The House of Favourite Newspapers

Unending Love – 57

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna, pia anakataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, wataoana na Anna.
Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.
Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William ambaye baadaye anakuja kumharibia maisha kwa kumpachika ujauzito.
Anna anarejea nyumbani kwao, Mwanza bila William kujua chochote lakini akiwa anaelekea uwanja wa ndege, anakutana na Jafet katika mazingira ambayo hakuyategemea. Hata hivyo, wanashindwa kuelewana.
Anna anapofika Mwanza, wazazi wake wanaonesha kuchanganyikiwa mno na taarifa kwamba alikuwa mjamzito. Harakaharaka anapelekwa hospitali huku wazazi wake wakiendelea kutupiana lawama.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Daktari huyo aliendelea kumsisitiza baba yake Anna juu ya umuhimu wa kumsimamia mwanaye kwa karibu ili kuhakikisha hajihusishi kwenye vitendo vinavyoweza kuiweka afya yake hatarini, ikiwemo kujihusisha na mapenzi, kunywa pombe na kutozingatia dozi.
“Nimekuelewa daktari, kwa hiyo si tunaanza na hili suala la kumtoa ujauzito kwanza?”
“Yaah! Hilo ndiyo litakuwa la kwanza na kama nilivyokwambia inabidi kwanza tufuatilie vibali kwa sababu kutoa mimba kisheria ni kosa la jinai isipokuwa kwa sababu za kitabibu ambazo nazo ni lazima zihakikiwe na bodi ya madaktari na kutolewa kibali,” alisema Dokta Kashinje na kumtaka baba yake Anna kutoka na kwenda kumsubiri nje, akaenda kuungana na familia yake.
“Unaona upumbavu ulioufanya unavyotugharimu?” baba yake Anna alimuuliza binti yake huyo ambaye muda wote alikuwa amejiinamia, machozi yakimtoka kwa wingi.
“Naongea na wewe!”
“Nisamehe baba, nimeyajua makosa yangu,” alisema Anna huku akiendelea kulia.
“Tumezungumza kwa kina na daktari na ametueleza kwamba litakuwa ni jambo la hatari sana kwako kujifungua kwa sasa kutokana na hali uliyonayo kwa hiyo ameshauri huo ujauzito utolewe,” alisema baba yake Anna, kauli ambayo ilimshtua mno msichana huyo.
Tangu aanze kupata akili zake, hakuwahi kudhani hata siku moja kwamba itatokea siku na yeye akaingia katika orodha ya wanawake makatili wanaotoa mimba. Japokuwa hakuwa tayari kwa suala hilo, baba yake alipomueleza madhara aliyoelezwa na daktari kwamba yanaweza kumpata, Anna alijikuta akikosa cha kujibu zaidi ya kukubaliana na kila kitu ingawa aliumia sana ndani ya moyo wake.
Ukimya ukatawala kati yao, hakuna aliyemzungumzisha mwenzake, kila mmoja alikuwa akiwaza lake kichwani. Dokta Kashinje ndiye aliyekuja kuvunja ukimya uliokuwa umetanda kati yao, akaomba kuzungumza na baba yake Anna.
Alimueleza kwamba suala la vibali limekuwa gumu kidogo hivyo waende nyumbani na kurudi baada ya siku tatu, mzee huyo akakubali na kuondoka na familia yake. Ukimya uliendelea kutawala kati yao, hakuna aliyemsemesha mwenzake mpaka wanawasili nyumbani kwao.
Kama kawaida yake, Anna akapitiliza na kwenda kujifungia chumbani kwake, akawa anaendelea kulia huku akiijutia sana nafsi yake kwa kilichotokea. Kingine kilichomfanya ajisikie vibaya sana, ni kuona William hamjali kwa chochote tena baada ya kupata alichokuwa anakitaka.
Kabla hajampa mwili wake, ilikuwa haiwezi kupita muda bila wawili hao kukutana au kuwasiliana kwa simu lakini mambo yalikuwa tofauti kabisa. Tangu alipoondoka Dar es Salaam bila hata kumuaga, William hakuwahi kumpigia simu Anna kumuuliza alipo wala kujua maendeleo yake, jambo ambalo lilimfanya aamini kwamba kumbe William hakuwa na mapenzi ya kweli kwake bali alikuwa akihitaji kufanya naye mapenzi tu.
“Huna haja ya kuendelea kulia mwanangu, kila jambo huwa linatokea kwa sababu maalum, huwezi kujua Mungu amekupangia nini katika hili.”
“Mama najisikia vibaya sana, naumia sana ndani ya moyo wangu.”
“Kipi kikubwa kinachokufanya uumie kiasi hicho?”
“Nimetupa kipande cha almasi na kuokota kipande cha chupa.”
“Sasa ukilia ndiyo utabadilisha ukweli?”
“Lakini mama wewe ndiyo chanzo cha yote,” alisema Anna na kuangua tena kilio kwa nguvu.
Kauli hiyo ilimuumiza sana mama yake Anna kwani hata mumewe alikuwa akimtuhumu hivyohivyo, akakosa cha kujibu zaidi ya kutoka na kumuacha mwanaye akiendelea kuomboleza, akiwa amejifungia ndani ya chumba chake.
Akiwa anaendelea kulia, alikumbuka kwamba kabla hajasafiri kuelekea nchini Marekani, alikuwa ameiandika namba ya simu ya Jafet kwenye moja ya ‘diary’ zake, harakaharaka akainuka pale kitandani alipokuwa amelala na kufungua kabati lililokuwa na vitu vyake kadhaa. Akaanza kupekua huku na kule kutafuta ‘diary’ iliyokuwa na namba hiyo.
Alitamani asikie neno lolote kutoka kwa Jafet akiamini atafarijika ndani ya moyo wake. Kama angekuwa na uwezo wa kurudisha siku nyuma, Anna alitamani arudishe siku nyuma na kurekebisha makosa yote yaliyotokea lakini hilo halikuwezekana. Aliendelea kutafuta ‘diary’ hiyo mpaka alipoipata lakini alipojaribu kupiga namba hiyo, ilikuwa haipatikani hewani.
Kila alipokuwa akikumbuka taswira ya jinsi Jafet alivyokuwa anang’ang’aniwa na yule msichana chotara, huku akionesha kumpenda kuliko kitu kingine chochote, Anna alikuwa akijisikia vibaya mno ndani ya nafsi yake. Aliendelea kujaribu kuipiga lakini bado majibu yalikuwa yaleyale, mwisho akachoka.
Siku hiyo ilipita, muda ukawa unazidi kuyoyoma na hatimaye siku ya tatu iliwadia ambayo Anna na wazazi wake walitakiwa kurudi hospitalini kwa ajili ya kufuatilia taratibu za kumtoa ujauzito msichana huyo.
Baba yake Anna, mkewe pamoja na Anna mwenyewe walijiandaa na baada ya kila mmoja kuwa tayari, waliondoka kwa kutumia gari lao mpaka Hospitali ya Bugando walikopokelewa na Dokta Kashinje, akaongozana na baba yake Anna mpaka ofisini kwake ambako kulikuwa na fomu maalum ambazo alitakiwa kuzijaza kabla mwanaye hajaingizwa kwenye chumba maalum kwa ajili ya kutolewa ujauzito huo.
Kwa kuwa alichokuwa anapigania ni usalama wa mwanaye, baba yake Anna alisaini fomu hizo zote kisha baada ya hapo mipango ya Anna kutolewa ujauzito ikaanza kufanywa. Ilibidi afanyiwe vipimo vya kina na baada ya madaktari kujiridhisha kwa kila kitu, aliingizwa kwenye chumba hicho na kazi hiyo ikaanza chini ya usimamizi wa madaktari wanne, akiwemo Dokta Kashinje.
***
Japokuwa Jafet alijitahidi kusimamia msimamo wake wa kutomfikiria kabisa Anna, kila alipokuwa anakumbuka jinsi alivyokutana na msichana huyo barabarani, akiwa kwenye hali iliyoonesha dhahiri kwamba ana matatizo makubwa, alijikuta akijisikia vibaya sana ndani ya moyo wake.
Ni kweli hakuwa na mpango wa kuendelea kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Anna kutokana na maumivu makali aliyomsababishia lakini hakutaka kumuona akiwa kwenye matatizo. Alijaribu kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu Anna.
Hakuelewa alifuata nini Dar es Salaam, kwa sababu katika kipindi chote walichoishi kama wapenzi, hakuwahi kumwambia kwamba ana ndugu Dar hata siku moja. Pia alijiuliza kwa nini Anna alikuwa ‘rafu’ kiasi hicho kwa sababu haikuwa kawaida yake. Alizoea kumuona msichana huyo muda wote akiwa msafi lakini siku walipokutana alikuwa tofauti kabisa.
“Jafet, nimekuja kukuchukua twende tukale chakula naona nimekusubiri kantini mpaka nimechoka,” sauti ya Suleikha, msichana aliyekuwa naye wakati alipokutana na Anna siku kadhaa zilizopita, ndiyo iliyomzindua kutoka kwenye lindi la mawazo.
Japokuwa mwenyewe hakuwa ameamua kuanzisha rasmi uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo, Suleikha alionesha kumpenda mno Jafet. Hakujali uzuri wa kipekee aliokuwa amejaliwa, japokuwa wanaume wengi chuoni hapo walikuwa wakimtongoza, mwenyewe aliamua kuwa karibu na Jafet akiamini lazima ipo siku atakubali kuanzia naye uhusiano wa kimapenzi.
Kila Jafet alipokuwepo, lazima Suleikha alikuwa pembeni yake, ndani ya kipindi kifupi tu tangu walipokutana, tayari watu wengi walikuwa na uhakika kwamba wawili hao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Comments are closed.