DAR ES SALAAM: CHAMA Cha Muziki wa Disco Tanzania (TDMA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kesho kinatarajia kuzindua mashindano ya taifa ya ma-dj saa 3:30 usiku.
Katibu Mkuu wa TDMA Taifa, Asanterabbi Mtaki (katikati) akizungumza na wanahabari.
Uzinduzi huo utafanyika katika Ukumbi wa JM Night Club uliopo Tip Top Manzese jijini Dar, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Ofisa Michezo wa mkoa wa Dar, Adorph Halii.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TDMA Taifa, Asanterabbi Mtaki amesema uzinduzi huo utaambatana na mashindano ya raundi tatu za mtoano wa Ma-Dj, ambapo raundi ya kwanza itafanyika kesho Novemba 18 ya pili Novemba 25 na ya tatu Desemba 2 mwaka huu ambapo washindi watakaoingia robo fainali watawakutanishwa na Ma-DJ mahili toka wilaya tatu za Temeke, Ilala, Kinondoni, Ubungo na Kigamboni .
Amesema mashindano hayo yatawawezesha Ma-Dj wajitambue kuwa wao ni kundi muhimu katika jamii ya watanzania ambao ni wapenzi wa muziki.
“Lengo la mashindano haya ni kuwahamasisha wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake kupanda miti, maua na kuyatunza mazingira yanayowazunguka kwa kuyaweka katika hali ya usafi na kuvutia” alisema.
Aidha alisema vigezo vya mashindano hayo ni nidhamu, uadilifu, umahiri wa kuchezesha nyimbo na kuzichanganya, kulitawala jukwaa la DJ, kuonyesha kazi za kutumia mikono ambapo kila DJ atapewa muda usiopungua dakika kumi.
Mashindano hayo yatawafanya Ma DJ kupata mbinu mbalimbali ambapo pia kutakuwa na zawadi kwa msindi wa kwanza kujipatia Shilingi laki tano, mshindi wa pili Shilingi laki tatu na wa tatu shilingi laki mbili na watakaoibuka washindi watakuwa mabalozi wa mazingira wa mkoa wa Dar es Salaam
Na Denis Mtima/Gpl