Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Dorcas alipoombwa msamaha na kaka yake Evance aliyegundua hakufurahishwa na zawadi ya nguo za ndani alizomnunulia ndipo msichana huyo akamsamehe na kuahidi kuzitumia.
Je, kilifuatia nini?
Endelea mbele…
“Hapo dada yangu umenifurahisha sana, hivyo ndivyo unavyotakiwa kuwa, nashukuru kwa kuzikubali zawadi nilizokuletea,” Dorcas anasema kaka yake alimwambia.
Baada ya kumaliza tofauti zetu kuhusu zawadi, niliendelea na majukumu yangu huku kaka akiwa anaangalia TV na wakati mwingine kunifuata jikoni na kunisemesha hadi mama na wengine walioondoka waliporejea.
Kama kawaida yetu usiku baada ya kupata chakula na kupiga stori za hapa na pale kila mmoja alikwenda kulala, hata hivyo nikiwa nimejilaza kitandani nautafuta usingizi, nikawa najiuliza maswali mengi kuhusu dalili za mapenzi alizoanza kunionesha kaka Evance.
Hata hivyo, kwa kujiamini nilijua hata angefanyaje asingeweza kunirubuni kwa vile nilikuwa najitambua na isitoshe pale nyumbani muda mwingi palikuwa na watu.
Licha ya Emmy aliyekuwa akisoma Tabora kunipita kidogo umri, sikuwa napenda kumshirikisha sana mambo yangu ya ndani ndiyo maana hata zile zawadi alizoniletea kaka sikumwambia.
Sikufanya hivyo kuhofia angehisi huenda nilikuwa nina uhusiano naye wa kimapenzi hivyo kumwambia mama na kuleta balaa jambo ambalo sikutaka litokee.
Kutokana na hofu niliyokuwanayo, niliamua kutozivaa zile nguo za ndani kwa sababu angeniuliza nilipata wapi fedha za kununua nguo zile za kisasa au angemuuliza mama iweje aninunulie mimi na kumuacha yeye.
Nilipanga kuzivaa nguo hizo nitakapoenda Mbeya kwani mama mkubwa angejua nilinunuliwa na rafiki yake, baada ya kupita kama siku mbili hivi nikiwa jikoni napika kaka Evance huku akichekacheka alinifuata na kuniuliza kama chupi alizoniletea zilinitosha na kunipendeza.
Kufuatia swali hilo, nilishindwa kumjibu nikabaki kumwangalia ndipo aliniita, nilipoitika aliniuliza mbona sikumjibu swali lake badala yake nilibaki nikimwangalia tu!
Ingawa nilizijaribisha zile nguo na kunitosha, kuepusha usumbufu wake nilimshukuru na kumwambia hazikuwa na tatizo na kuhusu kunipendeza au kutonipendeza ilikuwa siri yangu, akacheka sana na kusema;
“Wewe Dorcas una majibu ya mkato sana!”
Alipotoa kauli hiyo, Emmy ambaye alikuwa chumbani aliingia jikoni ndipo tulibadili mada na kuzungumza mambo mengine, Emmy aliniuliza kama nilinunua matunda ya kutengeneza juisi nikamwambia sikununua.
Baada ya kumjibu hivyo aliniomba nimpatie fedha za kununulia matunda, nilipompa alielekea sokoni na kuniacha nikiwa na kaka ambaye aliniuliza kwa nini nilikuwa na majibu ya mkato!
Nilimjibu kwamba nilimjibu kawaida tu akasema sikumjibu sawa aliniponiuliza kama zile nguo zilinipendeza au la, kwa kuwa niliona ananisumbua nilimwambia zilinipendeza.
“Hapo umenijibu vizuri, sasa ungenijibu hivyo tangu awali unafikiri ningekusumbua?” Dorcas anasema kaka yake alimwambia.
Alipotoa kauli hiyo nilimwambia yalikuwa yameisha ila nilimkanya asirudie tena kuniletea zawadi kama zile kwa sababu nilikuwa namheshimu kama kaka yangu.
Cha ajabu licha ya kuonesha kwamba sikupendezwa na alichonifanyia alicheka tu, nikamuacha na kwenda chumbani kwangu.
Maisha yaliendelea nakumbuka Jumapili iliyofuata pale nyumbani waliondoka wote kwenda Kijiji cha Ndembezi kuwasalimia ndugu wengine, kaka naye alipotoka kanisani hakurudi nyumbani.
Kufuatia pale nyumbani kutulia, baada ya kula nilichukua madaftari yangu na kuanza kujisomea lakini sikumaliza hata dakika thelathini kaka alirejea.
Aliponikuta najisomea alinisifia sana na kuniambia kwamba tena ilikuwa afadhali alirudi mapema hivyo angenifundisha kutumia laptop yake.
Baada ya kuniambia hivyo aliniuliza kama nilikuwa nimekula nikamwambia tayari nilikula muda mrefu ndipo akaingia chumbani kwake akabadili nguo na kuvaa bukta na fulana.
Alipobadili akaja sebuleni akanywa maji kisha akasema twende akanifundishe namna ya kutumia laptop yake, awali niligoma lakini akanibembeleza sana kwamba alichotaka kunifundisha kilikuwa muhimu.
Alipoona nasita alibeba madaftari yangu na kwenda nayo chumbani kwake kisha akanifuata, sijui ilikuwaje nikaamua kwenda bila kujua alikuwa na nia gani.
Tulipofika chumbani kwake, ambapo tayari alikuwa kishawasha kompyuta yake mpakato na kuiweka juu ya meza ndogo iliyokuwa mbele ya kitanda, wote tulikaa kitandani kwa sababu hakukuwa na kiti wala stuli.
Baada ya kukaa, akaiwasha laptop na kunifundisha kidogo, nikamuona akiwa na wasiwasi ndipo aliniuliza kama siku ile nilikuwa nimevaa moja ya nguo za ndani alizoninunulia.
Nilipomwuliza kwa nini aliniuliza vile, akacheka na kuniambia alitaka aone jinsi ilivyonipendeza, nikamwuliza kwa hasira alitaka kufanya nini?
Huku akiwa anacheka akaniambia alitaka kuona kama ilikuwa inanipendeza, nikamwuliza mbona alinivunjia heshima wakati nilikuwa namheshimu?
Nilipomwambia hivyo alisema hata yeye aliniheshimu na ili kumuonesha nilikuwa namheshimu nimuoneshe nguo hiyo, nikakataa nikashangaa kanishika na kuniambia kama nilikuwa sitaki kufanya hivyo angeniangalia kwa nguvu.
Baada ya kunishika tukaanza kuvutana huku nikijitahidi kujitoa mwilini mwake lakini alinizidi nguvu akanilaza kitandani, kwa kuwa nyumba yetu ilijitenga hata nilipojaribu kupiga mayowe ya kuomba msaada hakuna aliyesikia.
Hata hivyo, kuhakikisha anatimiza lengo lake akiwa amenibana akaniziba mdomoni kwa kutumia taulo kisha alifanikiwa kuipandisha juu sketi niliyovaa na kuichana nguo yangu ya ndani.
Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, nicheki kupitia namba hiyo hapo juu.