The House of Favourite Newspapers

Jini mweusi 57

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam kufuatia kupotea mfululizo kwa machangudoa katika mazingira ya kutatanisha. Taharuki kubwa inazuka kwani ndani ya kipindi kifupi tu, zaidi ya machangudoa kumi na moja wanapotea na hakuna anayejua walikopotelea.

Jambo hilo linasababisha jeshi la polisi kuingilia kati. Kinachozidi kuzua utata, wote wanapotea katika mazingira yanayofanana. Mwanaume mmoja asiyejulikana, aliyekuwa anatembelea gari la kifahari aina ya Volkswagen, aliyekuwa akienda eneo hilo usiku wa manane ndiye anayehusishwa na wote wanaopotea.

Upande wa pili, kijana aliyekuwa na mwonekano tofauti na binadamu wa kawaida, Dickson Maduhu au Zinja kama wenzake walivyokuwa wakimtania, amejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hisia kali za mapenzi zinasababisha kijana huyo aanze kutoka usiku na kwenda kutafuta machangudoa. Hivyo baadaye anahamishiwa Dar es Salaam.

Baada ya kuwa DCP, Dickson anakutana na msichana aitwaye Pamela, anatokea kuvutiwa naye, anafanya naye mapenzi kwa kumnunua Kinondoni. Kupitia changudoa huyo aliyetoka Arusha, anajikuta akianza kuwaua wanawake wengi jijini Dar es Salaam.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Hawakuchukua muda mrefu wakafika kituoni, alichokifanya polisi ni kumwambia kijana yule aliyejitambulisha kwa jina la Samto ampigie simu Hadija na kumwambia maneno yoyote yale ilimradi wakutane sehemu.

Hiyo ndiyo njia ambayo ilionekana kufaa kutumika kwani vinginevyo wasingeweza kumkamata mwanamke huyo. Wakati Samto amepewa simu kwa ajili ya kumpigia Hadija, Kamanda Dickson akamzuia kwa kumwambia kwamba hakutakiwa kufanya hivyo, kwa kuwa alikwishaipata simu yake, haikuwa na haja.

“Haina haja kufanya hivyo, nilichokuwa nakitaka ni simu tu,” alisema Kamanda Dickson hali iliyomfanya kila polisi kushangaa huku wengine wakimuona kuwa na roho nzuri.

“Hakuna tatizo afande.”

“Ila ningependa kuzungumza na huyu mtu.”

“Sawa mkuu!” alisema polisi mmoja kisha kupiga saluti.

Wakamchukua Samto na kumpeleka katika chumba kimoja kilichokuwa na meza moja ndefu na viti viwili. Walipofika wakamuweka kwenye kiti kimoja na kiti kingine kukaliwa na Kamanda Dickson, polisi wote wakatoka nje.

Kamanda Dickson akabaki akimwangalia Samto huku uso wake ukionekana kuwa na hasira mno. Alivimba kiasi kwamba ubaya wa sura yake kuonekana dhahiri. Samto alimfahamu mtu aliyekuwa mbele yake, alikuwa miongoni mwa watu waliosemekana kuwa na roho mbaya, hivyo kila alivyomwangalia na kwa jinsi alivyokuwa na hasira, akajua kwamba angeweza kufanywa kitu kibaya.

“Huyo Hadija anaishi wapi?” aliuliza Dickson.

“Anaishi Kinondoni A.”

“Kama kunaelekezeka hebu nielekeze,” alisema Dickson hivyo Samto kuanza kumuelekeza.

“Sawa. Alipokuuzia simu hii alikwambiaje?”

“Alisema kwamba ilikuwa yake hivyo nisiwe na hofu na kwa sababu huwa mara nyingi nanunua vitu kwake, nilimwamini sana,” alisema Samto.

“Huwa anapatikana nyumbani muda gani?”

“Mchana huwa yupo muda wote, ila kuanzia saa moja, anatoka kwenda kwenye mishe zake.”

“Na hapo anaishi na watu wangapi?”

“Yupo na wasichana wenzake wawili, Asha na Anita, ila pia ana marafiki zake wa karibu, Mariamu na Ashura ambao wanaishi kama nyumba ya tatu kutoka hapo anapoishi,” alisema Samto.

“Sawa. Wanafanya kazi gani?”

“Wanajiuza usiku.”

“Wote hao?”

“Ndiyo!”

Kamanda Dickson hakutaka kupoteza muda, alichokifanya ni kuondoka kituoni hapo huku akitoa agizo kwamba Samto asitolewe kituoni wala asiwasiliane na mtu yeyote na kama alihitaji chakula, ilibidi kununuliwa lakini si kuruhusu kuonana na mtu yeyote yule.

Ili kuonesha kwamba alimaanisha alichokisema, akaingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi cha shilingi elfu hamsini na kumgawia mkuu wa kituo huku akimtaka mkuu wa kituo ahusike katika ishu zote za chakula kwa Samto.

*********

“Dada samahani!” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja kutoka katika sehemu iliyokuwa na giza hafifu, kichwani alikuwa na kofia kubwa huku akiwa amevaa shati lenye maua.

“Nani? Mimi?” aliuliza msichana huyo, kwa kumwangalia tu, wala usingeweza kujiuliza mara mbili kwamba alikuwa akifanya kazi gani, mavazi yake tu, tena kwa muda kama huo alionekana kuwa changudoa, na kama hakuwa changudoa, basi alikuwa mtu wa kujirusha kwa sana usiku.

“Ndiyo dada! Nakuhitaji mara moja.”

“Mbona gizani?”

“Jamani! Kwani kuna giza hapa? Halafu sisi wengine wenye familia zetu hatutaki kuonekana, si unajua mke akituoni usiku hakulaliki…” alisikika mwanaume huyo.

Msichana yule akajisogeza karibu na mwanaume yule ila kwa mwendo ulioonesha kuwa na hofu na uwepo wa mwanaume yule mahali pale. Alipomfikia, alijitahidi sana kumwangalia usoni ili amuone vizuri lakini kutokana na kigiza kilichokuwa mahali pale, hakuweza kumgundua.

“Nataka mechi…” alisema mwanaume huyo.

“Nani kakwambia kama najiuza?”

“Jamani! Nimebanwa mwenzako, hata kama haujiuzi, naomba tu uniridhishe mtoto wa mwanamke mwenzio, nitakupa hela yoyote uitakayo,” alisema mwanaume huyo.

“Una kilo?”

“Hiyo tu? Hakuna tatizo,” alisema mwanaume huyo, hapohapo akaingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi cha shilingi laki moja na kumgawia msichana huyo. Alionekana kuwa na kiu ya kutaka kulala naye kwa kisingizo cha kutoka mkoani na gari la mizigo, hivyo njiani kote alikosa mwanamke wa kumkosha roho yake. Mwanaume huyo alikuwa Kamanda Dickson na mwanamke alikuwa Shamila, rafiki yake Hadija.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply