DERICK LWASYE, Mbeya
SHINDANO la Shinda Nyumba na Global Publishers awamu ya pili, limepokelewa vizuri na wasomaji wa magazeti ya Global Publishers, kampuni namba moja ya uchapishaji wa magazeti Tanzania.
Hii ni mara ya pili kwa shindano hili la shinda nyumba kufanyika, huku awamu ya kwanza akipatikana mshindi wa mjengo wenye thamani ya mamilioni kutoka mkoani Iringa, Nelly Mwangosi.
Wasomaji wa Mbalizi wakichangamkiaMagazeti ya Global Publishers ili kujaribu bahati yao ya Kushinda Nyumba.
Wakizungumza na Championi Jumatatu wakati wa promosheni ya shindano hilo iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya viunga vya Jiji la Mbeya, wasomaji hao walisema wana uhakika na kile kinachofanywa na Global Publishers.
“Siyo siri ninyi jamaa mko vizuri sana na hamna magumashi kwenye bahati nasibu zenu, hivyo nimejipanga kununua kopi nyingi za magazeti ya Global Publishers ili nijitengenezee mazingira mazuri ya kuibuka mshindi,” alisema Mussa Hassan ambaye ni Dereva Bajaji kwenye Kituo cha Kabwe.

Rodrick Robin, maarufu kama mzee wa Ijumaa Wikienda, alisema huu ndiyo wakati wa kujaribu bahati yake kutokana na kuwa mteja mzuri wa gazeti hilo ambalo huwa limesheheni hadithi zenye msisimko.
Wakazi wa Mwanjelwa wakichangamkia Shinda Nyumba.
“Nimekuwa mteja wa muda mrefu wa magazeti ya Global Publishers ila nilikuwa sitilii maanani mashindano yaliyokuwa yakiendeshwa kutokana na kutoamini kama mshindi anapatikana bila kupangwa, ila baada ya kuona mshindi wa awamu ya kwanza kapatikana kutoka Iringa, tena ni mwanamke mjasiriamali, nikashawishika sana na sasa tutakula sahani moja mpaka kieleweke,” alisema Robin.
Katika eneo la Nanenane ambapo ndiyo kuna stendi ya mabasi ya wilayani na mikoani, wasomaji wa magazeti ya Global Publishers walionekana kufurahia awamu hii ya pili ya Shinda Nyumba na Global Publishers.
Kwa upande wao wauza magazeti wa Jiji la Mbeya na nyanda za juu kwa ujumla, wamewataka mawakala wa magazeti ya Global Publishers kuagiza nakala nyingi ili kuepusha usumbufu kama ulivyojitokeza awamu ya kwanza ya shindano hili.
“Unajua shindano hili ni kubwa sana hapa Tanzania, hivyo kila mtu atataka kujaribu bahati yake, tunawaomba mawakala wajitahidi kuagiza nakala za kutosha ili kuwaondolea usumbufu wasomaji na wateja wetu, msimu uliopita kulikuwa na uhaba wa nakala, hivyo kuna baadhi ya wasomaji walikuwa wanakosa nakala.”
Maeneo mengine ambayo promosheni hiyo ilifanyika ni Mbalizi, Uyole, Mwanjelwa, Soweto, Iyunga na Sokomatola.