataki apate shida kabisa mtoto ana-enjoy tu maisha,” alisema mmoja wa majirani zake kwa sharti la kutotajwa.

NI WHITE HOUSE

Ili kupata ukweli wa maneno hayo, Global ilisogea karibu na mjengo huo ambapo lilishuhudia mambo makubwa.

Kwanza, binti huyo wa Kizanzibari yeye halali kwenye chumba kimoja na ndoo za maji kama waishivyo mabinti wengi mjini wanaojiita pisi kali.

Ni bonge moja la mjengo, siyo banda la uani la kufugia kuku; kifupi maisha ameyapatia.

Wakazi wa eneo hilo wao hupenda kuuita mjengo huo White House kutokana na kutawaliwa na rangi nyeupe kila kona huku mandhari yake ikiwa ni yenye kuvutia.

 

KIJANA ANAYEISHI NAYE

Baada ya waandishi wetu kushangaashangaa kidogo hali ya hewa ya eneo hilo, waliamua kubisha hodi ambapo baada ya muda mrefu kupita alitoka nje kijana aliyejitambulisha kuwa yeye ni ‘shamba boi’ nyumbani hapo ambapo mazungumzo yalikuwa hivi;

Global : Mambo vipi?

SHAMBA BOI: Poa, ninyi ni akina nani na niwasidie nini?

Global : Sisi ni waandishi wa Global, tuna shida ya kumuona Zuchu…

SHAMBA BOI: Zuchu hayupo (yupo Afrika Kusini), amesafiri kikazi.

Global : Oooh! Kumbe, hivi hapa anaishi na nani?

SHAMBA BOI: Anaishi yeye mwenyewe na baadhi ya vijana wake.

Global : Ina maana unataka kusema mama yake haishi hapa na wala hana boyfriend (mpenzi wa kiume)?

SHAMBA BOI: Mama yake haishi hapa, kuhusu kuwa na mpenzi sijui, lakini yote yanawezekana kwa sababu yule ni mtoto wa kike na ni mrembo ila binafsi sijawahi kumuona akija hapa.

Global : Ni kweli kwamba huu mjengo amepangishiwa na bosi wake Diamond?

SHAMBA BOI: Mmmh! Mimi mwenyewe ndivyo nilivyosikia, lakini sina uhakika sana.

Global : Poa, tunashukuru.

SHAMBA BOI: Haya karibuni.

MAJIRANI WAFUNGUKA

Global pia ilizungumza na baadhi ya majirani wa Zuchu ambao nao kwa upande wao walithibitisha mrembo huyo kuishi katika mjengo huo.

“Hii nyumba ni kweli anaishi Zuchu, hana muda mrefu tangu amehamia hapa,” alisema jirani mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Gudluck.

 

KWANI ZUCHU MWENYEWE ANASEMAJE?

Waandishi wetu walimtafuta mwanadada huyo mwenye sauti tamu ya kumtoa nyoka pangoni ili kuthibitisha kama kweli hayupo, lakini simu yake haikupatikana.

 

SOMO KWA MASTAA WENGINE

Pongezi ziende kwa viongozi wa Lebo ya WCB ambao wamejitahidi kadiri wawezavyo ili kuhakikisha msanii wao anakuwa bora kila siku, lakini siyo kuwa bora tu, bali hata kuishi maisha mazuri ya ndoto zao kwa sababu kuna lebo nyingi ambazo zinasaini wasanii na mwishowe wanakuwa hawana mwelekeo.

 

Pia ni Zuchu mwenyewe, mbali na kuwa watu wengi wanasema kuwa anabebwa na lebo na ukubwa wa jina la bosi wake ambaye ni Diamond Platnumz, lakini naye amejitahidi kuweka juhudi zake binafsi ambazo ndizo zimemfanya aishi maisha ya kifahari ambayo pengine alikuwa akiyatamani siku zote.

 

NYIMBO ZA ZUCHU ZILIZOTIKISA

Baada ya kusajiliwa na lebo hiyo Aprili 8, 2020, Zuchu alifanikiwa kutoa nyimbo ambazo zilifanya na zinafanya vizuri huku akitambulika na Ngoma ya Wana ambayo hadi sasa ina mamilioni ya watazamaji ndani ya muda mchache tangu kutoka kwake.

 

Baada ya ngoma hiyo, Zuchu akaendelea kuachia mikwaju mikali ambayo nayo ilifanya poa kwenye platforms zote ikiwemo YouTube. Ngoma kama Kwaru, Nisamehe, Raha, Mauzauza, Hakuna Kulala, Ashua na Tanzania ya Sasa zimefanya vizuri mno kwani hadi sasa zimejikusanyia mamilioni ya watazamaji na wasikilizaji akiwa ni msanii wa kwanza wa kike kwa Ukanda wa Afrika Mashariki kufikisha zaidi ya watazamaji (views) milioni 100.

 

ZUCHU ANANUKA PESA

Global imebaini kwamba, mastaa wengi Bongo wamekuwa wakihusudu maisha ya matumizi ya hali ya juu na kujisahau kufanya uwekezaji, jambo ambalo wengi wamekuwa wakiishia kubaya baada ya sanaa kuwakataa.

 

Kupitia ngoma zake jinsi zinavyofanya poa kwenye mitandao ya kupakua muziki na kazi za wasanii, Zuchu anaingiza mkwanja mrefu kwa kila mwezi.

Anakadiriwa kuingiza kiasi cha zaidi ya Dola za Kimarekani kati ya 19,000 hadi 29,000 kwa mwezi ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 66.1 za Kitanzania; kiasi ambacho anawafunika wasanii wengi ambao wamemtangulia na sasa ananuka pesa.

 

SHOO ZA KUMWAGA

Julai 18, mwaka jana, Zuchu aliangusha bonge la shoo pale Mlimani City iliyokwenda kwa jina la I AM ZUCHU Asante Nashukuru; shoo ambayo ilikuwa ni habari ya mjini, kwani alijaza nyomi tena kwa kulipia kiingilio chenye hadhi.

Baada ya hapo zilifuata shoo nyingi ambapo alianza kufanya shoo moja kwa shilingi milioni 20, lakini sasa anafanya kwa shilingi milioni 46 kwa shoo moja

 

HESHIMA MITANDAONI

Jambo lingine kubwa ambalo Zuchu amelipata, ni kupata tuzo ya kufikisha subscribers (watazamaji) zaidi ya laki moja kwenye Mtandao wa YouTube na mamilioni ya wafuasi kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ndani ya muda mfupi.

 

KUKUBALIKA NA MARAIS

Rekodi nyingine ambayo Zuchu ameweza kuiweka ni kukubalika kwa viongozi wa Serikali tangu enzi za Hayati Dk John Pombe Magufuli na sasa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Dk Hussein Mwinyi wa Zanzibar.

Imeandikwa na Khadija Bakari na Memorise Richard.

Fijum

Leave A Reply