Kamishna wa Kanda Maalum Dar es Salaam, CP Simon Sirro, akisoma taarifa.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Diana Masala, akizungumza jambo kuhusiana na jinsi walivyoshirikiana na jeshi la polisi kukamata wakwepa kodi.
Kamanda Sirro akionyesha mitambo ya kuvutia shisha waliyoikamata.
…Akionyesha baadhi ya silaha walizokamata katika matukio mbalimbali.
DAR ES SALAAM: Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Simon Sirro, amewaasa Watanzania kuwa watulivu wakati wa kuukaribisha mwaka mpya na waepuke kuvunja sheria kwa kuchoma matairi na kupiga milipuko.
Sirro aliyasema hayo leo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu shamra za kuukaribisha Mwaka Mpya zitakazofanyika kesho usiku.
“Jeshi la polisi litakuwa macho katika kufuatilia hilo na kila ambaye atahusika na ukiukaji huo wa maagizo, hatutosita kumchulia hatua za kisheria. Hivyo tunaomba watu wawe huru kwa kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha kutoka katika makundi yote ya ulinzi maana tutashirikiana nayo yote yakiwemo makampuni ya ulinzi shirikishi,” alisema Sirro.
Aidha kamanda huyo aliongeza kuwa wanashukuru kwa operesheni kubwa waliyoifanya toka mwaka huu uanze mpaka unapomalizika kwani wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza uhalifu.
Vilevile alieleza kuwa kwa kipindi cha kuanzia Januari 2015 hadi Novemba jumla ya matukio ya mauaji yalikuwa 327 ukilinganisha na kipindi kama hicho cha Januari 2016 hadi Novemba ambapo matukio hayo yamepungua na kufikia 291 ambayo ni sawa na asilimia 11.
“Matukio ya ulawiti mwaka 2015 yalikuwa 310 ikilinganishwa na ongezeko katika kipindi kama hicho cha Januari hadi Novemba 2016 ambapo kuna ongezeko la matukio 73 na hiyo inatokana na kwamba idadi ya madawati ya masuala ya watoto kuripoti matukio hayo imeongezeka tofauti na ilivyokuwa nyuma,” alisema.
Alisema sababu za kuongezeka au kupungua kwa matukio hayo kumetokana na juhudi za Polisi Kanda Maalum kuzuia na kupambana na uhalifu kwa kufanya doria na misako mbalimbali iliyosababisha kukamatwa kwa wahalifu wa makosa mbalimbali.