×

Mume: askofu anatishia…

Na Gladness Mallya, RISASI mchanganyiko

DAR ES SALAAM: KJN/8419/2016 KUTISHIA KUUA KWA MTANDAO ni RB iliyofunguliwa na Donald Kisanga (30) kwenye Kituo cha Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’ jijini Dar akimlalamikia Askofu Zefania Mollel wa Kanisa la Deliverance Assemblies of God lenye makao yake makuu, Maji ya Chai jijini Arusha kwamba anatishia kumuua huku mtumishi huyo wa Mungu akikanusha vikali na kufafanua.

TUANZE NA MLALAMIKAJI

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ofisi zilizopo Bamaga-Mwenge, Dar es Salaam, Kisanga alitoa sababu ya kumfungulia RB askofu huyo ambaye anajiita zaidi Nabii Zefania.

“Ni kwa sababu nimemtuhumu kuvunja ndoa yangu na mke wangu, Neema Jonas Mungure. Sasa nilipowasiliana naye kwamba, anirudishie mke wangu, akanitishia kuniua ndipo nikakimbilia polisi kutoa madai yangu,” alisema Kisanga.

ILIKUWAJE?

Kisanga: “Awali mimi nilikuwa nikiishi jijini Arusha na huyo mke wangu ambaye tulifunga naye ndoa Oktoba 20, 2012 kwenye Kanisa la KKKT Usharika wa Mjini Kati, Arusha. Ikafika mahali, mke wangu akaanza kwenda kuabudu kwenye kanisa hilo.

“Sikuona kama ni jambo baya mtu kuamua kumtafuta Mungu mahali f’lani. Hata mimi niliamua kumfuata japo tangu awali sisi ni washirika wa KKKT (Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania).”

NABII KWENDA NYUMBANI KWAKE

“Baada ya muda, nabii akaanza kuja nyumbani kwangu. Hilo pia sikuliona kama ni tatizo. Watumishi wa Mungu wengi tu huwa wanawatembelea waumini wao kwa ajili ya kuwatia moyo na pia kuwa nao karibu.”

JUNI MOSI, MWAKA HUU

“Kuna wakati alikuja nyumbani, akawa pale kwa muda. Nakumbuka ilikuwa tarehe 1 Juni, mwaka huu. Nikiwa natoka nyumbani kwenda kazini, nabii alikuwa nje nyumbani, akaniita.

“Niliporudi, akaniambia kwamba ameota ndoto mke wangu ametoroka nyumbani. Nilishtuka kidogo. Lakini nikamwambia huenda ni ndoto kwani mimi na mke wangu hatuna ugomvi wowote ule sasa atatorokaje?!”

JUNI 20, MWAKA HUU

“Nabii aliondoka zake kurudi kwake. Lakini ilipofika Juni 20, mwaka huu, nikiwa kazini, mama yangu mzazi ambaye alikuwa nyumbani kwangu alinipigia simu na kuniambia mke wangu amechukua mizigo yake, ameondoka nyumbani.

“Nilimuuliza mama kwa tatizo gani, akasema hata yeye hajui ila alimsikia mke wangu akisema eti kisa cha kuondoka alipata habari eti mimi nilimshika msichana wa kazi.

“Basi, nilirudi nyumbani na kukuta kweli mke wangu ameondoka pamoja na mtoto wetu na msichana wa kazi (hausigeli). Nilipompigia simu kumuuliza kisa alisema hayohayo eti nina uhusiano na msichana wa kazi. Na huyo msichana wa kazi mwenyewe aliletwa na yeye nabii.

“Sasa hapo ikumbukwe kwamba, ni siku ishirini tu tangu nabii aseme ameota ile ndoto yake kuwa mke wangu ametoroka. Mke wangu akawa amerudi kwao. Lakini kwao kwenyewe ni jirani na kanisa.”

MAWAZO YA NYUMA

“Nilirudisha mawazo nyuma sana. Nikawa nakumbuka nabii huyo ambaye ni askofu alivyokuwa akija nyumbani kwangu. Na mambo yalivyokuwa yakiendelea pale. Kwa hiyo nilipoanza kuwasiliana naye anirudishie mke wangu, akaanza kunitishia maisha, ndipo nikaenda kufungua RB.”

MENGI YANAFUNGWA NA DAWATI

Mambo mengi aliyoongea mlalamikaji huyo kuhusu mtumishi wa Mungu yanawekwa kwenye makabrasha ya gazeti hili.

SASA HUYU HAPA ASKOFU MWENYEWE

Baada ya kuzungumza na Kisanga, Risasi Mchanganyiko lilizungumza na mlalamikiwa ambaye alisema:

“Suala hilo sihusiki nalo, hao watu ni washirika wangu. Huyo mwanaume ana lengo tu la kuchafua kanisa, anataka kulivunja kabisa, nimeshachukua hatua za kisheria zaidi  siwezi kuongea sana kwani naye ananitishia maisha.”

ALIWAHI KUWASULUHISHA

“Waliwahi kuwa na mgogoro nikawasuluhisha ikashindikana, nimewaachia mdhamini wao. Sasa nashangaa ananihusisha, rafiki yake alinitobolea siri kwamba jamaa huyo ana lengo la kwenda kwenye vyombo vya habari kunichafua halafu alinitishia kuniua hivyo nasubiri kikosi kutoka Dar kije kiniue.

“Ndugu mwandishi wa habari hizo, tuhuma hizo si za kweli muwe makini na hilo suala siyo la kweli, ukweli anao mke wake (Neema), mimi nimeoa, nina watoto watatu, najiheshimu.”

 

MKE NAYE ANENA

Baada ya kuongea na mtumishi wa Mungu, Risasi Mchanganyiko lilizungumza na mke wa mlalamikaji ambaye alisema:

“Askofu hahusiki katika hili suala, mume wangu ndiye muhuni, anatembea na wasichana wa kazi na majirani,  anarudi nyumbani usiku wa manane.  Askofu nilimpelekea hitaji langu aniombee, akaniombea na hii kesi iko kwa mdhamini wa ndoa yetu na kila akimuita huyo mwanaume anamkimbia, yaani nitaenda kumfungulia mashtaka kwa kunichafulia jina langu maana huu mgogoro umeanza tangu mwaka 2013, haujaanza leo, nimeondoka kwa sababu ya uhuni wake na siyo kitu kingine.”