Mshambuliaji wa timu ya vijana ya Mbao FC U-20 ya mkoani Mwanza, Ismail Mrisho Khalfan anayevalia jezi nambari 4 amefariki dunia jana jioni baada ya kuanguka uwanjani Kaitaba wakati wa mtanange wao dhidi ya timu ya vijana wa Mwadui FC ya Mkoani Shinyanga, ikiwa ni mechi ya mwisho ya kumaliza duru la kwanza la Ligi ya Vijana.Ismail Khalfan alifariki baada ya kufikishwa Hospitali ya Serikali ya mjini Bukoba.
Ismail kabla ya kukumbwa na umauti aliweza kuifungia timu yake bao la kwanza na bao la pili lilifungwa kwa mkwaju wa penati hivyo mtanange kumalizika kwa 2-0.
Kabla ya kuanguka, Ismail aligongana na beki wa Mwadui FC na baadaye akiwa peke yake alianguka chini lakini akainuka halafu akaanguka tena na kutokana na ukosefu wa huduma ya kwanza na gari la wagonjwa katika Uwanja wa Kaitaba kulipelekea marehemu kupandishwa kwenye gari la zimamoto na kupelekwa hospitali ambapo mauti yalimkuta.
“Alianguka uwanjani ghafla baada ya kufanyiwa faulo mguuni akainama kushika mguu tukamuona ameshika kifua akaanguka chini lakini wakati anaanguka alikuwa peke yake”, ni maneno ya meneja wa Mbao FC, Bashiri wakati akizungumza na kituo kimoja cha radio cha mkoani Dar es Salaam.
“Tukajaribu kumsaidia kumpatia huduma madaktari wa timu zote pamoja na msalaba mwekundu tukasaidiana kumpeleka hospitali.”
“Wakati huo timu yetu ilikuwa ikiongoza kwa goli 1-0 goli lililofungwa na marehem Ismail Khalfan na jingine lilifungwa wakati mimi sipo nikiwa nimeenda hospitali.”
Aidha madaktari waliokuwa wakimtibu hospitalini hapo hawajatoa ripoti kamili kueleza chanzo cha kifo hicho ama ni eneo gani la mwili wa marehemu lilidhurika hadi kupelekea umauti wake.
Mwili wa marehemu Isamil unatarajiwa kusafirishwa leo Desemba 5, kwenda nyumbani kwao mkoani Mwanza kwa ajili ya mazishi.
Global Publishers inapenda kutoa pole kwa Mbao FC na wapenzi wote wa soka pamoja na wachezaji kwa kufikwa na msiba huo mkubwa.

