WAKATI naanza kuichezea Simba mwaka 2,000, niliikuta hali ya timu hiyo haikuwa nzuri kiuwezo, ilikuwa imepita miaka minne haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Simba ilitwaa ubingwa wa Bara mwaka 1995, baada ya hapo ufalme ukawa ni wa Yanga iliyotwaa ubingwa mara tatu mfululizo, lilikuwa pigo kubwa kwa Wanasimba.
Kila tulipokatiza kicheko kilikuwa ni kwa Wanayanga tu, ilituuma sana, wanaofuatilia soka kwa ukaribu hasa upinzani wa Simba na Yanga wanaweza kunielewa vizuri.
Mwaka 2001 uongozi wa Simba ukamwajiri kocha kutoka Kenya, James Aggrey Siang’a ambaye hakuwa na jina kubwa hapa nchini.
Siang’a alikuta Wanasimba wamekata tamaa kwa kuwa baada ya Yanga kutwaa taji mara tatu kilichofuata ni Mtibwa Sugar kutwaa mara mbili mfululizo, hivyo ikawa imepita miaka mitano Simba haijatwaa ubingwa.
Taratibu Siang’a akaanza kazi na kupewa ushirikiano na viongozi wa Simba. Katika msimu wake wa kwanza tu akaipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ilionekana kama maajabu kwa jinsi ambavyo Simba walivyokuwa wakiusubiri ubingwa huo.
Huo ulikuwa mwanzo tu, Siang’a akaendela kufanya vizuri zaidi na zaidi, sikumbuki mataji mangapi aliipa Simba lakini yalikuwa ni mengi na kwa ufupi heshima ya Simba ikarejea na kuwa juu zaidi ya ilivyokuwa awali.
Kizuri zaidi Siang’a aliiwezesha Simba kufuzu hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2003 kwa kuiondoa Zamalek ya Misri ambao ndiyo waliokuwa mabingwa watetezi.
Siang’a ambaye alifariki Ijumaa iliyopita Septemba 9, 2016 akiwa Bungoma nchini Kenya baada ya kuugua kwa muda mrefu, ameacha historia kubwa na kuna mengi ya kumzungumza.
Nimeamua kushea na wewe msomaji mambo kadhaa ya kukumbukwa kuhusu marehemu Siang’a.
Wasifu wake kwa ufupi
Aliwahi kucheza katika timu za Gor Mahia, Luo Union na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars akiwa kipa, mbali na kuifundisha Simba, pia aliwahi kuwa mwalimu wa Moro United, Express ya Uganda na Gor Mahia ya Kenya.
Siang’a aliidakia Kenya katika Kombe la Mataifa ya Afrika 1972, alikuwa kocha wa Harambee Stars mwaka 1999 na 2000.
Alitengeneza timu kuwa familia
Akiwa Simba alikuwa ni zaidi ya kocha kwa wachezaji, alikuwa kama baba yetu, alitulea vizuri na hakutaka makundi ndani ya timu, uwepo wake ulisababisha vijana wengi kuwa na kiwango bora na kutengeneza timu ambayo baadaye ilikuwa tishio.
Nakumbuka katika kikosi chake baadhi ya wachezaji ni mimi Matola, Victor Costa, Ulimboka Mwakingwe, Emmanuel Gabriel, Lubigisa Madata, Primus Kasonzo, Christopher Alex, Said Swedi, Ramadhani Wasso, Boniface Pawasa, Shekhan Rashid na Athumani Machuppa.
Unajua tena mambo ya vijana, kuna wakati alikuwa akitatua matatizo ya wachezaji ambayo yapo ndani ya uwezo wake bila kuhusisha viongozi.
Mfano ilipotokea mchezaji amekiuka kanuni za klabu au kuonyesha utovu wa nidhamu, alimuita na kuzungumza naye kisha kuyamaliza yeye mwenyewe wakati angekuwa kocha mwingine lazima aripoti kwa viongozi na unavyowajua viongozi wa Bongo mambo yanakuwa makubwa kwa kitu kidogo tu.
Kuna wachezaji walikuwa wakitoroka kambini kwenda kustarehe, alipogundua aliwaita na kuwakanya pasipo kuhusisha viongozi.
Avaa boksa tu baada ya kufungwa
Kuna tukio nalikumbuka mpaka leo, kuna mechi tulicheza dhidi ya Nkana FC ya Zambia, tulikuwa na kikosi kizuri sana na matumaini ya kushinda yalikuwa makubwa, lakini katika mchezo huo tukafungwa mabao 3-0.
Siang’a hakuamini kilichotokea, wakati akitoka uwanjani alikuwa na hasira sana, hakupenda kufungwa kabisa, waandishi wakamfuata wakiwa wamemzunguka, hakutaka kuzungumza, wao wakaendelea kumfuata, alipoona wanamsumbua zaidi, akaipiga kamera moja kwa hasira na akataka kumvaa yule mpigapicha, watu wakamuwahi wakamzuia.
Tulipofika kambini akaingia chumbani kwake na kujifungia, baadaye akaniita mimi kwa kuwa nilikuwa nahodha, nikaenda chumbani kwake, nilipoingia nikamkuta amelala kitandani akiwa na boksa tu, akaanza kuniuliza sababu za kufungwa 3-0.
Tukazungumza lakini akili yake haikuwa sawa, tulikaa siku mbili kule Zambia, alishindwa kula vizuri kabisa mpaka tulipoondoka na kurejea Dar, hiyo ilikuwa ni katika Klabu Bingwa Afrika.
Alipigwa na askari wa morogoro nusu kifo
AMES Aggrey Siang’a alikuwa ni kocha mwenye misimamo, alikuwa na hasira na hakutaka kuyumbishwa au kuona yeye au mchezaji wake akionewa.
Ilikuwa Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri tunacheza dhidi ya Polisi Morogoro, sasa kwa kuwa kipindi hicho tulikuwa na upinzani mkali na timu hiyo, siku ya mechi kulikuwa na askari polisi wengi sana uwanjani.
Tukajua zile ni mbinu za kutumaliza kisaikolojia lakini sisi tulitulia na kuonyesha uwezo mzuri tu, mwisho wa mchezo tukashinda mabao 2-0, huku kukiwa na vurugu za hapa na pale.
Wakati mchezo umeisha kukatokea mabishano kati ya beki wetu, Boniface Pawasa na Ali Moshi wa Polisi Moro, mimi nikaenda kuamua ule mzozo, wakati nawaamua kuna mchezaji wa Polisi akanipiga ngumi ya mgongo.
Kumbe wakati ananipiga, mchezaji wetu Madaraka Selemani alimuona na yeye akamtandika ngumi yule aliyenipiga mimi.
Kuona hivyo, basi wale askari waliokuwa nje ya ‘pitch’ wakaingia uwanjani wakaanza kumkimbiza Madaraka ili wampige, akakimbia lakini alifika sehemu akawa anarudi kinyumenyume, kumbe kuna askari alikuwa amevaa kiraia na ameshika rungu anamvizia Madaraka ambaye alikuwa akisogea upande wake ili amtandike na lile rungu.
Wakati yote hayo yakitokea Siang’a aliyaona, wakati yule askari akijiandaa kunyanyua rungu ampige Madaraka, Siang’a alitoka mbio moja kwa moja akamrukia yule askari aliyevaa kiraia, alimpiga kichwa cha hatari kama vile anaunganisha krosi.
Hasira zote za wale askari zikageukia kwa Siang’a, wakaanza kumpiga, walimpiga sana, baada ya pale alikimbizwa hospitali na kulazimika kushonwa nyuzi nyingi tu, kwa kuwa alikuwa ni mtu wa mazoezi na yupo imara, ndicho kilichomsaidia vinginevyo alikuwa apoteze maisha palepale kwa kile kipigo alichokipata.
Pamoja na kipigo kile, unajua nini kilitokea kwa yule askari aliyepigwa kichwa? (Matola anacheka) Daaa! Alizimika palepale uwanjani, ikabidi akimbizwe hospitali na kugundulika kuwa alikuwa amezimia na amepata maumivu makali ya kichwa.
Kesho yake Mkuu wa Jeshi la Polisi Morogoro akakutana na viongozi wa Simba na wale askari wakazungumza na kuyamaliza kwa kuwa yalikuwa ni masuala ya mpira tu!
Enyimba noma, walimfanyia kitu kibaya
Kuna siku tulienda Nigeria kucheza dhidi ya Enyimba, tulifika siku nne kabla ya mchezo huo. Siang’a alikuwa na kawaida ya kuzungumza na wachezaji mida ya saa sita mchana siku ya mechi, alikuwa akielezea mipango na kutaja kikosi.
Siku ya mchezo huo mpaka kufikia saa nane alikuwa bado kalala tu chumbani kwake, ilipofika saa tisa ikabidi twende na viongozi kujua kulikoni, tulipofika tukamkuta hajiwezi yupo hoi kitandani, akilalamika kuumwa ghafla na mkono mmoja ukawa haufanyi kazi.
Ikabidi nipewe mimi ile listi na maelekezo kadhaa nikaenda kuwaambia wachezaji. Muda wa mchezo alienda uwanjani lakini alikuwa yupoyupo tu hakufanya chochote, tukapigwa mabao 3-0. Ikaonekana kama Wanigeria wamemfanyia kitu.
Alikuwa kiboko ya Yanga
Nakumbuka Yanga walikuwa hawamsumbui kabisa, kwenye mechi nyingi tuliwafunga au kupata sare wakati kabla ya hapo Yanga walikuwa wakiionea sana Simba.
Amtandika kichwa Micho
Tukio lingine ni kwamba Siang’a aliwahi kumpiga kichwa aliyekuwa Kocha wa SC Villa, Milutin Sredejevic ‘Micho’ raia wa Serbia katika fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Simba ikilala kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda.
Micho alikwenda katika benchi la Simba kumsalimia Siang’a aliyekuwa ana hasira za kipigo na kukosa kombe lakini akaambulia maumivu.
Afichua tuhuma za rushwa
Alipoondoka Simba, Siang’a aliwahi kufichua mpango wa kiongozi mmoja wa juu wa klabu wa wakati huo kutaka kumshawishi kupokea kitu kidogo kutoka kwa Zamalek ili alegeze kamba, ilikuwa mwaka 2003 lakini alikataa.
Aidha, kuna kipindi aliwahi kutoa ripoti maalum akidai rushwa imekithiri katika soka la Tanzania, hakutiliwa maanani sana yawezekana aligusa maslahi ya vigogo wa soka.
Makocha wa Simba tangu mwaka 1998
MWAKA JINA NCHI
1998: Mohamed Kajole Tanzania
1999: David Mwamaja Tanzania
2000: Nzoyisaba Tauzany Burundi
2000: Abdallah Kibaden Tanzania
2000: Syllersaid Mziray Tanzania
2001: James Siang’a Kenya
2005: Patrick Phiri Zambia
2006: Neider dos Santos Brazil
2007: Talib Hilal Tanzania
2010: Milovan Cirkovic Serbia
2010: Patrick Phiri Zambia
2011: Krasmir Benziski Bulgaria
2012: Moses Basena Uganda
2012: Milovan Cirkovic Serbia
2012: Partick Liewing Ufaransa
2013: Abdallah Kibaden Tanzania
2013: Zdravko Logarusic Croatia
2014: Patrick Phiri Zambia
2015: Goran Kopunovic Serbia
2015: Dylan Kerr England
