Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Kebwe, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Darasa la Fursa linaloendeshwa na Clouds Media mapema jana kwenye ukumbi wa Midland Msamvu, Morogoro.
Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, akiwapa mbinu baadhi ya wakazi wa Morogoro za kujikwamua kimaisha kwa kutumia fursa zilizopo mkoani hapo.
Mkuu wa Chuo cha Mlimani Professional, Hassani Ngoma, akiwaeleza wakazi wa Morogoro namna alivyofanikiwa kimaisha.
Msanii wa muziki wa Hip Hop, Bongo Nikki wa Pili (kushoto) akiongea jambo kwa wakazi wa Morogoro juu ya kutumia fursa za mkoa huo ili kufanikiwa kimaisha.
Kebwe (katikati), akiongea jambo na Ruge baada ya kuwasili ukumbini hapo.
Baadhi ya wafuatiliaji wa semina hiyo wakimsikiliza mmoja wa watoa mada.
Sehemu ya wakazi wa Morogoro waliojitokeza kujifunza kwenye darasa la ‘Fursa’ jana.
Kebwe akiagana na Ruge Mutahaba.
MKUU wa mkoa wa Morogoro Stephen Kebwe, mapema jana alipata muda wa kuwakaribisha na kuwapokea wazungumzaji wa Darasa la Fursa ambalo limekuwa likifanyika kila mkoa ambapo tamasha la Fiesta linafanyika.
Kebwe aliipokea timu nzima ya fursa ndani ya ukumbi wa Midland uliyopo maeneo ya Msamvu mjini Morogoro, ambapo alienda kulifungua darasa hilo na kuwashuhudia baadhi ya wakazi wa mkoa wake walivyojitokeza kusikiliza na kuonyeshwa namna ya kutumia rasilimali za mkoa huko katika kujikwamua.
Akizungumza mara baada ya kuingia katika ukumbi huo, Kebwe alisema kuwa amefurahishwa sana na timu ya Fursa na hasa Clouds Media Group kwa kuwafikishia tamasha la Fiesta ambalo kwake anaamini lina mchango mkubwa sana kwa wananchi wake hasa katika kuongeza kipato na kuwafanya wananchi wake kwa aslilimia kubwa kutumia fursa hiyo kujifunza mambo mengi.
“Nimpongeze sana Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, kwa kutambua umuhimu wetu na kuamua kutuletea tamasha la Fiesta likiwa limeambatana na darasa la Fursa. Natambua watu wengi hawaelewi umuhimu wa darasa hili ila kwangu mimi ninajua wananchi wangu watajifunza kupitia Fursa maana kama ilivyo kaulimbiu yake ni kweli kabisa watu wataongeza thamani kwa kupitia mafunzo haya,” alisema Kebwe.





