CARRIE FISHER aliyekuwa mcheza sinema maarufu wa kike wa Marekani akiwa amevuma zaidi katika filamu ya Star Wars alipotumia jina la Princess Leia Organa, amefariki baada ya kukumbwa na shambulio la moyo. Mwigizaji huyo alikuwa na umri wa miaka 60.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa familia ya marehemu, Simon Halls, kwa niaba ya binti wa Fisher aitwaye Billie Lourd mwenye umri wa miaka 24, ilisema:

“Ni kwa masikitiko makubwa Billie Lourd anathibitisha mama yake mpendwa, Carrie Fisher, amefariki asubuhi ya leo.
“Marehemu alikuwa anapendwa na walimwengu wengi na hivyo watamkosa na kumkumbuka kwa muda mrefu. Familia yote inawashukuru watu wote kwa hisia zao na sala zao katika tukio hili.”
Fisher alikuwa anatoka London kwenda Los Angeles siku ya Ijumaa, Desemba 23 ambapo alipatwa na tatizo hilo la moyo na ikabidi ashushwe kwenye ndege na kupelekwa hospitali ya karibu ambako alipewa matibabu na baadaye kufariki.
Fisher aliyetokana na familia ya waburudishaji kwa baba na mama yake, alikulia katika mazingira ya uigizaji wa filamu, michezo na masuala ya televisheni.
Akiwa ameachana na shughuli za filamu za Hollywood mwaka 1973, alijiunga na chuo cha utoaji hotuba na uigizaji cha London, Uingereza, alikokaa kwa mwaka mmoja. Ujuzi alioupata ndiyo ulimfanya hadi akashiriki filamu maarufu ya ‘Star Wars’ mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 19 tu.
Pamoja na kushiriki filamu hiyo sehemu zote tatu za Star Wars, pamoja na ile ya mwaka jana ya The Force Awakens, Fisher alishiriki akiwa nyota katika sinema zilizotoka miaka ya 1980 ambazo ni The Blues Brothers, The Man with One Red Shoe, Woody Allen’s Hannah and Her Sisters mwaka 1986 na baadaye, When Harry Met Sally.
Pamoja na umaarufu wote alioupata maishani mwake, Fisher alikuwa anavuta bangi na kutumia madawa ya kuleva, vitu ambavyo alivianza akiwa na umri wa miaka 13 tu.
Mwigizaji huyo aliolewa na mwanamuziki Paul Simon mwaka 1983. Billie Lourd, mtoto pekee wa Fisher, alizaliwa mnamo Julai 1992. Billie ambaye naye kama mama yake alikuwa nyota katika filamu ya The Scream Queens, baba yake alikuwa Bryan Lourd aliyekuwa mpenzi wa Fisher kwa miaka mitatu baada ya kuachana na Paul Simon. Hivi sasa Billie ameolewa na Bruce Bozzi.
Fisher amemwacha mama yake aitwaye Reynolds, binti yake Lourd, kaka yake Todd Fisher, dada wa kambo Joely Fisher na Tricia Leigh Fisher, na mbwa wake mpendwa wa Kifaransa aitwaye Gary.