The House of Favourite Newspapers

Huu ndiyo ukweli wa Kitwanga Kuhusu Ulabu

0

kitwanga8Stori:  Mwandishi Wetu, WIKIENDA

DAR ES SALAAM: Ajali ya kisiasa! Gumzo kuhusu Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ kumtumbua Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Muhangwa Kitwanga (56) kwa madai ya kuingia bungeni akiwa ‘amechangamka’ bado liko vinywani mwa Wabongo huku sasa, upande wa pili wa hali hiyo ukijulikana, Ijumaa Wikienda limechimba.

Ijumaa iliyopita, JPM alitengua uteuzi wake akidaiwa kuingia mjengoni akiwa amelewa hivyo kukosa umakini wakati akijibu maswali ya wizara yake.

Habari zilizonaswa na Wikienda zinasema Kitwanga ni mnywaji lakini si kwa kiwango cha kukosa umakini kiasi cha kushindwa kutiririka vyema kwenye kujibu maswali, ila siku hiyo ilisababishwa na msongo.

MSIKIE HUYU

“Mimi sikatai ndiyo, Kitwanga anapiga ulabu, lakini yule jamaa yuko makini sana. Huenda siku ile alizidisha lakini naijua sababu.

“Unajua siku za hivi karibuni, jamaa amekuwa akiandamwa sana na baadhi ya wabunge kuhusu sakata la Kampuni ya Lugumi na ufungwaji wa vifaa vya kutambua alama za vidole vya wahalifu.

“Alishajieleza sana kuwa, Kampuni ya Lugumi haikuwa na mkabata na Kampuni ya Infossy, lakini wabunge wapi! Kila siku walikuwa wakitaka jamaa ajiuzulu licha ya kwamba sakata la Lugumi liko kwenye kamati ya bunge,” kilisema chanzo hicho.

LEMA AKANUSHA, AWABEBESHA LAWAMA WATU WATATU

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ni miongoni mwa wanasiasa waliokuwa wakimwandama sana waziri Kitwanga wakimtaka ang’atuke nafasi yake hiyo kwa sababu ya kuhusishwa na Lugumi.

Akizungumza na gazeti hili Jumamosi iliyopita siku moja baada ya JPM kumtumbua, Lema alikanusha vikali madai hayo akisema si ya kweli kwa vile yeye na mtumbuliwaji huyo ni marafiki.

“Ni kweli aliingia bungeni akiwa ‘amechangamka’ au amekunywa pombe kama utenguzi ulivyosema na mimi sitarajii mbunge aingie bungeni akiwa amelewa.

“Lakini mimi naamini kabisa wanaotakiwa kubebeshwa mzigo ni wasaidizi wake.

“Ninavyojua waziri ana wasaidizi watatu, kuna katibu mkuu, dereva na mtu mwingine (katibu wa mbunge). Ina maana hawa wote hawakumshauri waziri baada ya kuona hali yake? Walipaswa kujua kila kitu juu ya bosi wao ili wamshauri kwa sababu kulewa kazini tena bungeni ni kinyume na maadili ya utumishi,” alisema Lema.

WALIVYOSEMA WANASIASA

Kwa upande wao, baadhi ya wanasiasa waliozungumza na Wikienda walisema rais amethibitisha kuwa katika serikali yake hataki uzembe kwa watendaji wake hasa wale ambao amewateua mwenyewe.

“Achana na masuala ya kashfa ya mkataba wa Kampuni ya Lugumi. Unajua kuna baadhi ya watu wanadai hiyo ndiyo imemng’oa kwa sababu anahusishwa nayo, lakini ninavyojua, hilo rais hawezi kuliingilia kwani lipo chini ya Kamati ya Bunge na ni mhimili tofauti,” alisema mwanasiasa mmoja aliyeomba hifadhi ya jina na kuongeza:

“Tusitafute visingizio, na uzuri zile video zake akijibu maswali bungeni zipo kwenye mitandao ya kijamii. Zinaonesha kila kitu, kusitokee mtu akadhani kuwa JPM hajui kinachoendelea bungeni. Wewe unadhani ni nani anaweza kuthubutu kufanya hivyo halafu akasalimika kwa Magufuli?”

Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutochorwa majina yao gazetini, walisema;

“Kusema ukweli, Kitwanga ukiachia mbali hiyo pombe iliyotajwa kule bungeni, lakini wauza unga wanamjua na hawatamsahau. Jamaa amekamata wengi tena bila kuogopa wala kupendelea,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

“Mimi siikosoi hatua ya Rais Magufuli maana lazima kuwepo kwa utaratibu wa wakati wa kazi na wakati usio wa kazi, lakini kwa wauza unga kama wameshinda, Kitwanga amewakamata wengi, sasa sijui atakayekuja,” alisema mwingine.

“Jamaa anawakamata sana. hajali wewe unajuana na nani au na nani, ukishukiwa tu ndani. Naamini wauza unga wataisha kwa Kitwanga,” alisema mtumishi huyo.

KITWANGA HAPOKEI SIMU

Juzi alipotafutwa Kitwanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi (CCM) ili kujua amepokeaje utenguzi huo wa rais, simu yake iliita bila kupokelewa.

Leave A Reply