INASIKITISHA SANA: Binti mmoja ambaye ni model na mwimbaji wa muziki wa Bongofleva na ngoma za asili aliyetambulika kwa jina la Juliana Issa (22) maarufu kama JULIANA ISAWAFO (pichani) ambaye picha yake ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia jana ikionyesha mwili wake ukiwa umetupwa eneo la Ndoro katika majaluba ya mpunga mita chache kutoka barabara ya Moshi–Arusha nje kidogo ya Chuo Kikuu cha Makumira, Arusha huku akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili baada ya kudaiwa kubakwa na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jana kuwa upelelezi wa awali unaonyesha aliuawa baada ya kupigwa, kubakwa na kunyongwa kisha kutupwa eneo la Makumira, Kata ya Usa River wilayani Arumeru.
“Jana (juzi) saa tano tuliokota mwili wa Juliana ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali kuashiria alipigwa, pia mikwaruzo ya kucha shingoni na amevimba sehemu za siri kuashiria kwamba kabla ya kuuawa walimbaka kisha kumnyonga,” alisema Mkumbo.
Mmoja wa Viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, (jina lake halikufahamika mara moja) amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kusema kuwa ameokotwa majira ya saa tano asubuhi jana akiwa amekufa na mwili wake kutelekezwa kwenye shamba la mpunga nje kidogo ya eneo la chuo hicho.
Mbali na kuthibitisha kifo hicho, kiongozi huyo ameeleza pia kuwa, msichana huyo ni mwanafamilia wa Chuo cha Makumira ila hakuwa mwanafunzi rasmi kama watu wanavyodai.
Ameongeza pia kuwa, msichana huyo alikuwa akiishi ndani ya eneo la chuo kwa Mzungu mmoja ambaye ni mmoja wa walimu wa Sanaa chuoni hapo.
Mwisho akaeleza hisia zake namna ambavyo familia ya chuo hicho ilivyoguswa na msiba huo kwani msichana huyo alikuwa kama dancer wa matamasha mbalimbali ya Chuo cha Makumira.
Kamanda Mkumbo alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Mount Meru, huku watuhumiwa wakisakwa.
Audio: Sikiliza Mahojiano | Msichana Abakwa Hadi Kufa Makumira University, Arusha
