Makala: Imelda Mtema | Risasi Jumamosi
ELIAS Barnaba, moja kati ya ‘mafundi’ wazuri wa Muziki wa Bongo Fleva. Anaujua ‘kuufinyanga’ muziki kadili anavyotaka. Ni mtunzi mahiri na muimbaji. Kwa sasa anasumbua na Wimbo wa Lover Boy.
Hapa chini amekutana uso kwa uso na Risasi Jumamosi ndani ya studio yake iliyopo maeneo ya Mwananyamala jijini Dar, mambo yalikuwa hivi:
Barnaba akiwa kwenye studio yake.
Risasi: Tumesikia kwamba huu wimbo unakugusa wewe mwenyewe kwa maana ya wewe ni muaminifu kuna ukweli wowote?
Barnaba: Huu wimbo niliimba kwa mfano wa mimi mwenyewe lakini unazungumzia watu zaidi ya kumi kwa sababu sasa hivi watu wengi kwenye mapenzi siyo waaminifu wengine wanajifanyisha.
Risasi: Kivipi, unaweza kufafanua kidogo?
Barnaba: Sasa hivi unamkuta mwanaume anayempenda msichana lakini ni muhuni tu na si mwenye mapenzi ya dhati, wengi wapo kwa ajili ya haja zao halafu basi, sasa nilikuwa najaribu kuzungumza kuwa kuna wengine ni wanaume sahihi siyo wote wazugaji.
Risasi: Kwa sasa unamiliki studio kubwa ya kwako mwenyewe lakini ni changamoto gani umepitia mpaka hapa ulipofikia?
Barnaba: Kwa kweli changamoto ni kubwa, kwanza nilianza kuweka studio kwenye korido nikaitoa nikaiweka sebuleni mara wenye nyumba hawataki makelele yaani ni shida tupu mpaka nikapata akili ya kuweza kutafuta nyumba yenye nafasi ya kutosha na sasa niko vizuri kabisa.
Risasi: Kwa nini mara nyingi gitaa lako huliachi hata unapokuwa matembezini?
Barnaba: Gitaa limekuwa ni moja ya maisha yangu ya kila siku na mwanamuziki wa kweli kabisa lazima apende gitaa kwa sababu linakuwa na hisia za muziki wa ndani kabisa, kwa kweli kwangu mimi bila hilo naona sijafanya kitu.
Risasi: Kutokana na kazi yako ya muziki pia na kusimamia studio ni kwamba unaweza kukesha, vipi kuhusu familia yako na maanisha mkeo hana tatizo na hilo?
Barnaba: Kwanza huwa sikeshi studio lakini nagawa muda wangu vizuri kwa familia yangu na wao wenyewe wanajua wazi kazi yangu.
Risasi: Video ya wimbo wako wa Awalade uliomtumia mkeo kama ‘video queen’, ndiyo kusema na yeye unamuingiza kwenye mambo ya muziki taratibu?
Barnaba: Hapana, hilo silitaki hata hiyo ilitokea bahati mbaya, sitaki ajiingize kwenye muziki ndiyo maana niliamua kuishi naye, awe msaidizi wangu katika familia kuhusu kujiingiza kwenye muziki hapana.
Risasi: Vipi kuhusu mtoto wako Steve, ungependa naye aje kuwa mwanamuziki?
Barnaba: Ninachopenda mtoto wangu afanye kazi inayoendana na jamii kama atakuwa daktari basi atasaidia wengine kupona, kama rubani atasaidia watu kusafiri na kama mwalimu atasaidia wengine kujifunza chochote cha jamii afanye tu.
Risasi: Ni mafanikio gani umeyapata mpaka hivi sasa?
Barnaba: Mafanikio ni mengi, nimetengeneza mtandao wa watu kunifahamu na kubwa zaidi kuwa tegemezi kwa watu kwa sababu mimi ni mwanamuziki, mtunzi, mwalimu na vitu vingi kuhusiana na muziki.
Risasi: Ulitamani kufanya nini utakapokuwa na mafanikio?
Barnaba: Nilitamani mama yangu angekuwepo leo hii kuona mafanikio yangu kwa sababu alinisaidia sana.
Risasi: Nini matarajio yako ya sasa?
Barnaba: Natarajia kutoa albamu mwishoni wa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao.
Risasi: Siku za hivi karibuni wanamuziki wengi hawataki kutoa albamu unafikiria ni kwa nini?
Barnaba: Unajua hakuna kitu kipya na pia hakuna ulinzi wa kuweza kufanya watu wasitoe kopi lakini kwa upande wangu najua nitafanyaje ili kudhibiti.
Risasi: Nakushukuru sana Barnaba
Barnaba: Asante karibu.


