The House of Favourite Newspapers

Sababu ya upungufu wa damu mwilini

uchovu 3Leo tuangalie tatizo la upungufu wa damu mwilini. Anaemia ni jina la jumla linalotumiwa kubainisha aina mbalimbali za upungufu wa damu mwilini.

Kiwango cha kawaida cha chembe nyekundu za damu (Hb) katika mwili wa binadamu ni kati ya gramu 12 mpaka 14 kwa kila mililita ya damu na zikiwa pungufu ya hapo mtu huyo anakuwa na tatizo la upungufu wa damu.

Upungufu wa damu mwilini hutokea iwapo mkusanyiko wa pamoja wa chembe nyekundu za damu (haemoglobin) zinapopungua kupita kiwango cha kawaida kinachotakiwa kwenye mwili wa binadamu.

Tatizo hili linaweza kumpata mtu yeyote ingawa visababishi vinaweza kutofautiana.
Licha ya utofauti huo mara nyingi tatizo hili husababishwa na mambo makuu matatu ambayo ni kupoteza damu mfano wakati wa hedhi kwa wanawake hasa wanaotokwa na damu nyingi au kuvuja damu kunakosababishwa na vidonda vya tumbo.

Sababu nyingine ni uzalishwaji duni wa chembe nyekundu za damu unaosababishwa na upungufu wa vitamini au lishe duni pamoja na magonjwa sugu. Pia magonjwa ya kurithi (Hereditary).

Iwapo mtu atapungukiwa kiasi cha madini, ulaji wa madini ya chuma katika mlo wa kawaida wa mtu hauwezi kufidia kiwango cha madini kilichopotea na kiasi hicho kinachokuwa kimebaki hutumika mara moja.

Aina za upungufu wa damu mwilini
Zipo aina mbalimbali za upungufu wa damu ikiwemo Haemolytic Anaemia. Hali hii ya upungufu wa damu, chembe nyekundu za damu huharibiwa haraka kuliko mwili unavyoweza kuzalisha chembe nyingine.

Upungufu huu husababishwa na mambo mengi ikiwemo kansa aina ya lymphoma au utumiaji wa baadhi ya dawa ambazo huweza kuangamiza chembe nyekundu za damu kwa mfano dawa aina ya Methylodopa.

Mtu mwenye aina hii ya upungufu wa damu anaweza kupatwa na homa, kutetemeka kwa mwili, maumivu ya tumbo na mgongo na mapigo ya moyo kushuka ghafla.
Pernicious anaemia Huu ni upungufu wa damu unaotokana na ukosefu wa kutosha wa asidi aina ya Folic (Folate) katika chakula.

Asidi aina ya Folate hupatikana katika mbogamboga za rangi ya kijani, matunda na nyama.

Aplastica Anaemia
Huu ni upungufu wa damu unaotokea wakati chembe nyekundu za damu zinaposhindwa kuzalishwa ipasavyo.

Sickle cell Anaemia
Ni aina nyingine ya upungufu wa damu ambao chembe nyekundu za damu huwa na muundo usio wa kawaida unaozuia na kuathiri mishipa midogo ya damu na hivyo kusababisha kuziba kwa mishipa hiyo ya damu.

Dalili za upungufu wa damu mwilini (Anaemia) ni kuwa mtu mara nyingi huwa amepauka mwili na hujisikia kuchoka, udhaifu na huwa na mwendo kasi wa damu (yaani high pulse rate). Mgonjwa kuhisi kiu, kizunguzungu wakati akisimama, kuhema mfululizo na kuwa na mahangaiko ya moyo wakati akitumia nguvu kufanya jambo lolote.

Dalili nyingine ni mapigo ya moyo kwenda kwa kasi, kuhisi uchovu sana au hata kuishiwa kabisa na nguvu, maumivu ya kifua, kupoteza nguvu na macho kukosa nuru ya kuona vizuri.

Comments are closed.