
Mgombea wa urais wa chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump amelazimika kuondolewa jukwaani kwa muda na walinzi wake baada ya kuwepo taarifa za mtu mwenye silaha aliyetaka kumdhuru katika mkutano wake wa kampeni mjini Nevada.
Wafuasi wa Trump wameeleza kuwa walinzi wake walifanikiwa kumuondoa jukwaani licha ya hofu kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa amejihami kwa silaha miongoni mwao.
Mpinzani wa Trump, Hillary Clinton.
Trump alikuwa anakaribia kilele cha hotuba yake ndani ya ukumbi wa Reno, Nevada uliyojaa wafuasi wake kabla ya kutokea sintofahamu hiyo karibu na jukwaa.
Wafuasi wake waliojawa na hofu walianza kukimbilia katika lango kuu la kutokea kwenye ukumbi huo kufuatia madai ambayo hayakuthibitishwa.
Polisi wamemkamata mtu mmoja kufuatia tukio hilo lakini aliachiwa huru muda mfupi baadaye baada ya kutopatikana na silaha kama ilivyodaiwa.
Tukio hilo limetokea zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.
