ILIPOISHIA:
Siku ya pili niliwafuata kina Doi ili niwapeleke kwa Papaa, niliamini kupitia mimi ile ndoto ya kuacha kupigwa na baridi na kuumwa na mbu itatimia. Siku hiyo niliwafuata mwenyewe na gari la kifahari aina ya BMW.
SASA ENDELEA…
Kwa kweli muonekano nilioonekana ungeambiwa mimi ni muuza utamu wa mwili ‘changudoa’ usingekubali hata kwa mtutu wa bunduki.
Nilivaa nguo za heshima, vitenge kutoka chini mpaka juu kifuani nilikuwa na hereni, cheni zaidi ya sita zenye uzito tofauti. Utajiuliza vito hivyo vilikuwa wapi, huwezi kuamini katika nyumba ya Papaa kulikuwa na chumba kilichokuwa na nguo na mapambo ya kike aliyoyaweka kwa ajili ya mwanamke atakayeishi naye.
Kwa kauli yake bahati hiyo iliniangukia miye na kujiona mwanamke mwenye bahati, japokuwa sikujua nini hatima ya maisha yangu kutokana na mipango ya hatari aliyokuwa akiicheza. Kwa upande mwingine haikunitisha sana kwa vile maisha ya usanii na utapeli nilikuwa nimeyazoea.
Wasiwasi wangu usanii nilikuwa naufanyia ugenini tofauti na nyuma nilikuwa naufanyia nyumbani lakini niliamini lolote linaloweza kunitokea ingekuwa ajali kazini.
Baada ya kuaminiwa na Papaa alinionesha kile chumba na kunikabidhi rasmi kuwa changu na kutumia kitu chochote nikitakacho. Muonekano wangu ulibadilika hata rafiki zangu walinishangaa kwa jinsi nilivyokuwa nikimeremeta. Hata niliposimama mbele ya kioo nilijikubali, si vibaya kujisifia we mwenyewe uzuri wako kama sifa ni zako kweli.
Niliposimamisha gari mbele ya nyumba yetu na kuteremka, Bahati aliyekuwa nje akiosha vyombo aliyeliangalia gari likiingia na mimi kuteremka, pamoja na kulikodolea macho na mtu aliyeshuka alionesha kunishangaa kuonesha hakunielewa.
Kwa akili yake hakuamini kama naweza kuteremka kwenye gari la kifahari kama lile. Hata nilivyokuwa nimevaa nilikuwa na tofauti kubwa na nilivyoondoka jana yake. Hata nilipomwita alinishangaa kabla hajaniuliza:
“Ha! Ni wewe Konso?” aliniuliza huku akinisogelea nilipokuwa nimesimama pembeni ya mlango wa gari uliokuwa wazi.
“Ndiyo mimi.”
“Muongo!”
“Kwa nini Bahati?”
“Hapana siamini, nilijua mke wa waziri na kujiuliza mke wa waziri amefuata nini uswahilini!”
“Ni mimi ndugu yangu kwani kipi cha ajabu?”
“Konso unajijua kuwa wewe ni mzuri?” aliniuliza kama siku ile ndiyo siku ya kwanza kuniona.
“Kwa nini?”
“Konso kila siku unazidi kuwa mzuri, kazi ya kuuza mwili haikufai kabisa.”
“Ndiyo kazi yetu inayotupa riziki.”
“Ha…ha…pana, hii si kazi tunaifanyia dhiki.”
“Mbona nipo kawaida.”
“Shoga hakika umependeza.”
“Asante.”
“Jamani kila mwanadamu ana nyota yake, huna hata mwezi lakini umegeuka lulu?”
“Kila mbegu na udogo wake, huku mbegu yangu imekubaliana na udongo kupanda kidogo mavuno kibao.”
“Konso, wewe si mwenzetu sasa, hilo gari labda ndotoni ndiyo nitaliendesha.”
“Walaa, muda si mrefu utaendesha.”
“Kwa sura na shepu gani ya kupendwa na bwana mwenye pesa zake?”
“Walaa kila kitu kina wakati wake.”
“Wapiii! Wengine tuna mwaka wa kumi tumeishia kupata kijumba cha kujisitiri, lakini mwenzetu mwezi tu unatembelea gari la thamani.”
“Hili siyo gari langu, kuna kazi nataka kupewa nikiifanya vizuri kutumia gari kama hili haitakuwa shida kila mmoja atamiliki lake hata kama si la gharama kama hili.”
“Sipeee, Doiii,” aliwaita kina Doi waliokuwa ndani kwa sauti ya juu ambao walitoka ndani mbio kama kuna tukio la kutisha.
Ajabu nao hawakunijua macho yao yalikuwa kwa Bahati kutaka kujua amepatwa na nini. Lakini hakuwa na jibu zaidi ya kunitolea macho kama mjusi kabanwa na mlango na kuwafanya wenzake wahamishie macho kwangu na kuniangalia mimi niliyekuwa bado nimesimama nje ya gari nimeishikilia mlango uliokuwa wazi.
Baada ya kuniangalia bado hawakunielewa, walirudisha macho kwa Bahati na kumuuliza:
“Bahati kuna nini?”
“Konso.”
“Kons…Haaa!”
Jamani! Shoga zangu walishtuka baada ya kunitambua na kuja kunivamia kidogo tuanguke chini.
“Jamani ni wewe Konso,” walikuwa hawaamini kuniona katika hali ile kama mke wa waziri au mfanyabiashara mkubwa.
“Ndiyo mimi ndugu zangu.”
“Umekuja na hii gari?”
“Ndiyo.”
“Ukiendesha mwenyewe?”
“Ndiyo.”
“Mmh! Umetisha sasa hivi si mwenzetu.”
“Jamani maneno gani hayo kama ningekuwa si mwenzenu ningekuja, kipi kinawafanya mseme hivyo?”
“Mwenzetu una tofauti kubwa na sisi, sasa hivi unakula kwa upole huliwi na mbu wala kupigwa baridi la usiku. Sasa hivi mapenzi kwako si biashara bali starehe.”
“Jamani mbona mmekuwa na maneno mazito hivyo au hamkupenda niwe hivi? Basi ili kuonesha sipo kwa ajili ya utumwa wa pesa, nitarudisha kila kitu cha Papaa ili tuendelee na kazi yetu,” nilisema vile kuwapima lakini hata siku moja hakuna anayeingia peponi akarudi duniani kwenye shida zisizoisha kila kukicha afadhali ya jana.
“Hapana Konso hatuna maana hiyo!” alisema Sipe.
Itaendelea katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.