The House of Favourite Newspapers

Zuchu Bado Siamini Kama Nipo Wasafi

0

“KUKUHINI kusokwisha umeangukia pemani…Roho yanidadarika kanshatoka shetwani..Nimeumbiwa makosa mwanadamu na mimi…Moyo umekunja ndita nakumis jamani..Ngumu safari ilifanya njiani ushukiee…

Ukakosa siti miliki gari yako mwenyewe…Nikajivika masharti nikajiona mi ndiyo mie…

 

Kweli mbaya halisi na wema akosie…Nisamehee…”Kwa sasa kwenye Bongo Fleva huwezi kuacha kulitaja jina la Zuchu ambaye amekuwa ni msanii aliyetikisa behewa la burudani kwa muda mfupi tu.

 

Hayo ni mashairi ya ngoma yake ambayo inasumbua pale YouTube.Zuhura Kopa ‘Zuchu’ ni zao jipya kunako lebo kubwa ya muziki Bongo ya Wasafi Classic Baby (WCB), ambalo limefanya maajabu kwa muda mfupi.

 

Zuchu amejizolea umaarufu kupitia mama yake, Malkia wa Taarab Afrika Mashariki na Kati, Khadija Omari Kopa.Zuchu alitambulishwa rasmi kuwa memba wa lebo hiyo miezi mitatu iliyopita kama second lady baada ya first lady Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’.

 

Sasa Zuchu amekuwa msumari wa moto kwa Darleen na anatishia kukalia kiti cha first lady kufuatia kufanya wandaz na kuweka rekodi nyingi kwenye Bongo Fleva.Amefanya poa na ngoma kali zote za Wana, Kwaru, Raha, Ashua, Mauzauza, Hakuna Kulala na Nisamehe na zote zikiwa ndani ya extended playlist yake (EP).

Baada ya kuachia ngoma hizo ambazo zimejikusanyia watazamaji zaidi ya milioni 10 kwenye YouTube, Zuchu ameendelea kutikisa baada ya kupata tuzo ya kufikisha subscibers (wafuasi) laki moja na kumfanya kuonekana kama msanii wa kwanza wa kike aliyetazamwa na watu wengi kwa muda mfupi.

 

Safari yake ya muziki imekuwa ni yenye maajabu kwani alisota Wasafi kwa muda mrefu bila kuona mafanikio, lakini muda wa Mungu ulipofika ndipo akaonekana.Mbali na aina yake ya uimbaji wenye mashairi matamu na yenye mahadhi ya Pwani, Zuchu amekuwa ni msanii wa kike wa tofauti kutokana na kujaaliwa kipaji kikubwa cha uandishi ambacho kimekuwa ni adimu kwa wasanii wa kike hapa Bongo.

Zuchu amekuwa akiandika ngoma zake mwenyewe bila kutegemea mtu mwingine.Hivi karibuni ameendelea kupasua anga, baada ya kuachia Ngoma ya Tanzania ya Sasa ambayo imezungumzia na kusifia uongozi wa Rais Dk John Pombe Magufuli.Zuchu anatarajiwa kufanya shoo ya kibabe ambayo itakuwa ni kama shukrani zake kwa mashabiki kumpokea kwa mikono miwili kwa muda huo mfupi.

 

IJUMAA SHOWBIZ imeketi kitako na Zuchu na kufanya naye mahojiano maalum (exclusive) ambapo anafunguka mengi ikiwemo ishu nzima ya kusota Wasafi hadi kusajiliwa kiasi kwamba hadi sasa bado haamini kama ndoto yake imetimia;

 

IJUMAA SHOWBIZ: Zuchu hongera kwa kazi nzuri ulizotoa.

ZUCHU: Asante sana.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Kwanza kabisa kwa mara ya kwanza kutambulishwa rasmi kama msanii wa WCB ulijisikiaje?

 

ZUCHU: Ilikuwa ni furaha isiyo na kifani, maana ni ndoto ambayo niliipambania kwa muda mrefu. Hivyo naamini sasa malengo yangu yanakwenda kutimia ingawa bado kuna muda siamini kama nipo Wasafi.

IJUMAA SHOWBIZ:Mashabiki wangependa kujua safari yako hadi kufika ulipo sasa?

 

ZUCHU: Safari yangu haikuwa nyepesi kama watu wanavyofikiria. Nimekaa WCB kwa muda mrefu mpaka kufikia kutambulika naweza kusema nimesota sana.

IJUMAA SHOWBIZ:Unaizungumziaje timu ya WCB katika safari yako?

 

ZUCHU: Kiukweli wamekuwa ni watu ambao walinitia moyo na kunifariji, maana nilifikia hatua ya kutamani kuacha muziki nikafanye kazi nyingine, lakini nashukuru Mungu kaka yangu, Mbosso na Queen Darleen walinipa moyo na kuendelea kunishawishi nibaki.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Baada ya kuingia WCB baadhi ya watu walizungumza ujio wako ni tishio kwa Darleen, je, unalizungumziaje hilo?

 

ZUCHU: Watu wanaweka fiksi tu, dada Darleen hata anikosee vipi siwezi kumvunjia heshima ndivyo hivyo hata kwenye muziki, siwezi kuwa tishio kwake kwa sababu nilimkuta. Naacha waongee sisi tunaendelea kupiga kazi.

IJUMAA SHOWBIZ: Queen Darleen ana mchango gani kwenye muziki wako?

 

ZUCHU: Ananionesha sapoti sana, naweza kusema hana roho mbaya kabisa, amekuwa ni mtu muhimu kwangu.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Kuna tetesi kuwa hujui kuimba unabebwa na lebo yako, huwa unajisikiaje?

 

ZUCHU: (anacheka) katika kila safari ya mafanikio vikwazo havikosekani, hata kujiunga kwenye ebo hii siyo kazi rahisi. Naamini uwezo ninao na kipaji pia ninacho, ndiyo maana nikaaminika na uongozi na kufanya kazi na mimi. Nabebwa na juhudi zangu tu na si kitu kingine.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Ok, vipi kwa wanaosema kwamba unaimba Taarab?

 

ZUCHU: Kwenye Ngoma ya Quarantine niliwathibitishia kila kitu kuwa mimi ni wa tofauti. Siimbi Taarab kama wanavyosema.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Umeandaa shoo kesho pale Mlimani City, je, nini lengo la shoo hiyo?

 

ZUCHU: Lengo kubwa ni kusema asante kwa Watanzania, walivyonipokea kwa ukubwa zaidi. Asilimia 30 ya mapato yatakayopatikana yatakwenda kugusa wasichana wenye uhitaji.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Kwenye shoo hiyo mashabiki watarajie nini?Z

 

UCHU: Itakuwa ni shoo kubwa mashabiki zangu waje kwa wingi maana mbali na shukrani nitatoa burudani.

 

IJUMAA SHOWBIZ:Unaizungumziaje menejimenti yako?

 

ZUCHU: Menejimenti yangu imekuwa na umuhimu kwenye muziki wangu, maana kumsimamia msanii wa kike si kazi ndogo. Bosi Diamond na uongozi wote wamekuwa wakinipambania tangu kutambulishwa kwa mashabiki mpaka sasa, nina mengi mazuri ya kuwazungumzia.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Kuna tetesi kuwa una uhusiano wa kimapenzi na Diamond, unalizungumziaje hili?

 

ZUCHU: Diamond ni kaka yangu, nimekuwa nikimtazama tangu nikiwa shule, hajawahi kunivunjia heshima.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Ulijisikiaje marais kuukubali muziki wako?ZUCHU: Ilikuwa ni ndoto yangu kupiga picha na Rais Msatafu, Dk Jakaya Kikwete, nashukuru Mungu, naye aliliona hilo akaja kupiga picha na mimi. Pia nilifurahi sana Rais Magufuli kunishika mkono kwa sababu ni bahati kubwa na siichukulii kawaida, ni jambo ambalo sikulitegemea.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Wasanii wengi wa kike wamekuwa wakikutana na changamoto ya rushwa ya ngono, kwako imekaaje?

 

ZUCHU: Kama nilivyosema kwenye mkutano wangu na waandishi wa habari nilisema sijawahi kutoa hata ya busu. Nakumbuka kaka yangu Mbosso aliwahi kunipeleka studio kwa Mocco na kumuomba nirekodi wimbo maana sikuwa na hela na alinisaidia bila hata rushwa.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Je, umejiandaaje kulibeba jina lako bila kushuka?

 

ZUCHU: Mwenyezi Mungu amenipa bahati ya kuzaliwa kwenye familia ya mtu mkubwa. Siwezi kulewa sifa maana niko sehemu ambayo ni mfano wa kuniongoza katika maisha ya kisanaa.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Ni msanii gani wa kike ambaye unamtazama sana?

 

ZUCHU: Kwanza kabisa ni mama yangu (Khadija Kopa), nimekuwa nikimtizama kwa muda mrefu sana, pia dada yangu Lady Jaydee natamani kukutana naye ili anielekeze njia sahihi za kufanya kwenye muziki.

Leave A Reply