ILIPOISHIA RISASI JUMATANO:
Aliingia ndani kwake, akamkuta mumewe sebuleni…
“Umechelewa sana mama Monica.”
“Ni kweli mume wangu, kulikuwa na wateja sana leo,” alisema mama Monica huku akiweka ule mkoba juu ya meza huku akivua sendozi. Kumbe alikuwa hajafunga zipu, zile shilingi laki sita zote zikatoka na kusambaa sakafuni.
SHUKA NAYO…
“
Ah! Mama Salama ataniponza mimi mwaka huu. Yaani hizi pesa zake zinaanguka si mtu anaweza kujua ni pesa zangu?” alisema kwa sauti mama Monica huku akionekana kuwa na wasiwawasi.
Mumewe alizitumbulia macho zile pesa, akamuuliza…
“Unataka kuniambia hizo pesa ni za mama Salama siyo?”
“Ndiyo mume wangu.”
“Ziko shilingi ngapi?”
“Zipo shilingi laki sita kamili. Zihesabu kama unabisha au huniamini,” alisema mama Monica.
“Namba ya mama Salama si unayo?” aliuliza baba Monica.
“Ndiyo ninayo,” alisema mama Monica huku moyoni akijua kama angedanganya na kama mumewe anataka mwanamke huyo aje, angeweza kwenda hata mwenyewe tu.
“Mpigie sasa hivi aje hapa. Sitaki uongouongo mimi,” baba Monica alikuja juu akionekana hana utani au amehisi kitu.
Mama Monica alimpigia simu mama Salama akiwa palepale sebuleni…
“Haloo…uko nyumbani…uje basi uchukue zile pesa zako laki sita ulizoniachia,” alisema mama Monica na kukata simu.
Mama Salama alijiuliza maswali mengi kuhusu wito wa mama Monica…
“Hivi huyu mama Monica siku hizi ana nini? Siku ile kasema ana vitu vyangu. Kwenda nikakuta vile. Leo ana laki sita zangu, kuna nini kwani kwake?” alijiuliza mwanamke huyo.
***
Kule nyumbani, mama Monica moyo ulimuuma sana…
“Yaani niiache hii laki sita iende hivihivi kweli? Hapana, safari hii sikubaliani hata kidogo. Akija kuichukua, baadaye namfuata nyumbani kwake kumwambia ukweli,” alisema moyoni mama Monica.
Ndani ya dakika tano tu, mama Salama aliwasili kwa sauti iliyojaa bashasha na uchangamfu wa hali ya juu. Alikuwa kama anayejifanya hakuna geni katika yote aliyoambiwa.
Alisalimiana na baba na mama Monica kisha akasimama bila kukaa huku akisema…
“Sasa mimi sikai sana jamani.”
“Zile pesa zako ulizoniachia hizi hapa. Ziko vilevile,” alisema mama Monica kwa sauti iliyokosa ujasiri…
“Laki sita?”
“Ee laki sita. Au zilikuwa zaidi ya hapo mama Salama?”
“Hata laki sita.”
Mama Salama alizipokea, akazificha kwenye kanga alizojifunika na kuaga. Lakini akiwa anaondoka, baba Monica akamwambia…
“Mimi nitakuja nyumbani kwako, mwambie baba Salama, nina mazungumzo kidogo.”
“Sawa baba Monica. Karibu sana, nitamwambia.”
Tamko la mumewe lilimfanya mama Monica aishiwe nguvu kabisa. Hakujua mume wake atakwenda kule saa ngapi lakini pia hakujua anataka kwenda kuongea nini!
“Haitawezekana tena kwenda. Huenda baba Monica akifika kule anataka kwenda kumpeleleza kama kweli pesa ni zake…lakini laki sita zangu ziende hivihivi kweli jamani? Yaani mechi nicheze mimi ushindi apewe mama Salama!” alijiuliza mama Monica akisikia uchungu mkubwa moyoni.
***
Usiku wa siku hiyo haukuwa mzuri kwa mama Monica kwa mambo makuu mawili. Kwanza kabisa, baba Monica hakuonesha uchangamfu tangu kuonekana kwa zile laki sita.
Pili kuona kiasi kile cha pesa kinapotea hivihivi anakiona halafu mbaya zaidi ni mara ya pili vitu vyake kwenda kwa mama Salama.
Kwa upande wake, baba Monica yeye alikuwa akiwaza ya kwake. Siku ya tukio la kwanza aliamini kuwa kweli vile vitu na pesa vilikuwa vya mama Salama, lakini safari hii aliona si kweli kwani maisha ya mama Salama na mumewe anayajua vizuri, si watu wa laki sita…
“Mama Salama ninayemjua mimi. Ashike laki sita. Si kweli! Baba Salama anaombaga hata elfu mbili za kununua unga na mimi ndiyo huwa nampa…hizi laki sita zimetoka wapi na ni za nini?” alijiuliza baba Monica. Akaamua kumuita mkewe ili ampe ufafanuzi…
“Mama Monica…mama Monica…”
“Abee,” mama Monica aliitika kutokea usingizini…
“Nina swali, naomba unijibu kwa usahihi na ufasaha wa hali ya juu. La sivyo hali itakuwa si hii…”
“Swali gani mume wangu?”
“Zile laki sita ulisema ni za mama Salama siyo?”
“Ndiyo baba Monica.”
“Umezitoa wapi wewe na kwa nini zimepita mikononi mwako badala ya kwenda kwake mwenyewe mama Salama?”
“Mimi kuna mtu alikuja kwangu gengeni akasema nimpe mama Salama.”
“Huyo mtu ni tofauti na yule aliyeleta vile vitu siku ile?” aliuliza baba Monica kwa sauti ya kukatakata na kukwaruzakwaruza, kuashiria kwamba hayuko sawasawa.
“Ni tofauti kabisa baba Monica.”
“Sasa sikia, mimi kesho asubuhi nitadamkia nyumbani kwa baba Salama. Nitampa maelezo yote ya vitu na fedha za mke wake kupitia wewe, ili nione kama anajua haya mambo au mke wake ana siri moyoni…”
“Mh! Baba Monica, ndiyo nini sasa?” aliuliza mama Monia huku akikaa kwenye kitanda.
Je, unajua nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Risasi, Jumatano ijayo.