The House of Favourite Newspapers

BANANA: UMAARUFU UNAISHIA KWANGU, FAMILIA YANGU NO!

0
Banana Zoro.

Akiwa ameanza kufahamika kwa mashabiki enzi hizo akiwa na Kundi la B Love M, lililomshirikisha pia Alex Masinga, Banana alipata jina kubwa baada ya kufanya kazi peke yake, solo artist, akitoa kazi nyingi zilizopendwa na mashabiki.

 

Kwa sasa, Banana, baba wa watoto wawili, anamiliki bendi yake mwenyewe, iitwayo B Band, ambayo hupiga katika mahoteli na kwenye shughuli mbalimbali za kijamii. Risasi Vibes, lilikutana naye ndani ya Ukumbi wa Paparazzi, Slipway jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa na bendi yake na kufanya naye mahojiano maalum.

 

Another Beautiful Day  “Nimepitia changamoto nyingi sana katika muziki hadi hivi sasa, kiasi kwamba nikisimama hivi katika muziki najiona ni mpambanaji wa kweli niliyefanikiwa. “Miongoni mwa chang amoto hizo ni pamoja na kuweza kukaa muda mrefu katika ndoa (alimuoa Suzi Walele mwaka 2007). Maana katika kazi yetu ya muziki na ustaa huu, hii ni changamoto kubwa sana.

 

 

“Na hii ni kwa sababu nilikataa kuunganisha maisha ya familia na muziki, nikiwa nyumbani ni baba na nikiwa katika muziki nipo kazini. Lakini pia nimekuwa makini kujilinda na kujiheshimu, ndiyo maana unaona niko kama nilivyo.

 

“Katika ndoa yangu nimebahatika kupata watoto wawili, Randy na Jermaine na kitu ambacho
kimesaidia ndoa yangu kudumu ni upendo na kuiheshimu familia.

 

“Ninafanya muziki siyo kwa sababu ninapata fedha, bali kwa vile mimi nimezaliwa katika muziki, nimemkuta baba yangu akiwa mwanamuziki na moja kwa moja nikaanza kujihusisha nao na ninaupenda kwa asilimia mia moja.

 

“Sijawahi kufanya kazi nyingine mbali na muziki. Ninafahamu kuwa mimi ni mtu maarufu, lakini umaarufu wangu unaishia kwangu, sitaki kabisa familia yangu ijiingize katika umaarufu kwa vile ninajua madhara yake.

 

“Pamoja na umaarufu wangu ndani na nje ya nchi, ninaizuia familia yangu ikae mbali kabisa na ustaa, sitaki hata kuweka picha zao katika mitandao ya kijamii. “Najaribu kujenga nidhamu kubwa ya kazi, natofautisha sana maisha yangu binafsi na kazi, yaani nikiwa  kazini hata wanamuziki wangu wananijua, naweka pembeni urafiki, nataka tupige kazi.

 

“Nashukuru muziki wetu wa Bongo Fleva kwa sasa upo juu, unasikika hadi nje ya mipaka yetu, vijana wanafanya vizuri na sasa unasikika Afrika nzima na duniani kwa jumla. Kuhusu mikakati yake kimuziki, Banana ambaye kibao chake kiitwacho Mama kilipata kuwa ‘wimbo wa taifa’ alisema kwa sasa anaimarisha bendi yake ili kujiongezea mashabiki wengi zaidi kutokana na staili ya muziki wao. Wito wake kwa wasanii wenzake ni kuzidisha ushindani baina ya wanamuziki kwani kama kila mmoja atatoa kibao kikali, hiyo itakuwa chachu ya kuukuza muziki wao.

 

MAKALA: ISSA MNALLY| RISASI JUMAMOSI

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App

Leave A Reply