×

Yanga kupigwa faini ya Sh 28m

 

Omary Mdose, Dar es Salaam

IMEFAHAMIKA kuwa, baada ya Yanga kuchelewesha kuwasilisha majina ya wachezaji wao watakaowatumia kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, timu hiyo italazimika kulipa faini ya dola 500 kwa kila mchezaji ambazo ni sawa na shilingi milioni moja.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Yanga imewasilisha majina ya wachezaji 28 kwa ajili ya msimu ujao, lakini ilikuwa nje ya muda uliopangwa. Hivyo jumla watatakiwa kutoa zaidi ya Sh milioni 28 kama faini.

Agosti 6, mwaka huu usajili wa wachezaji kwa timu za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili ulifungwa, ambapo Yanga na Coastal Union hazikuwasilisha kwa wakati majina ya wachezaji wao ndani ya TFF, jambo ambalo limezua mjadala.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya TFF, zimeeleza ni wazi Yanga na Coastal zitapigwa faini kwani tayari zimewasilisha barua ya utetezi kama walivyotakiwa kufanya kueleza kwa nini zimechelewesha majina ya wachezaji wao.

“Baada ya kuwataka walete barua za utetezi wao, tumezipokea, hivyo kinachofuata hapo ni lazima watapigwa faini na si kingine.

“Hapa Yanga imewasilisha majina ya wachezaji wao 28, hivyo watatakiwa kulipa dola 500 kwa kila mchezaji, sasa hapo ukifanya hesabu kwa jumla nadhani utapata hiyo faini ni kiasi gani cha fedha,” alisema mtoa taarifa hiyo.

Championi lilimtafuta Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa kuzungumzia hilo, simu yake iliita bila ya kupokelewa, lakini Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema ni wazi timu hizo zitapigwa faini kutokana na kanuni zilivyo japo hakufafanua ni kiasi gani.